MGOGORO WAWAWEKA 'KITANZINI' MAASKOFU KANISA LA MORAVIAN...

Askofu Kiongozi Alinikisa Cheyo
Huku hali ya sintofahamu ikizidi kuligubika Kanisa la Moravian Jimbo la Misheni Mashariki jijini Dar es Salaam, Maaskofu wa Kanisa hilo wamewekwa ‘kikaangoni‘ kwa kuagizwa kumaliza mgogoro huo haraka.
Agizo hilo limetolewa na Umoja wa Mabaraza ya Wazee wa Jimbo la Misheni Mashariki na linawahusu maaskofu Alinikisa Cheyo ambaye ni Askofu Kiongozi wa Kanisa la Moravian Tanzania, Lusekelo Mwakafwila wa Jimbo la Misheni Mashariki, Isaac Nicodem wa Jimbo la Tabora na Askofu Jonas Kasitu wa Jimbo la Rukwa.
Agizo hilo limewataka maaskofu hao kuchukua hatua haraka za kumrejesha madarakani Mwenyekiti aliyesimamishwa Clement Fumbo na Mweka Hazina aliyesimamishwa Nyambilila Lwaga.
Umoja huo wa Mabaraza ya Wazee umetishia kuwafukuza mara moja wachungaji 10, kama maaskofu hao watashindwa kuwarejesha watumishi hao.
Katibu wa Umoja huo wa Mabaraza ya Wazee, Nelson Ngajilo amethibitisha umoja huo kuonana na Maaskofu baada ya kuwaita Dar es Salaam hivi karibuni, lakini amekataa kuzungumzia maazimio ya kikao hicho akisema kuwa ni siri hadi pale hatua za utekelezaji zitakapoanza kuchukuliwa.
Ingawa umoja huo wa Mabaraza ya Wazee hautajwi katika vikao vinavyotambuliwa na Katiba ya Moravian na hivyo kukosa nguvu za kimamlaka, hoja zinaelezwa kuwa na mantiki.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya kanisa hilo zinasema katika kikao hicho ambacho Maaskofu kama walezi na washauri walikuwa wasikilizaji tu, wajumbe wa mabaraza hayo waliwataka Maaskofu kumrejesha haraka Mwenyekiti Fumbo.
"Kimsingi tumewaambia Maaskofu kama watashindwa kuchukua hatua hiyo tutawafukuza wachungaji 10 ambao tunajua ndio chanzo cha kusimamishwa kazi kwa Mwenyekiti Fumbo na Mchungaji Lwaga, kwa chuki binafsi. Tumewaambia maaskofu walifanye hili haraka sana, wakichelewa tutachukua hatua na tayari tumeanza kuzuia mapato kutoka kwa baadhi ya sharika kwenda jimboni ili kuwakomoa," kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, agizo hilo ni kama linawatia kitanzini maaskofu hao kutokana na ukweli kwamba chombo kilichotumika kuwasimamisha Mwenyekiti Fumbo na Mweka Hazina Lwaga ndio chombo cha juu kwa uamuzi kwa mujibu wa Katiba ya kanisa hilo na suala linaposhindikana katika ngazi hiyo ngazi ya rufani ni Mkutano Mkuu wa Sinodi ambao kwa namna mgogoro huo ulivyo hivi sasa ni lazima uitishwe.
Mmoja wa wachungaji wanaotajwa kuwa katika orodha ya kutaka kufukuzwa kwa kuhusika kumsimamisha Mwenyekiti Fumbo, Mchungaji Yustazia Mbao, alikiri kupata taarifa ya Maaskofu hao kuagizwa kumrejesha Mwenyekiti huyo madarakani, lakini akasema ni kinyume cha Katiba na kwamba hatua hiyo inaweza kusababisha mgogoro zaidi. Wachungaji wengine walio katika mkumbo huo wa kufukuzwa hawakutajwa.
Kuhusu maaskofu kuagizwa kumrejesha madarakani Mwenyekiti Fumbo, Mchungaji huyo alisema ni kinyume cha Katiba kwa vile Maaskofu wapo ndani ya halmashauri na si juu ya halmashauri.
Jumapili iliyopita, ilifichuka siri ya chanzo cha mgogoro huo kwamba umechangiwa na matumizi mabaya ya karibu Sh milioni 529 za Jimbo, upotevu wa vyerehani 10, jenereta, kamera katika Usharika wa Ukonga, na pia upuzwaaji mkubwa wa vikao vya kanisa.
Upotevu wa fedha na mali hizo uliripotiwa na Tume maalumu iliyoundwa Kikatiba ili kuchunguza mwenendo wa fedha na mali za kanisa hilo baada ya kuwepo madai kuwa kuna ubadhirifu.
Hata hivyo, Mwenyekiti Fumbo anadaiwa kukataa kuitambua Tume hiyo.
Anadaiwa pia kupuuza kumuondoa madarakani Mweka Hazina aliyesimamishwa Lwaga ambaye alidaiwa na Sinodi kutokuwa na sifa. Anadaiwa kupuuza pia kumuajiri Mkaguzi wa Ndani, kushinikiza kubarikiwa kwa Mchungaji Lwaga pia kuwa na sifa na pia kutaka kubadili eneo la Makao Makuu ya Kanisa hilo kutoka Chamazi – Chanika kwenda Tabata tofauti na uamuzi wa vikao.
Hata hivyo, alipozungumza na gazeti hili hivi karibuni, Mchungaji Fumbo pamoja na kukiri kuwepo kwa mgogoro huo, lakini alisema unatokana na kuwepo kwa watu wachache wenye nia ya kutaka kuliharibu kanisa hilo kwa kutaka kuwaweka madarakani watu wanaowataka wao na kusema kwamba atasimama kidete katika kusimamia ukweli na haki ya waumini.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item