BASIL MRAMBA YUKO HOI, MAHAKAMA YAMPA KIBALI AKATIBIWE NJE YA NCHI...
http://roztoday.blogspot.com/2013/07/basil-mramba-yuko-hoi-mahakama-yampa.html
Basil Mramba. |
Aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba anayekabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya ofisi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 11.7, anaumwa na amepewa kibali na Mahakama kwenda nje ya nchi kutibiwa.
Wakili wake, Elisa Msuya amedai jana mahakamani kwamba ugonjwa unaomsumbua umeathiri uwezo wake wa kuongea na hakuna mtu anayeweza kujibu maswali badala yake.
Hayo yalifahamika jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya Wakili wa Utetezi, Msuya kuomba kibali cha mshitakiwa huyo kusafiri kwenda Australia au India kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya ugonjwa ambao hakuutaja.
Kesi hiyo jana ilikuja kwa ajili ya mawakili wa Serikali kumhoji Mramba, lakini kabla Hakimu Sam Rumanyika hajaiahirisha kwa kuwa jopo la mahakimu wanaosikiliza kesi halikukamilika, Wakili Msuya alitoa ombi hilo.
Wakili Msuya alidai hali ya afya ya Mramba siyo nzuri na Juni 9 mwaka huu alizidiwa na kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Aga Khan ambapo madaktari walimshauri aende kati ya Australia au India kupata matibabu.
Aliomba kibali kesi hiyo iahirishwe hadi Mramba atakaporejea akidai ugonjwa unamsumbua umeathiri uwezo wake wa kuongea na hakuna mtu anayeweza kujibu maswali badala yake.
Wakili wa Serikali, Osward Tibabyekoma alidai hana pingamizi na ombi la kibali lakini aliomba ushahidi wa mshitakiwa huyo usimame na upande wa utetezi ulete mashahidi wengine wakati mshitakiwa huyo akipatiwa matababu ili kesi hiyo iishe haraka.
Hata hivyo hoja hiyo ilipingwa na Wakili Msuya akidai kwa mujibu wa sheria mshitakiwa anatakiwa kuwepo mahakamani kusikiliza kesi yake na hoja ya Tibabyekoma ingekubalika endapo anayetoa ushahidi angekuwa shahidi na siyo mshitakiwa.
Hakimu Rumanyika alikubali ombi la upande wa utetezi na kuahirisha kesi hiyo hadi Septemba 16 na 20 mwaka huu itakaposikilizwa mfululizo kwa siku nne. Kwa mujibu wa Wakili huyo Mramba anatarajia kusafiri Agosti na matibabu yake yanaweza kuchukua wiki mbili.
Mbali na Mramba, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu wa zamani wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja.
Wanadaiwa kati ya Agosti, 2002 na Juni 14, 2004 jijini Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa umma walitumia vibaya madaraka yao na kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 11.7 kwa kutoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya M/S Alex Stewart ya nchini Uingereza kinyume cha sheria.