BINTI ABAKWA KWA KUKOSA SENTI 20 TU...

KUSHOTO: Joseph Moran. JUU: Kituo alichopandia basi binti huyo. CHINI: Bustani ya Uwanja wa Recreation alikobakwa binti huyo.
Akiwa hajui la kufanya usiku wa manane majira ya saa 9 alfajiri wakati wa moja ya usiku wa baridi sana katika mwaka.
Mwanafunzi wa sheria mwenye miaka 22 alimwomba dereva wa basi kumruhusu apande lakini dereva huyo akakataa kabisa kisa tu binti huyo kapungukiwa Senti 20 katika nauli aliyotakiwa kulipa ya Pauni za Uingereza 5 kuweza kumfikisha nyumbani kwake.
Hakuna hata abiria mmoja aliyemsaidia, na kumwacha mikononi mwa mbakaji katika tukio la mfano mbaya wa kutokujali wengine.
Joseph Moran mwenye miaka 19, alimrukia ghafla wakati mlengwa wake alipoanza kutembea kwa miguu kuelekea nyumbani. Alimshambulia vibaya sana kiasi cha mama yake kushindwa kumtambua.
Moran, ambaye anatuhumiwa pia kwa makosa kadhaa ya uporaji wa kutumia silaha na kushambulia, alipatikana na hatia ya kubaka na kujeruhi mbele ya Baraza la Mahakama Kuu ya Nottingham juzi.
Jaji James Sampson aliahirisha hukumu hadi Julai 27 kwa taarifa, lakini alimhakikishia Moran hukumu ya haraka kuinusuru jamii.
Aliongeza: "Vyovyote hukumu ilivyo, lazima itakuwa ya muda mrefu. Hili lilikuwa kosa la mauti."
Shambulio hilo lilitokea Desemba, mwaka jana. Kamera za CCTV zimeonesha msichana akimuomba dereva wa basi kwa muda wa dakika nane kabla ya kuondoka kivyake.
Abiria wengine kadhaa wanaonekana wakipanda basi wakati binti huyo akiomba kuruhusiwa kuingia. Hakuna yeyote aliyejitokeza kumuazima hizo Senti 20 alizokuwa akihitaji.
Akizungumza baada ya hukumu, ofisa anayehusika na kesi hiyo alihoji sababu abiria wengine waliopanda basi hilo wakati binti huyo akibembeleza kuruhusiwa kushindwa kumuazima Senti 20 alizokuwa akihitaji kukamilisha safari yake ya maili 14 hadi kwake.
Mpelelezi Mkuu Inspekta Rob Griffin kutoka kituo cha polisi cha Nottinghamshire alisema: "Inashawishi kuanza kulaumiana, na mmoja anaweza kujaribu kumlaumu dereva wa basi.
"Lakini kama binti huyo angefanikiwa kupanda basi, nadhani angemshambulia mwingine yeyote. Mtu pekee wa kulaumiwa ni Joseph Moran.
"Ni vigumu kuwaongelea abiria wengine kwenye basi na walifanya hukumu usiku ule. Wakifahamu nini wanachokijua sasa, wangempatia hizo Senti 20."
Katika picha hizo za kamera ya CCTV, wanaonekana wanaume kwa wanawake wakipishana kila mmoja akijaribu kuwahi kiti kwa ajili ya safari ya kurudi nyumbani kutoka katikati ya mjini wa Nottingham.
Ulikuwa usiku wa baridi kali Desemba, ambapo halijoto ilikuwa chini ya nyuzi 5 lakini hali miongoni mwa wasafiri ilikuwa ya kisherehe.
Hatahivyo, roho ya usamaria mwema miongoni mwao ilikuwa chini mno. Kwa dakika nane, kwa mujibu wa picha hizo, abiria walidharau maombi ya binti huyo mwenye nywele nyeusi aliyekuwa kasimama kando ya dereva.
Binti huyo alikuwa akinywa na rafiki zake kwa matumaini ya kupata basi la usiku la Pronto kumrejesha nyumbani kwa wazazi wake ambao wanaishi umbali wa dakika 20. Ni usafiri aliokuwa akitumia mara kwa mara.
Kwa msisitizo, binti huyo ambaye alipungukiwa kiasi hicho cha pesa, alizidi kumuomba dereva amvumilie hadi atakapofika kwenye mashine ya kutolea fedha (ATM).
Ombi lake hilo liliishia kwenye masikio ya kiziwi. Hivyo binti huyo akaomba kama anaweza kulipa fedha hizo siku nyingine au ampatie fedha atapokutana na mama yake kwenye kituo cha mwisho.
Aliweka mikono kwenye mifuko ya koti lake akiwatazama kwa jicho la kuomba msaada abiria wengine waliokuwa wakimkodolea macho akitumaini mmojawao atajitolea kumlipia Senti 20 alizohitaji.
Haikuwa hivyo na dereva kumuamuru ashuke kutoka kwenye basi. Kilichotokea baadaye lazima kitamuumiza dereva huyo na abiria wengine milele sababu, upande mwingine wa Bustani ya Uwanja wa Recreation, Joseph naye alikuwa njiani kuelekea kwake.
Akiwa amekunywa bia na Bacardi, alikuwa ametoka tu kuachiwa mwaka huo huo, baada ya kutumikia nusu ya kifungo cha miezi minane kwa kosa la uporaji wa kutumia silaha na makosa mengine.
"Kiwango cha uhalifu katika shambulio hili kiliwa kikubwa ambacho kimemshitua kila mmoja. Hakipimiki ni neno pekee linaloweza kusemwa.
Akiwa amechanganyikiwa na mwenye hasira ya kushindwa kumpata rafiki yake wa kike kwenye simu, akamuona mlengwa wake akikatiza mbele yake. Chini ya nusu saa baada ya kushushwa kwenye basi, Moran alimshambulia kwa fujo mwanafunzi huyo. alimkaba shingoni na kumburuta kwenye bustani.
Alimbaka, kisha kumpiga vibaya sana kiasi cha mama yake aliyefika eneo la tukio baadaye kushindwa kumtambua binti yake.
Moran aliweka mikono yake kichani juzi wakati Baraza la Mahakama Kuu ya Nottingham kumtia hatiani.
Binti huyo ambaye ameelezewa kuwa ni maarufu anayetokea kwenye familia yenye upendo, wacha Mungu, alishindwa kuhudhuria mahakamani kutokana na kuwa kwenye mitihani.
Alikuwa pia kwenye mitihani siku ya shambulio, ambapo baadaye alisafiri kwenda Nottingham kushiriki maonesho ya Krismasi na kupata chakula cha pamoja na marafiki zake. Alirejea katikati ya mji huo jioni, na kufikia kwenye klabu ya usiku kabla ya kufanya mipango ya kurejea nyumbani. Lakini dereva wa basi akasitisha kila kitu.
Nilikuwa nikihesabu kiasi gani cha fedha nilichonacho," aliwaeleza polisi baadaye. "Nakumbuka nilipungukiwa Senti 20, inawezekana zaidi ama pungufu kidogo ya kiasi hicho. Nakumbuka kuwa na majibizano na dereva wa basi. Nilisema nimepungukiwa na kuomba kama naweza kupanda hivyo hivyo na akanijibu Hapana.
Ni kweli makampuni ya mabasi yamekuwa yakipambana vikali na wazamiaji. Lakini hapa alikuwa msichana mdogo, peke yake, mida mibovu, akiwa na sehemu kubwa ya nauli inayotakiwa mkononi, kaahidi kumpigia simu mama yake kuandaa malipo mara tu atakapofika kituo anachokwenda.
Badala yake akatelekezwa peke yake kwenye usiku wa baridi kali kutafuta njia mbadala ya kufika nyumbani.
"Kilichotokea siku hiyo hakika ni tukio la kushitusha mno," alisema Alex Hornby, Mkurugenzi wa Biashara wa Kampuni ya Mabasi ya Trent Barton inayomiliki mabasi ya Pronto.
"Mara tu baada ya tukio hilo, uchunguzi kamili wa kina ukaanza."
Kilichogundulika katika uchunguzi huo hakikuweza kufahamika na hata walipofuatwa, madereva wa kampuni hiyo walificha utambulisho wa mwenzao.
"Huwezi kupata chochote kutoka kwetu," alisema mmoja wa maofisa. "Uongo umesemwa mahakamani na hatuchangii chochote kuhusu ambacho anaweza kuwa alifanya ama kutofanya dereva. Magazeti yanasema abiria alisukumwa nje ya basi. Tunafikiri kinyume chake."

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item