UTAFITI WABAINI MAJANI NA UNGA WA UBUYU NI SALAMA KWA MATUMIZI...
http://roztoday.blogspot.com/2013/07/utafiti-wabaini-majani-na-unga-wa-ubuyu.html
Ubuyu. |
Utafiti wa kisayansi, haujabainisha athari za kiafya zinazoweza kujitokeza kwa ulaji wa unga na majani ya mbuyu, isipokuwa kwa mafuta yatokanayo na mbegu za mti huo.
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imesisitiza, kwamba mafuta hayo ni hatari ikisema yana kiwango cha tindikali ya mafuta ya Cyclopropenoic.
TFDA katika taarifa yake ya ufafanuzi iliyotolewa jana, ilisema kiwango cha tindikali hiyo huweza kuondolewa katika mafuta hayo kwa kuyachemsha kwa kiwango cha nyuzi joto 180 kwa saa nane, au kutumia teknolojia ya kuyagandisha.
“Kwa sasa nchini, hakuna aina ya usindikaji unaofanyika wenye uwezo wa kuondoa tindikali ya Cyclopropenoic katika mafuta ya ubuyu,” ilieleza taarifa hiyo.
Iliendelea kusema, hadi sasa hakuna kiwango chochote cha ubora na usalama cha kitaifa au kimataifa cha mafuta yatokanayo na mbegu za ubuyu.
“Ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya mafuta hayo, jamii inashauriwa kuepuka ulaji wake,” ilisisitizwa taarifa hiyo.
Mamlaka hiyo pia, ilitoa mwito kwa wananchi na jamii kushirikiana kulinda afya za walaji kwa kutoa taarifa wanapouziwa au kuhisi kuwepo kwa chakula, dawa, vipodozi na vifaatiba duni na bandia, ambavyo havikidhi viwango vya usalama na ubora.
Hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya bidhaa zinazotokana na ubuyu, ikiwa ni pamoja na mafuta, unga na majani ya mbuyu.
Tamko la TFDA lililotoka hivi karibuni katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, kuhusu hatari ya matumizi ya mafuta hayo ya ubuyu, limezua mjadala huku baadhi wakipinga na wengine wakihoji sababu za Mamlaka hiyo kukaa kimya na kuachia biashara hiyo ikiendeshwa kwa muda mrefu.
Mmoja wa wataalamu wa masuala ya lishe na chakula wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema nchini, hakuna utafiti uliofanyika juu ya madhara ya mafuta hayo, ingawa alikiri kuwapo uwezekano wa madhara.
Mtaalamu huyo aliyezungumza na gazeti hili, alikiri kwamba mafuta hayo yanafaa kwa kujipaka na si kwa kunywa kama inavyofanyika sasa.
“Nchini, hakuna utafiti uliofanyika na kuwekwa wazi juu ya madhara ya mafuta ya ubuyu, lakini upo ukweli, jamii inabidi ichukue hadhari, haya mafuta hayafai kwa kunywa bali yatumike kama kipodozi,” alisema.
Hata hivyo, alisema jambo ambalo linaweza kufanya wengi wasizingatie hadhari iliyotolewa juu ya mafuta hayo, ni muda na mfumo uliotumiwa na Mamlaka kuhabarisha umma.
“Mafuta haya yametumika kwa muda mrefu sana bila Mamlaka kutoa angalizo…hata kama Mamlaka ilikuja kubaini hatari zake, ilipaswa itoe taarifa rasmi na yenye mapana na si kutegesha kwenye maonesho ya Sabasaba, na kuzungumza na baadhi ya magazeti wakati suala lenyewe ni nyeti sana,” alisema.