'TRENI LA MWAKYEMBE' YAINGIZA HASARA SHILINGI MILIONI 1.2 KWA SIKU...
http://roztoday.blogspot.com/2013/07/la-mwakyembe-yaingiza-hasara-shilingi.html
Treni hilo likiwa katikasafari zake za kila siku jijini Dar es Salaam. |
Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) imesema inapata hasara ya wastani wa Sh milioni 1.2 kwa siku, kutokana na gharama kubwa za uendeshaji wa usafiri wa treni katika Jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza na mwandishi wiki iliyopita, Mkurugenzi Mtendaji wa TRL, Kipalo Kisamfu alisema gharama hizo zinachangiwa na sababu mbalimbali, ikiwemo utumiaji wa vitendea kazi, ambavyo siyo maalumu kwa huduma za usafiri wa treni za mijini.
Alisema matumizi ya vichwa na mabehewa ambayo siyo maalumu kwa usafiri wa mijini, yamesababisha gharama kubwa za uendeshaji, kutokana na matumizi makubwa ya mafuta ya dizeli.
Kutokana hali hiyo, alisema Serikali inaangalia namna ya kupata treni maalumu, ambazo hutumika kwa usafiri wa mijini.
Hata hivyo, alisema kuwa pamoja na hasara hiyo, TRL imekuwa ikisaidia kuchangia ukuaji wa uchumi kwa kiasi kikubwa.
"Pamoja na kwamba sisi tunapata hasara hiyo kwa siku, lakini uchumi kwa ujumla unafaidika kwa sababu watu wanawahi kazini na tumepunguza foleni katika Jiji hivyo hii hasara ya TRL tunapaswa kuiangalia kwa mapana zaidi, maana uchumi unakua na tunafaidika," alisema.
Kisamfu alisema usafiri wa treni katika Jiji, umepata mwitikio mkubwa kutoka kwa wakazi wa jiji hilo, ambapo wastani wa abiria 5,000 hutumia usafiri huo kwa siku.
Alisema mwanzo walipendekeza nauli ya Sh 800 ili angalau kukidhi gharama hizo, lakini Mamlaka ya Usafiri wa Nchikavu na Majini (Sumatra) ilikutana na wadau na kupendekeza nauli iwe Sh 400 kwa watu wazima.
Ili kuufanya usafiri huo kuwa bora zaidi, alisema kunahitajika miundombinu ya kuwezesha vituo vyote saba vya njiani, kuwa na uzio na majukwaa ya abiria.
"Miundombinu hii itasaidia kuwawezesha abiria kuingia kwenye vituo hivyo kwa utaratibu mzuri zaidi, kuliko ilivyo sasa hivi na pia majukwaa yatawasaidia kupanda na kushuka kwa urahisi zaidi na kutoa huduma kwa abiria wa marika yote," alisema.