MSAJILI AIONYA CHADEMA KUHUSU KUANZISHA KAMBI YAKE YA MAFUNZO...

John Tendwa.
Msajili  wa  Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, ameionya Chadema, kwamba isithubutu kuanzisha kambi za mafunzo ya kulinda amani kwa kuwa hatua hiyo si sahihi.

Tendwa ametoa onyo hilo katika taarifa kwa vyombo vya habari, iliyotolewa jana kwa niaba yake na Ofisa katika ofisi yake, Rajab Juma.
Alisema uamuzi wa Chadema kutaka kuanzisha kambi za mafunzo ya kulinda amani si sahihi na kuonya kuwa chama chochote kitakachojaribu, atakichukulia hatua, ikiwamo kukifuta.
Taarifa hiyo ilifafanua kwamba, Katiba ya nchi imempa jukumu kila mwananchi kulinda amani na usalama wa nchi na kujilinda mwenyewe na mali zake.
Fursa hiyo kwa mujibu wa Tendwa, inamtaka mwananchi kutoa taarifa katika vyombo vya Dola pale anaposikia au kuona mtu anataka kufanya au anafanya uhalifu au amemdhuru mtu.
Alisema kusudio la Chadema lilitangazwa na Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe bila kuwasiliana na taasisi husika ikiwamo Ofisi ya Msajili, ili kupata ushauri kuwa jambo wanalotaka kufanya ni sahihi.
"Katiba ya nchi na za vyama vya siasa, hazitakuwa na maana, kama kila mwananchi au kikundi, wataruhusiwa kufanya mafunzo ya kijeshi au ukakamavu. 
 "Jukumu la vikundi kama hivi, ni kutoa taarifa kwa vyombo vya Dola na si kupambana na wahalifu au watu wanaotaka kuwadhuru, na wenye jukumu la kupambana na wahalifu ni vyombo vya ulinzi na usalama, ambavyo vipo kisheria, mojawapo ikiwa ni Jeshi la Polisi," alisema  Tendwa katika taarifa hiyo. 
Alikitaka chama hicho na vyama vingine vinavyofikiria  au kufanya jambo hilo, kuacha mara moja kwani kufanya hivyo ni kukiuka sheria za nchi ikiwamo Sheria ya Vyama  vya Siasa ya 1992.
Alisema sheria hiyo inakataza chama cha siasa kuruhusu kutumika, kushabikia au kutumia nguvu kufanikisha malengo yake ya kisiasa.
Tendwa alisisitiza, kwamba chama cha siasa kutoa mafunzo ya kutumia nguvu kwa wanachama wake, ili kutekeleza jambo lolote ikiwamo kujilinda, ni moja  ya masuala yanayokatazwa  na Sheria  ya Vyama  vya Siasa.
Aliongeza kuwa kifungu cha (20) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, kinasema uamuzi wa Msajili ni wa mwisho na hauwezi kukatiwa rufaa mahakamani.
Kuhusu madai kuwa CCM wana kambi za mafunzo ya kupambana kwa vijana wake, Tendwa alisema madai hayo hayana msingi.
"Kama CCM  wanakiuka sheria ni jukumu la Chadema, kila chama na kila Mtanzania kutoa taarifa na ikiwezekana na ushahidi katika taasisi husika, ikiwemo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ili suala hili lishughulikiwe kisheria," alisisitiza.
Msajili  aliviasa vyama vya siasa kutumia muda wao kufanya shughuli za siasa ili kuchangia maendeleo ya nchi, badala ya kutumia uwezo wao na muda, kubuni mambo yanayoleta mtafaruku na kuhatarisha amani na utulivu wa nchi.
"Amani ikitoweka, vyama vya siasa vitakuwa katika makaratasi tu. Hakutakuwa na mikutano ya kamati kuu, hakuna mikutano na vyombo vya habari, wala operesheni za kuzunguka nchi nzima.  Demokrasia hutekelezwa na kukua mahali penye amani na utulivu," alisema.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item