ATAKA WATOAJI TALAKA NAO WAHAME NYUMBA...

Mkazi wa Kimara Baruti Dar es Salaam, Mwajuma Selemani (37) amependekeza Katiba mpya ilazimishe wanaume wanaotoa talaka kwa wake zao nao wahame nyumba waliyokuwa wakiishi na familia.
Mwajuma alisema hayo jana mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuongeza kuwa wanawake wamekuwa wakinyanyasika baada ya kupewa talaka na waume zao.
“Ninaomba sana Katiba mpya itambue suala la talaka anayotoa mwanamume, kwamba badala ya mke kuondoka eneo hilo, mume naye awe tayari kufungasha na kuondoka,” alisema Mwajuma.
Alisema kwa kufanya hivyo, heshima ya mwanamke itaongezeka na vitendo vya unyanyasaji anavyofanyiwa kupungua, hasa ikizingatiwa kuwa wapo walioishi miaka zaidi ya 48 na kuzaa na kuishia kutalikiana.
Mwajuma alisema jambo lingine ambalo Katiba inapaswa kulitambua ni pamoja na mwanamke mjane kuruhusiwa kuishi katika nyumba aliyoachiwa na mumewe na kuwa huru kupata mwenza mwingine kama ambavyo mume anavyoweza kufanya.
“Jamani mama akifariki dunia baba huleta mke mwingine katika nyumba ileile na kitanda kilekile alichokuwa akilala na mkewe, ila baba akifariki dunia  mama akitaka kuanza uhusiano mpya, huondoka eneo hilo, sasa Katiba itambue hilo  na kumpa mama uhuru pia,” alisema Mwajuma.
Asha Juma (56) alipendekeza Katiba mpya imlinde mwanamke ili asisumbuliwe wakati mumewe anapofariki dunia na mali  waliyozalisha pamoja ibaki kuwa ya familia husika.
Alipendekeza elimu ya Katiba ianze kutolewa tangu shuleni na wanaosoma wapewe mitihani ya Katiba ili kuwekea mkazo somo hilo walielewe kwa undani.
John Ndomba alipendekeza Katiba mpya itamke waziwazi kuhusu salamu ya Mtanzania ili kuondoa mkanganyiko katika mikutano na halaiki ya watu.
“Kuwe na salamu maalumu na hizi salamu za Tumsifu Yesu Kristu na Asalaam Aleykum ziondoke, kwani zinatugawa,” alisema Ndomba na kuongeza kuwa pia liwepo vazi la Mtanzania litakalowatambulisha vyema.
Deogratius Mtosho (23) alipendekeza uteuzi wa wakuu wa mikoa ufanyike katika mikoa husika kwani ndio wanaofahamu maeneo na kero zinazosumbua wananchi kuliko kuteua asiyekuwa mkazi wa eneo hilo.
Pia alipendekeza mawaziri wasiwe wabunge na Muungano uvunjwe na wananchi waulizwe kama wanauhitaji na maoni yao yasikilizwe.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item