MATAJIRI 17 WALIOCHANGIA BILIONI 2 KKKT WAINGIA MATATANI...

Askofu Mkuu Thomas Laizer.
Baadhi ya wachungaji, wainjilisti na washarika wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, Arusha wamepinga mpango wa viongozi wa Dayosisi hiyo kutaka ‘kubinafsisha’ mali za Kanisa hilo kwa matajiri 17 wa jijini hapa.
Mpango huo ulibuniwa na viongozi waandamizi wa Dayosisi hiyo, wakiongozwa na Mkuu wa Dayosisi, Askofu Thomas Laizer ikiwa ni jitihada za kuokoa mali za Dayosisi hiyo zisipigwe mnada na benki baada ya kushindwa kurejesha mikopo.
Mali za Dayosisi hiyo zenye thamani ya mabilioni ya fedha ambazo zimejengwa kwa jasho la waumini wa Kanisa hilo na sasa ziko hatarini kufilisiwa ni pamoja na hoteli ya kitalii ya Arusha Corridor Springs na Hospitali ya Rufaa ya Seliani zilizopo jijini hapa.
Mikopo hiyo yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 11 ilitolewa na benki (jina linahifadhiwa kwa sasa) ili kujenga mali hizo zilizotarajiwa kuwa vitega uchumi vya Kanisa lakini inadaiwa ufisadi umesababisha deni hilo kushindwa kulipwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika ibada ya kumsimika Mwinjilisti Yesse Solomon Mushi wa Usharika wa Kijenge  kuwa Mchungaji juzi, wachungaji hao ambao hawakutaka majina yao yaandikwe kwa kuhofia ‘kushughulikiwa’, walipinga mali zao kupewa matajiri wachache.
Ibada hiyo iliongozwa na aliyekuwa Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT, Askofu mstaafu Dk Erasto Kweka  na Mchungaji Mushi sasa anakuwa Mchungaji Kiongozi katika Usharika wa Shambarai
Wachungaji hao walisema: “Sikiliza ndugu mwandishi, hatuwezi kukubali mali zilizopatikana kwa sadaka zetu na jasho letu wakabidhiwe matajiri 17 bila sisi kuelezwa kinaga ubaga kitu gani kimetufikisha hapa na nani anahusika na anawajibishwa vipi?” alisema Mchungaji mmoja aliyeonekana wazi kuwa na hasira na kuongeza:
“Huwezi kuwakabidhi kienyeji matajiri wachache mali za washarika zaidi ya 600,000 wa Kanisa letu kwa kisingizio chochote kile, kwani mali zile si za Askofu Laizer wala Karyongi (Katibu Mkuu wa Dayosisi), ni mali zetu na hakuna wa kuzichezea watakavyo bila ya ridhaa yetu.” 
Mchungaji mwingine ambaye kwa sababu zinazoeleweka hakutaka jina lake litajwe alisema kuwa washarika wanaelewa kuwa kuna mtandao wa ufisadi ndani ya Dayosisi hiyo unaojumuisha viongozi waandamizi watano (majina tunayo) ambao sasa umeamua kuuza na kugawa mali za Dayosisi kwa marafiki zao.
“Tunawafahamu na tumewavumilia kwa muda mrefu mafisadi hao tukidhani watajirekebisha, lakini sasa kwa hatua waliyofikia ya kutaka kuwapa mali zetu marafiki zao,tena chee,tumeamka na kamwe hatukubali hilo labda tukiwa makaburini.
“Tunajua wamejipanga na kila anayehoji chochote anashughulikiwa kwa kuzushiwa kila ubaya, lakini sasa zamu yao ya kushughulikiwa nayo imefika kwa sababu Mungu hamfichi mnafiki na anamuumbua pale pale na lazima waumbuke,” alisisitiza Mchungaji huyo.
Msharika aliyejitambulisha kwa jina moja la Sayore, alisema hawako tayari kuitika mwito wa Askofu Laizer wa kila msharika kuchangia Sh 20,000 kwa sababu hawana imani na kiongozi hata mmoja wa Dayosisi hiyo.
“Nakwambia hapa, hata wakisema tuchangie thumuni (senti 50) hakuna atakayetoa, kwa aina ya viongozi waliopo kwa sasa, labda wachukue hatua zitakazoturidhisha kwamba kweli wana uchungu na mali za Dayosisi yetu, vinginevyo tunasubiri mali hizo zifilisiwe halafu wataona cha moto,” alisisitiza bila kufafanua.
Kwa mujibu wa nyaraka ya kuwataka matajiri hao 17 kunusuru mali za Dayosisi hiyo, Askofu Laizer aliwaita na kukutana nao Agosti 4, mwaka jana katika hoteli ya Arusha Corridor Springs ambako aliwaomba wachangie Sh milioni 100 kila mmoja ili kuokoa jahazi.
Siku tatu baadaye, Agosti 7,  Askofu Laizer aliandika barua rasmi kwa kila tajiri akiwakumbushia waliyokubaliana katika kikao cha Agosti 4, na umuhimu wa kutekeleza makubaliano ili kuokoa mali za Dayosisi.
“Kiasi cha fedha  utakachotoa kwa ajili ya kunusuru hali iliyopo, kitakuwa ni sehemu ya hisa zako utakazonunua katika kampuni ya uwekezaji ya Arusha Lutheran Investment Company(ALUICO) au kurejeshwa kwako kwa makubaliano tutakayofikia katika uendeshaji wa hoteli,” ilisema sehemu ya barua hiyo ya Askofu Laizer kwa mmoja wa matajiri hao na kuongeza:
“Pamoja na ombi hili nakuomba uhudhurie kikao kingine kilichopangwa kufanyika Agosti 13, 2012 saa 9 alasiri katika Hoteli ya Arusha Corridor Springs.”

Post a Comment

  1. Appreciate this post. Let me try it out.

    Feel free to surf to my weblog: diet plans that work

    ReplyDelete

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item