KESI YA LWAKATARE YAAHIRISHWA HADI APRILI 30...
https://roztoday.blogspot.com/2013/04/kesi-ya-lwakatare-yaahirishwa-hadi.html
Wilfred Lwakatare wakati wa kusikilizwa kesi dhidi yake. |
Kesi ya ugaidi inayomkabili Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare na mwenzake Ludovick Joseph, imeahirishwa hadi Aprili 30 mwaka huu.
Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Aloyce Katemana aliahirisha kesi hiyo jana kwa kuwa jalada la kesi lipo Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Kabla kesi hiyo haijaanza kusikilizwa kutokana na upelelezi kutokamilika, imefikishwa Mahakama Kuu ambako Lwakatare amepeleka ombi la kuitaka ifanye marejeo katika mwenendo wa majalada ya kesi mbili za ugaidi zilizofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Awali washitakiwa hao walifikishwa mahakamani Kisutu Machi 18 mwaka huu na kusomewa mashitaka, hata hivyo Machi 20 mwaka huu Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) alifuta mashitaka dhidi yao na kuwafungulia tena mashitaka hayo upya.
Katika mashitaka yao, wanadaiwa Desemba 28 mwaka jana katika eneo la King’ong’o Kimara Stop Over Wilaya ya Kinondoni Dar es Salaam, walipanga njama ya kutenda kosa la jinai la kutumia sumu kumdhuru Mhariri wa gazeti la Mwananchi, Dennis Msacky.
Katika shitaka linalomkabili Lwakatare, inadaiwa aliruhusu mkutano kati yake na Joseph ufanyike nyumbani kwake katika eneo la King’ong’o kwa lengo la kuhamasisha vitendo vya ugaidi.