NYUKI WAZUSHA TAFRANI MSIBANI MOSHI VIJIJINI...

Paroko wa Parokia ya Mkombole ya Kanisa Katoliki, aliyetajwa kwa jina moja la Ephraim amelazimika kuweka kando shughuli za maziko na kutimua mbio baada ya makundi matano ya nyuki kuvamia waombolezaji mara baada ya kuzika.
Katika tukio hilo la aina yake, Paroko Ephraim na Mwenyekiti wa Halmashauri wa Wilaya ya Moshi Vijijini, Morris Makoi walijikuta wakikimbia waombolezaji na magari yao ya kifahari kwenda kujificha mashambani kuepuka kudhuriwa na nyuki hao.
Kabla ya nyuki hao kuvamia msiba huo juzi, Paroko Ephraim aliwaongoza waomboleza kumzika Agnes Malya (30) katika kijiji cha Osaki, Kibosho wilayani Moshi Vijijini aliyefariki hivi karibuni kwa maradhi.
Baada ya maziko, Paroko Ephraim, Makoi walikaribishwa na kukaribia katika chakula kilichoandaliwa kwa waombolezaji wote kijijini hapo.
Hata hivyo, wakati waombolezaji wakijipanga kushiriki chakula hicho, ghafla walijitokeza nyuki wakiwa katika makundi matano na kuvamia waombolezaji waliokuwa hata hawajagusa chakula hicho.
Uvamizi huo ulisababisha Mwenyekiti wa Halmashauri wa Wilaya ya Moshi Vijijini, Makoi na Paroko Ephraim kutangulia kutimua mbio kuokoa roho zao baada ya kushambuliwa na kung'atwa na kundi la nyuki walioibuka na kuvamia msibani huo na kufuatwa na mamia ya waombolezaji wengine.
“Marehemu aliacha wosia kutokana na ndugu wa marehemu mumewe kukataa kuchangia matibabu yake wakati akiwa hospitali, basi wasije wakajidai kuandaa sherehe wakati akifa kwa kupika vyakula, pombe na viywaji.
“Sasa si mnaona shughuli ya kumzika imekwenda vizuri ila kabla watu hawajala ndio nyuki wakajitokeza?” alisema mmoja wa ndugu wa marehemu ambaye hakutaka jina lake litaandikwe.
Muombolezaji mwingine, Gerad Temba aliwalaumu ndugu wa marehemu kwa kukiuka wosia wa dada huyo aliyeweka bayana kwamba asingependa sherehe na madoido ya aina yoyote katika msiba wake.
“Kabla na wakati wa mazishi nilikuwa nikikumbusha alichosema marehemu, lakini hawakutaka kusikia sasa matokeo yake ndio haya,“ alisisitiza Temba.
Akizungumzia kisa hicho, Makoi ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ukaoni alisema ni mara ya kwanza kuona tukio la namna hiyo na limemshtua mno.
“Tulilazimika kukimbia mbio kuokoa maisha yetu, ni tukio la kushangaza sana nyuki wengi kiasi kile kutokea kusikojulikana na kuanza kushambulia waombolezaji kabla ya kumaliza shughuli za mazishi.
“Kuna tetesi kuwa marehemu hakutaka chakula wala pombe na vinywaji wakati wa mazishi yake vitu ambavyo alisema gharama zake zingetosha kumtibu ugonjwa uliomwua, sasa sina hakika kama ni kweli,” alidai Makoi.
Baadhi ya waombolezaji walikimbizwa katika vituo vya afya vilivyopo karibu na kijiji hicho akiwamo wifi wa marehemu ndiye aliyeandaa chakula katika msiba huo, Mery Sembeki.
Sambeke aliumwa na nyuki mwili mzima na kulazimika kuvua nguo na baadaye alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC ambako alitundikiwa maji ya dawa.
Majeruhi wengine 8 walikimbizwa katika Hospitali ya Misheni ya Kibosho ambako walipatiwa huduma ya kwanza na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Pia kutokana na kizaazaa hicho, chakula na vinywaji vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 5 vilimwagwa jana asubuhi kama ishara ya kutimiza alichokisema marehemu Agnes. 
Wakizungumzia tukio hilo, baadhi ya waombolezaji walishauri jamii kubadili mtizamo wake kwa kuchangia mambo ya msingi kama wagonjwa katika matibabu badala ya kutoa michango mikubwa wakati mgonjwa anapofariki.
“Tutalazimika kubadilika, badala ya kuchanga mamilioni kwenye mazishi tuchange kumnusuru mgonjwa ili yeye mwenyewe atambue mchango ule badala ya kuchangia maiti” alisema mmoja wa waombolezaji ambaye hakupenda jina lake litajwe.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item