WANAWAKE WATATU WAUAWA KATIKA MAUAJI YA KUTISHA SHINYANGA...
http://roztoday.blogspot.com/2012/09/wanawake-watatu-wauawa-katika-mauaji-ya.html
Wanawake watatu wameuawa kikatili kwa kuchinjwa kwa mapanga, ikiwa ni pamoja na mmoja wao kutenganishwa kichwa na kiwiliwili.
Kamanda wa Polisi mkoani Simiyu, Salum Msangi alisema ofisini kwake mjini Bariadi jana kuwa, wanawake hao wameuawa kikatili katika matukio na maeneo tofauti na Polisi wanaliona kama endelezo la wimbi la mauaji ya kikatili dhidi ya wanawake vikongwe kutokana na imani potofu za kishirikina.
Alisema, tukio la kwanza lilitokea saa tisa za alfajiri ya kuamkia jana katika kijiji cha Bupandagila Kata ya Nyakabindi Tarafa ya Dutwa Wilaya ya Bariadi ambako mwanamke mkulima wa kijiji hicho, Luja Ngalu (75) akiwa amelala na mume wake nyumbani kwao, walivamiwa na kushambuliwa kwa kukatwakatwa kwa mapanga mpaka kusababisha kifo chake papo hapo.
Alisema, katika tukio hilo, Luja alichinjwa shingo na kutenganishwa kichwa na kiwiliwili chake na mgeni wake, Minza Godi (65) aliyefika nyumbani kwao kumsalimia Luja aliyekuwa mgonjwa wa homa, naye alishambuliwa kwa kukatwakatwa kwa mapanga sehemu mbali za mwili wake na kusababisha kifo chake.
Kamanda Msangi alisema, uchunguzi wa awali wa polisi umebaini kuwa chanzo cha mauaji hayo ni mtoto wa mke mwenzie mkubwa na Luja Magese Malongo (52) kufiwa na mtoto wake mwezi Machi mwaka jana na mtoto wake mwingine akafariki Agosti 28 mwaka huu na alipokwenda kwa mganga kuchunguza sababu za kifo cha mtoto wake, aliambiwa kuwa alirogwa na bibi yake ambaye ni Luja.
Kufuatia mauaji hayo polisi inawashikilia mtoto wa kambo wa marehemu Luja, Magese Malongo na mume wa marehemu mzee Malongo Malimi (90) kwa tuhuma za kushiriki katika mauaji hayo na hasa ikizingatiwa kuwa mzee Malimi siku ya tukio alikuwa amelala na mke wake Luja akachinjwa lakini yeye hakuguswa, hakupiga kelele wala kutoa taarifa kwa mtu yeyote.
Katika tukio jingine lililotokea majira ya saa tisa za alfajiri ya kuamkia jana huko katika kijiji cha Longalombogo kata ya Migato wilaya ya Bariadi, mwanamke mwingine Kundi Ndeli (35) aliuawa kikatili kwa kuchinjwa kwa mapanga na mtu au watu wasiojulikana.
Alisema, Kundi aliuawa akiwa amejipumzisha nje ya nyumba yake na mtoto wake Minza Ndulu mwenye umri wa mwaka mmoja. Minza kwa sasa amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Bariadi kwa uchunguzi na matibabu.
Alisema, uchunguzi wa awali wa polisi umebaini kuwa marehemu Kundi aliuawa na mume wake baada ya kupiga ramli na kugundua kuwa mtoto wao wa kwanza aliyekufa mwaka jana alitolewa kafara na mke wake kwa wachawi wenzake waliomtaka amtoe mtoto wao anayempenda zaidi ili atumike kwenye uchawi.
Kufuatia mauaji hayo, polisi wanamshikilia mume wa marehemu Ndulu Masalu (43) kwa tuhuma za kuhusika katika mauaji ya mke wake Kundi na mara baada ya uchunguzi wa polisi kukamilika atafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayomkabili.