MAHOJIANO YANGU NA SHARO MILIONEA...

Ni saa nne kasorobo usiku wa Jumatatu, napokea simu kutoka kwa ndugu wa karibu akitaka kujua kama kweli Hussein Ramadhan Mkieti ‘Sharo Milionea’ amefariki dunia! Anasimulia Anastazia Anyimike, mwandishi wa gazeti la HABARILEO.
Sikuwa na uhakika na taarifa hizo, na pia nilijipa moyo kuwa huenda ni uzushi kama ambavyo siku hizi uzushi huo unavyokithiri kupitia mitandao ya kijamii.
Nilizidi kujipa moyo hasa baada ya kuendelea kuangalia tangazo la biashara akiwa na msanii mchekeshaji Mzee Amri Athumani ‘King Majuto’ la ‘Nimehamia Airtel’.
Lakini moyo wangu unaingiwa na ubaridi baada ya kuthibitishiwa kuwa taarifa hizo ni za kweli, ndipo akili yangu inapokumbuka mengi, kazi zake nyingi, mtandao wa Facebook ambao mara nyingi ‘status’ zake aliweka habari za wasanii, lakini kubwa ni siku nilipokutana naye kwa ajili ya mahojiano.
Kwangu mimi, Sharo Milionea alikuwa msanii anayejua anachokifanya na kuheshimu taaluma yake, ni miongoni mwa wasanii ninaowakubali kama Irene Sanga na Ambwene Yesaya ‘AY’ ambao ukiwapigia simu na kutaka kuzungumza nao si watu wa kujidai na kupandisha mabega kutokana na umaarufu wao.
Nakumbuka ushirikiano mkubwa alionipa wakati wa mahojiano na kueleza maisha aliyopitia na malengo yake ya baadaye. 
Sharo Milionea ni mtoto wa mwisho wa familia ya watoto watatu wa Ramadhani na Zainabu Mkieti, aliyezaliwa mwaka Oktoba 27, 1985 katika kijiji cha Lusanga, Muheza, Tanga.
Alipata elimu ya msingi katika shule ya Lusanga na baadaye kujiunga na sekondari ya Kwabutu alikosoma hadi kidato ya tatu, akaacha shule kutokana na matatizo ya kifamilia.
Mwaka 2003 baada ya kuona maisha hayaendi, aliamua kuhamia Dar es Salaam kuungana na mama yake ambaye alikuwa mjasiriamali mdogo.
“Baada ya kufika Dar nikapelekwa kujifunza masuala ya ufundi magari kwenye gereji moja ambako nilikaa wiki mbili na baadaye nikapelekwa kwenye ufundi wa friji ambako nilijifunza kwa wiki tatu, nako huko maisha yalizidi kuwa magumu kwangu, nikaamua kuhamia kwenye biashara ndogo na nilifikia hata kuuza magazeti Kiwalani,” anasema.
Alisema baadaye mama yake aliamua kurejea Muheza kwenda kumuuguza bibi yake na kujikuta akiishi peke yake katika jiji hili la Dar es Salaam, “baada ya mama kuondoka, nilibaki mwenyewe, gharama za maisha nilizibeba mwenyewe, kusema ukweli maisha yalikuwa magumu sana kwa upande wangu.”
Sharo Milionea anaongeza: “Mwonekano wangu uliwafanya watu wengi wanisukume kuingia kwenye fani hii akiwamo rafiki yangu Chiba, msanii Siasa Mohamed, kutokana na matendo yangu, lakini wakati huo nilikuwa naimba mwenyewe mitaani.”
Mwaka 2005 akiwa na marafiki zake, Snura Mushi, Nas na Dats waliamua kuunda kundi lao la muziki na kuandaa nyimbo kadhaa, lakini kundi hilo halikudumu baada ya Snura kujiengua na kwenda kuigiza filamu ya Jumba la Dhahabu.
Sharo Milionea alijiunga na kundi la maigizo la Jamal Arts lililokuwa chini ya Gumbo Kihorota na hapo aliigiza filamu ya Zinduna na Itunyama ambayo aliigiza na wasanii kama Emmanuel Mgaya ‘Masanja', Alex Chalamila ‘Mack Regan’.
“Mbali na uigizaji, Mungu amenisaidia nina utundu wa utunzi pia, na nilitunga filamu moja niliita dakika moja ambayo hadithi yake ilimvutia Snura akaamua kuitengeneza na kuigeuza jina kwa kuiita ‘Sekunde Chache.”
Anasema kwa mara ya kwanza alichukuliwa na Musa Kilali na aliigiza kwenye filamu ya vichekesho ya Mbwembe Vol. 2 ambaye aliigiza kama ’Brazamen’ aliyeko kijijini ambapo alipewa sehemu tatu, filamu hiyo aliigiza na wasanii kadhaa wakiwamo Kiwewe (Robert Augustino), Masele (Christian Masele).
“Kusema ukweli, pamoja na mimi kuwa mchanga katika fani, lakini niliweza kufanya vizuri, pamoja na ugeni wangu na kuigiza na wakongwe lakini nilifanya vizuri.”
Sharo Milionea anasema: “Kutokana na kufanya vizuri, Kiwewe aliniomba niingizwe kwenye filamu yao ya vichekesho iliyoitwa ‘Vichwa Vitatu’, Matumaini (Tumaini Martin) alikuwa na mashaka nami, hakutaka nishiriki, nilipopewa nafasi niliweza kumhakikishia dada huyo kwa kufanya vizuri katika filamu hiyo.”
Alisema alifanikiwa kuigiza filamu za futuhi zake mwenyewe ambazo aliziita Sharo Baro na Sharo Milionea. Alisema mwaka jana aliingia mkataba wa mwaka mmoja na Khalfan Abdallah anayemiliki Kundi la Bongo Super Stars Comedy ambalo linashirikisha waigizaji kadhaa akiwamo King Majuto na Masele, pia aliigiza futuhi ya Back From New York na Mtoto wa Mama ambayo ndiyo ilifanya usemi wa ‘Kamata mwizi meen’ kuvuma na kuwa vinywani mwa watu wengi.
Akizungumzia safari ya maisha ya usanii, Sharo Milionea anasema: “Nimepitia maisha ya aina mbalimbali, mabonde na milima, lakini sasa nimeanza kunyanyuka, kwa sababu mimi sanaa yangu ni tofauti kama ilivyo ya Will Smith wa Marekani, ambaye anaweza kuigiza futuhi, filamu  na kuimba pia.
Sharo Milionea anaongeza: “Ninachoshukuru, nimeleta mapinduzi makubwa kwenye tasnia ya filamu hususani katika fani ya ucheshi, watu wengi waliamini kwamba ili uchekeshe, lazima mtu avae nguo zilizochanika au awe mchafu au apake masizi usoni, lakini mimi nimeonesha kuwa unaweza kuchekesha hata ukiwa unapendeza.”
Sharo Milionea ambaye alionekana kuzoeleka kwenye komedi, lakini sasa ameweza kuubeba uhusika wake vizuri katika filamu inayotamba sasa ya Chumo iliyoongozwa na Jordan Riber yenye maudhui ya kupambana na malaria.
Katika filamu hiyo, Sharo Milionea ameigiza kwa jina la Juma akiwa kijana masikini anayetokea kumpenda Amina (Jokate Mwegelo), ingawa baba yake Amina, Ali anataka binti yake awe na maisha mazuri, hivyo kutaka aolewe na Yustus (Yusuph Mlela) ambaye anatoka familia ya kitajiri.
Pia Sharo Milionea ameigiza kwenye wimbo wa ‘Sababu ya Ulofa” wa msanii Top C.
Akizungumza chanzo cha jina la Sharo Baro, anasema: “Jina hilo nilipewa na mashabiki wangu kutokana na staili yangu ya kibrazamen. Tangu nikiwa mdogo Tanga suala la usafi lilikuwa jadi yangu, hata kama nina nguo mbili basi nitazifua, ilimradi nionekane nadhifu.
“Nilipoitwa jina hilo kuna studio ilikuwa inaitwa Sharobaro, kwangu mimi niliona ni kawaida tu, kama kuna  MJ Records, kuna ubaya gani kama nitaitwa MJ au kuna Bongo Rank, je nikijiita Bongo litakuwa jina la mtu? Lakini baada ya Bob Junior ambaye anamiliki Sharobaro Records kusema jina lake, nikaona isiwe shida, basi mimi nikajiita Sharo Milionea.
Anapozungumzia changamoto za kazi ya sanaa, anasema fani hiyo imekuwa na majungu na kuoneana wivu huku baadhi yao wakikosa ubunifu.
“Fani hii kwa Bongo bado, ni majungu ndiyo yanayotawala, mfano mzuri ni pale baadhi ya watu walitaka kufanya kazi na mimi wakati nina mkataba, wanataka nifikishwe kwenye vyombo vya sheria kwa sababu ya Sh 50,000 anayotaka kunilipa, haiwezekani, lakini unasikia maneno ‘anaringa sana, yule tumemlea wenyewe’”.
Anasema, lakini pia baadhi ya wasanii wanakosa ubunifu na ndio maana watu wamekuwa wakiigana kwenye mitindo ya uigizaji.
“Mimi huwezi ukaniambia niigize kama Kingwendu, ile ni staili yake, hebu waangalie wasanii wanavyoiga staili yangu ya kibrazamen, na ndiyo maana sasa nimekuja na swaga ya ‘Ooh mama’ na hiyo ikianza kuchuja au watu wakiiga basi nitabadilisha nyingine.”
Alipozungumzia wasanii ambao anakubali kazi zao, Sharo Milionea anawataja, Joti na King Majuto, “Hawa ni wasanii ninaowakubali sana kwenye fani ya ucheshi. Joti ana mitindo mingi na ni mbunifu sana, pia King Majuto ni msanii ambaye si wa kumfananisha na mtu yeyote.
“Kwa kazi nilizofanya na King Majuto, nimejifunza mambo mengi, ni msanii ambaye anabadilika pamoja na utu uzima wake, kuna futuhi tumeigiza naye inaitwa ’Alosto’, ameigiza kama teja, yaani ameweza kuigiza uteja vilivyo.”
Alisema, kama angepata nafasi ya kuigiza na wasanii wa vichekesho wa nje, basi angechagua wasanii wenye vituko kama Mr Bean, Eddy Murphy na Will Smith. “Hawa ni wasanii ambao mara nyingine napenda kuangalia kazi zao na kama ningepata nafasi ya kuigiza nao basi ningefurahi na kiu yangu ingekatika.”
Akizungumzia mafanikio, Sharo Milionea alisema sanaa hiyo ilibadilisha maisha yake ya awali ya kuwa tegemezi na kuwa mtu wa kujitegemea kimaisha ingawa kiu yake kubwa ilikuwa kuwa mwigizaji wa kimataifa na kujipatia fedha za mtaji wa biashara.
Sharo Milionea alisema: “Hakuna siku niliyokuwa na furaha nilipopokea simu kutoka kwa mtu aliyeko  Marekani akisema mtaa wao watoto wanamwiga kutembea na anavyoongea, na mwingine akapiga kutoka Italia. Nimefarijika sana kuona hatimaye kazi yangu inatambuliwa na watu walioko nje.
Akizungumzia umaarufu wake katika sanaa, Sharo Milionea alisema: “Kusema kweli nikipita mtaani watu wananiangalia na kama nitakutana na watoto basi najua hapo lazima nifuatwe nyuma, lakini napendwa na watu wengi hususani akina dada ambao wengi wananisumbua sana, lakini mimi nawapotezea.”
“Ule ni uigizaji tu, mimi nina mbio sana, hebu jaribu kuniibia uone, lakini  kimtindo ndo ile ‘Kamata mwizi meen!’ ‘Kamata mwizi babu....’ ni swaga tu zile.”
Akitoa mwito kwa wasanii wa vichekesho, aliwataka kuwa wabunifu zaidi, naamini ubunifu ndio utakaofanya sanaa yetu ikue kama Mr Bean na wasanii wengine.
Mpaka mauti inamkuta, alijikita katika muziki wa Bongofleva na kushirikiana na wasanii, kadhaa. Ndoto na malengo ya Sharo Milionea yamekatishwa kwenye ajali ya gari. Ni hakika kuwa ni kipaji kilichoyeyuka mithili ya mshumaa uliowaka na kuzimwa na upepo wa kifo. Mungu ailaze pema roho ya Hussein Ramadhan Mkieti ‘Sharo Milionea’. Amen.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item