WAJUKUU WADAI MZEE MANDELA SASA ANATABASAMU...
http://roztoday.blogspot.com/2013/07/wajukuu-wadai-mzee-mandela-sasa.html
Mzee Nelson Mandela. |
Wajukuu wawili wa kike wa Rais wa zamani Nelson Mandela, Zaziwe Dlamini-Manaway na Swati Dlamini, wamesema babu yao 'anatabasamu' na 'anawasiliana kwa kupepesa macho'.
Wawili hao wamekuwa wakiwasiliana na jamii kwa njia ya mtandao wa kijamii-Twitter-kwa saa tisa kwa siku wakijibu maswali juu ya hali ya babu yao na mgogoro kuhusu eneo atakapozikwa.
Zaziwe na Swati walisema jana, kwamba Mandela, ambaye ni Rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, 'anatabasamu' na familia yao imeendelea kuwa pamoja.
Ndugu hao walishiriki pia kwenye kipindi cha televisheni kiitwacho Being Mandela (Kuwa Mandela), kilichooneshwa kwa mara ya kwanza Marekani. Mandela (94) amelazwa katika hospitali ya Medi-Clinic, jijini hapa, kwa zaidi ya mwezi sasa hali yake ikiwa mbaya.
Mandela alifungwa miaka 27 jela kwa kupambana na utawala wa weupe wachache, kabla ya kuachiwa mwaka 1990 na kuchaguliwa kuwa Rais mwaka 1994. AlingÕatuka baada ya kuongoza kwa miaka mitano.
Wiki mbili zilizopita, mgogoro ulizuka katika familia ya kiongozi huyo juu ya eneo la maziko yake na ya watoto wake watatu, waliofariki dunia mwaka 1947, 1969 na 2005.
Mahakama iliamua makaburi ya watoto hao yahamishwe Mvezo alikozaliwa Mandela na kupelekwa Qunu ambako amekuwa akiishi baada ya kustaafu katika jimbo la Eastern Cape.
Hatua hiyo ya Mahakama ilitokana na kesi iliyofunguliwa na wanafamilia 16 ambao walimshitaki mjukuu wa kiume wa Mandela, Mandla, kwa kuhamisha makaburi matatu kinyume cha sheria na kuyapeleka Mvezo mwaka 2011, ili Mandela naye akifariki dunia azikwe hapo. Wosia wa Mandela unatamka kuwa akifariki dunia azikwe karibu na makaburi ya wanawe hao.
Wakijibu maswali, Zaziwe na Swati walisema hawakufurahia jinsi mambo hayo yalivyojitokeza. "Yalilazimika kutokea na mwishowe tumeendelea kuwa familia," walisema katika Twitter yao.
Walipoulizwa jinsi familia hiyo itakavyojenga tena umoja wake, walisema: "Tumeruhusu wazee wa familia watuongoze Umoja huo haujatoweka, ilikuwa ni mwanafamilia mmoja tu ambaye aliamua tofauti. Tutaendelea kumpenda ndugu yetu (Mandla)."
Wawili hao ni mabinti wa Zenani Mandela, binti wa Mandela kwa mkewe wa zamani, Winnie Madikizela-Mandela. Mandela aliachana na wake mara mbili na sasa amemwoa Graca Machel wa Msumbiji ambaye ni mjane wa Rais wa zamani wa Msumbiji, marehemu Samora Machel.