DUNIA KUFANYA KAZI ZA KUJITOLEA MAADHIMISHO YA SIKU YA MANDELA...

Mzee Nelson Mandela.
Taasisi ya Nelson Mandela, imetaka watu duniani, wafanye shughuli za kujitolea kwa dakika 67, wakati kiongozi huyo akifikisha umri wa miaka 95 wiki ijayo.

Mandela atafikisha miaka 95 Alhamisi, ambayo pia itakuwa kumbukumbu ya nne tangu kuanzishwa kwa Siku ya Kimataifa ya Mandela.
“Lengo letu ni rahisi, tunataka kila mtu ajue ana uwezo na wajibu wa kuleta mabadiliko,” taarifa ya taasisi hiyo ilieleza katika tovuti rasmi ya taasisi hiyo. Taarifa hiyo pia imetolewa kupitia mtandao wa mawasiliano wa Twitter.
Taasisi hiyo imeeleza kuwa Mandela alitoa miaka 67 ya maisha yake, kupigania haki za binadamu, ndiyo maana imeanzisha kampeni maalumu, kuomba watu binafsi, vikundi vya kijamii na kampuni na taasisi za umma na binafsi, kujitolea siku hiyo.
“Hata ikiwa ni kitendo kidogo tu, lengo letu ni kubadili ulimwengu kwa mazuri kama Mandela alivyofanya,” imeelezwa katika mtandao huo.
Taasisi hiyo imekuwa ikitumia mtandao huo kutoa kauli alizowahi kutoa kiongozi huyo ambaye alifungwa miaka 27, kwa kupiga vita ubaguzi wa rangi.
“Jambo muhimu katika maisha, si ukweli kwamba tunaishi. Ni mabadiliko tutakayoleta katika maisha ya watu wengine, yatakayoleta umuhimu wa maisha tunayoishi.” Nukuu ya Mandela inayotumika katika kampeni hiyo.
Akizungumzia hali ya afya ya Mandela baada ya kumtembelea hospitalini juzi jioni, mara ya pili mfululizo, Rais Jacob Zuma alisema hali ya Mandela inatia matumaini.
"Tumepata matumaini, afya ya Madiba imeanza kuimarika kulingana na matibabu anayopewa, naomba umma uendelee kumwunga mkono kwa kumwonesha upendo, unaompa yeye na familia nguvu,” ilieleza taarifa ya Zuma.
Awali kabla ya Zuma kumtembelea, Mfalme wa Kabila la AbaThembu, analotoka Mandela, Buyelekhaya Dalindyebo, alimtembelea hospitalini juzi mchana na kusema afya yake inaendelea vizuri na anatambua wageni.
"Hakuweza kuzungumza, lakini alinitambua na kutoa ishara chache kuonesha alikuwa akinisikiliza kwa kutumia macho,” alisema Dalindyebo, ambaye ni mpwa wa Mandela.
Wakati afya ya shujaa huyo wa vita dhidi ya ubaguzi wa rangi, ikielezwa kutia moyo, wakazi wa kijiji cha Qunu, wanajiandaa kukodisha nyumba zao na farasi, kwa wageni wakati Mandela atakapokuwa akizikwa.
Taarifa kutoka kijiji hicho, zilisema wakati hali ya Mandela ikitia matumaini, kumekuwa na maandalizi ya mazishi Qunu.
Mmoja wa wakazi wa Qunu, Adelaide Madyibi na wanawe wa kike, Kholosa na Tulile, wanajiandaa kukodisha nyumba yao ya vyumba vitano vya kulala na wao kuhama kwa muda wakati ukifika.
Madyibi alilieleza jarida moja la Qunu kwamba, hana uhakika na bei atakayotoza kwa chumba, lakini atakodisha gari lake la kukokotwa na farasi kwa randi 700 kwa siku.
Mwanamama huyo mjasiriamali, anaamini usafiri wa farasi wakati huo, utakuwa rahisi kwa wageni kutembelea kijiji cha Qunu.
"Ndugu yangu mmoja, Nobuntu, tayari amekodisha farasi wawili kwa wageni ambao wamesisitiza kutumia usafiri huo kwenda nyumbani kwa kiongozi huyo wakati ukifika,” alisema.
Taarifa za maandalizi ya maziko ya Madiba, zimepokewa kwa hisia tofauti huku wananchi wakituhumiwa kwa kukosa utu.
“Hawa watu hawana utu, Mandela hajafa na watu wameanza kutengeneza fedha kutokana na kifo chake, hawana aibu licha ya mambo makubwa aliyofanya kwa watu wa Afrika Kusini,” alisema Christina Setloboko.
Carol Seymour alisema jambo hilo linasikitisha na kuhoji iweje watu wafanye biashara kwa kifo cha mtu na kuongeza kuwa dunia ya sasa imepoteza utu.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item