ASILIMIA 84 YA GESI KUBAKI MTWARA...

Yona Killagane.
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limewatoa wasiwasi wananchi wa Mtwara kuhusu gesi itakayosafirishwa kwenda Dar es Salaam kwa kuwa zaidi ya asilimia 84 ya gesi hiyo, itabaki mkoani humo.
Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Yona Killagane alisema hayo jana wakati akijibu hoja ya Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM) aliyetaka kujua shirika hilo linachukuliaje hoja za wananchi wa Mtwara kuhusu kutandazwa kwa bomba hilo la gesi kwenda Dar es Salaam.
“Gesi itakayotumika ni iliyopatikana kwenye kina kirefu cha maji, ambapo ni umbali wa kilometa 80 kutoka nchi kavu, lakini Serikali imeamua mitambo yote ya kuzalisha gesi iwe nchi kavu na gesi itakayopelekwa Dar es Salaam ni asilimia 16 tu na itakayobaki Mtwara ni asilimia 84,” alisisitiza.
Alisema mpango wa uzalishaji na usambazaji gesi hiyo unaonesha kuwa, wakati bomba hilo linatandazwa kutakuwa na matoleo maalumu kwenda viwandani katika maeneo 10 ya Mtwara, Lindi na Mkuranga ya kusindika gesi.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huo, kwa sasa Tanzania ina uwezo wa kuzalisha futi za ujazo trilioni 35 za gesi, kati ya hizo, futi za ujazo trilioni 26.57 zinatokana na gesi inayozalishwa kwenye maji ya kina kirefu na futi za ujazo trilioni 1.42 zinatokana na gesi inayozalishwa nchi kavu.
Alifafanua kuwa gesi inayozalishwa ni lazima ifanyiwe usindikaji na kubadilika kutoka mfumo wake wa hewa na kuwa kimiminika, ili isafirishwe na inapofika inakosafirishwa pia husindikwa na kugeuka hewa kwa matumizi.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Kabwe Zitto  alitaka kujua hatua zilizochukuliwa na shirika hilo katika kuelimisha wananchi kuhusu matumizi ya gesi hiyo.
Akijibu hoja hiyo, Killagane alisema tayari wameshirikiana na uongozi wa Mtwara kuanzisha programu za kuelimisha wananchi kuhusu manufaa watakayopata kupitia mradi huo.
Hata hivyo, Mangungu aliendelea kuibana TPDC na kuwataka wahakikishe kuwa kasi wanayoitumia katika kuendeleza mradi huo wa gesi, waitumie pia katika kusambaza elimu zaidi kwa wananchi, ili kupunguza matukio ya uvunjifu wa amani na maandamano yasiyo na lazima.
Zitto alilibana shirika hilo na kutaka mkataba wa ujenzi wa bomba la gesi baina ya Serikali na kampuni ya Kichina inayojenga bomba hilo, uwasilishwe mbele ya Kamati hiyo kwa uchunguzi zaidi, huku akisisitiza juu ya umuhimu wa kuwapo Sheria ya Matumizi ya Gesi na Sera.
Baadhi ya wananchi wa Mtwara wakihamasishwa na vyama vya siasa, waliandamana kwa kutembea mwendo wa kilometa tisa kutoka Mtwara mjini hadi Msimbati ambako gesi asilia inavunwa na kutangaza mikakati ya kupinga mpango wa Serikali wa kusafirisha nishati hiyo kutoka mkoani humo hadi Dar es Salaam.
Maandamano hayo ambayo yaliandaliwa na kupokewa na viongozi wa vyama tisa vya upinzani na asasi kadhaa zisizo za kiserikali, yalikuwa na mabango yenye ujumbe wa kupinga hatua hiyo ya Serikali.
Baada ya maandamano hayo, viongozi wakubwa wa kisiasa wa upinzani waliunga mkono hatua hiyo licha ya Serikali kuwapa taarifa za manufaa yatakayopatikana Mtwara.
Kutokana na ufafanuzi wa TPDC, hoja za gesi ya Mtwara zilizokuwa zikiendeshwa kisiasa zilipotea na Kamati ikajielekeza katika matumizi na mapato ya shirika hilo.
Kamati ilitaka shirika hilo lijieleze upya na kuwasilisha taarifa yake kwa Kamati hiyo kabla Bunge la Februari halijaisha, kuhusu fedha za mafunzo ambazo ni dola za Marekani milioni tatu zinazotolewa na kampuni za mafuta kila mwaka.
“Hamjafuata maagizo yetu tuliyowapa tukiwa na Kamati ya Nishati na Madini mara ya mwisho tulipokutana; tuliagiza asilimia 50 ya fedha hizo iundiwe mfuko ambao mtautangaza kwenye vyombo vya habari, ili kuwezesha Watanzania wanaotaka kusoma kupata fursa hiyo, lakini hapa tunaona fedha hizi mmezipeleka serikalini, tunataka maelezo,” alisisitiza Zitto.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item