MTOTO ALIYETANGAZWA KUFA WAKATI WA KUZALIWA 'AFUFUKA' KWENYE MADHABAHU...
http://roztoday.blogspot.com/2013/07/mtoto-aliyetangazwa-kufa-wakati-wa.html
KUSHOTO: Dokta Aurelio Filipak. KULIA: Madhabahu ambako Yasmin 'alifufuka'. |
Mtoto mdogo wa kike ambaye alitangazwa kufariki mara baada ya kuzaliwa 'amefufuka' masaa matatu baadaye kwenye madhabahu ya kanisa dogo hospitalini hapo, imeripotiwa jana.
Mwili wa Yasmin Gomes uliwekwa kwenye sanduku na kuachwa kanisani hapo katika hospitali hiyo iliyoko mjini Londrina, kusini mwa Brazil, na muuguzi mmoja ambaye 'hakuweza kumchukua na kumpeleka kwenye chumba cha maiti', kwa mujibu wa ripoti.
Lakini pale mama wa kichanga huyo aliyejawa huzuni alipowasili akiwa na msimamizi wa mazishi kuchukua mwili huo kwa ajili ya maziko walipatwa na bumbuwazi pale mtoto huyo aliporusha mguu wake mmoja, na kufumbua macho yake.
Bibi wa mtoto huyo, Elza Silva alieleza: "Kwanza sikuamini, hatukukubali hilo lingeweza kutokea.
"Kisha tunashuhudia kwamba alikuwa akipumua. Tulikumbatiana kila mmoja na kuanza kupiga kelele, "yuko hai, yuko hai'. Ulikuwa ni muujiza."
Kumbukumbu za hospitali zinaonesha Yasmin alizaliwa akiwa hai kwa njia ya kawaida Jumanne asubuhi kwenye Hospitali ya Lincoln Graca, lakini akaacha kupumua mara baada ya kuzaliwa.
Madaktari walijaribu bila mafanikio kuokoa maisha ya mtoto huyo mara kadhaa lakini mwishowe ikatangazwa kuwa amekufa majira ya Saa 5 asubuhi, na cheti cha kifo kutolewa.
Mama wa Yasmin, Jenifer da Silva Gomes, mwenye miaka 22, alieleza kwamba alikuwa wa kwanza kuambiwa kuwa binti yake amefariki.
Anakumbukia: "Nilihisi dunia imenielemea ghafla. Lilikuwa tukio la kuchanganya kuliko yote pale ndoto zangu zote zilipotoweka."
Muuguzi Ana Claudia Oliveira, ambaye alikuwapo wakati wa kuzaliwa mtoto huyo, alisema aliagiza mwili wa mtoto huyo ulazwe kwenye kanisa dogo hospitalini hapo, badala ya taratibu za kawaida za kupelekwa kwenye majokofu ya chumba cha maiti.
Alisema: "Ni malaika mdogo, mtoto. Sikuweza kupata wazo la yeye kupelekwa kwenye chumba cha maiti."
Aliongeza kwamba aliuosha na kuuvika mwili wa mtoto huyo aliyekufa na hakukuwa na shaka yoyote kwamba alikuwa amekufa.
Alisema: "Ninaweza kukuhakikishia, mtoto huyo alikuwa amefariki. Mboni zake hazikuweza kuhisi mwanga. Ishara zake zote zilionesha kabisa kutokuwapo kwa uhai.
"Nilishuhudia kwa macho yangu mwenyewe. Alikuwa wa bluu mwili mzima, alikuwa amekufa kabisa," alisema.
Baba wa Yasmin Cleverson Carlos Gomes, mwenye miaka 26, alisema alipokea taarifa hizo wakati akisubiria kwenye kibaraza cha hospitalini hapo na kwenda moja kwa moja kwenye kanisa hilo dogo.
Alisema: "Niliona binti yangu aliyesawajika, mwili usiokuwa na uhai. Sikuweza kukaa pale. Nilikimbia nje ya kanisa huku nikibubujika machozi."
Mwili wa Yasmin ulibakia kwenye sanduku ndani ya kanisa hilo hadi Saa 8 mchana, pale bibi yake alipowasili na mmiliki wa duka la mazishi, rafiki wa familia Rosilis Ferro, kubeba jeneza la mtoto huyo.
Lakini mapema wakati wakielekea kumchukua, mtoto huyo akarusha mguu wake mmoja, kwa mujibu wa Ferro.
Alisema: "Lilikuwa ni tukio la hisia za kipekee. Nilianza kutetemeka na sikuweza kuongea, nilijawa na furaha isiyoelezeka.
"Nilimwita muuguzi ambaye mwanzoni hakuniamini, alitueleza kwamba ulikuwa mshtuko. Lakini kisha mtoto akafumbua macho yake."
Mama Jennifer alisema alikuwa bado akifarijiwa na wanafamilia ndipo muuguzi alipoingia kwa kasi kwenye chumba hicho na kupiga kelele: "Binti yako yuko hai".
Anakumbuka: "Kwanza sikufanya chochote, sikujua nini cha kufikiria. Kisha nikaanza kujihisi kuumwa. Lakini baada ya hapo sikuweza kudhibiti furaha yangu."
Mtoto huyo alikimbizwa kwenye kitengo cha uangalizi maalumu katika hospitali ya watoto ya Sagrada Familia iliyoko jirani na hapo, ambako hali yake ilielezwa kuwa imeimarika.
Dokta Aurelio Filipak, ambaye alipambana kumwokoa Yasmin na kusaini cheti chake cha kifo, alisema: "Watu wanaweza kufanya maamuzi yao binafsi, lakini wale wote ambao walikuwapo pale wanafahamu vizuri nini kilichotokea.
"Katika miaka 20 ya matibabu, sijawahi kushuhudia chochote kama hiki."
Alisema timu ya madaktari ilijaribu kuokoa maisha ya mtoto huyo kwa karibu saa moja. "Vifaa vyote, kama kidhibiti mapigo ya moyo na mashine ya oksijeni, vyote vilionesha kwamba alikuwa hapumui na hakuwa na mapigo ya moyo," aliongeza.
Jana familia ya Yasmin ilisema wanapanga kubadili jina lake na kuwa Victoria - 'ushindi' kwa Kireno - na walisema wanaamini 'kufufuka' kwake ilikuwa ni muujiza.
Jennifer alisema: "Hakuna miujiza inayoelezeka. Inatokea kama Mungu anavyopenda. Kama ilikuwa ni mapenzi yake kwamba binti yetu alikufa, tungekubaliana na hilo, lakini alimrejesha, hivyo lazima ana mipango mikubwa naye."