MGOGORO KANISA LA KKKT SASA WAIBUKIA KWINGINE...

Sakata la ubadhirifu na ulaji fedha ndani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati, sasa limeibuka katika Usharika wa Ngaramtoni, Arumeru mkoani Arusha baada ya Askofu wa Jimbo la Arusha Magharibi, Godwin Lekashu kutuhumiwa kutafuna fedha za harambee za usharika huo zaidi ya Sh milioni 24.
Wiki iliyopita, Baraza la Wazee la Usharika wa Ngateu uliopo ndani ya jimbo hilo, ulimkataa Askofu Lekashu kufanya shughuli zozote ikiwamo za ibada,  kwa madai kuwa Askofu huyo ndiye chanzo cha mgogoro wa Kanisa hilo na kusababisha mchungaji Philemon Mollel kufukuzwa na kusimamishwa shughuli za kichungaji katika kanisa hilo nchini.
Habari kutoka Usharika wa Ngaramtoni, zilisema fedha hizo zilikuwa za kwaya ya Usharika huo baada ya kuendeshwa harambee na Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo, Machi 11 mwaka jana.
Vyanzo vyetu vilidokeza kuwa kiasi hicho cha fedha, kilipatikana siku hiyo, ikiwa ni pamoja na ahadi na fedha taslimu; na kwa kuwa kwaya hiyo haikuwa imefungua akaunti benki, fedha zilikabidhiwa kwa Askofu Lekashu na Mwinjilisti Christopher Daniel ili azihifadhi katika akaunti ya Usharika.
Inadaiwa kuwa miezi miwili baadaye, uongozi wa Kwaya uliomba fedha hizo kutoka kwa Askofu huyo, kwa lengo la kufanya ununuzi wa vitu vilivyokusudiwa, lakini Askofu hakutoa ushirikiano na kutoa vitisho kwa viongozi wa kwaya wenye ‘kiherehere’ cha kuulizia fedha hizo.
Vyanzo vilisema uongozi wa kwaya, ulisimama kidete kutaka fedha hizo na ulikuwa tayari kufukuzwa kwa ajili hiyo; na ndipo Askofu Lekashu alipoamua kutoa Sh milioni 7 tu, hali iliyowakatisha tamaa wanakwaya wa usharika huo.
‘’Huku ndani ya KKKT hali ni mbaya sana, kuna ‘mchwa’ wa kula fedha za waumini na wakubwa wa Kanisa, ndio wanaoongoza kula fedha na ukiwa mstari wa mbele kukemea hilo unafukuzwa kazi, sasa ni wakati wa kutoa siri zote za Kanisa hili,’’ alisema mtoa habari wetu.
Alipopigiwa simu, Askofu Lekashu hakutoa ushirikiano wa kutoa ufafanuzi wa tuhuma hizo, zilizoelekezwa kwake na badala yake alifoka na kumtaka mwandishi wa habari kuwasiliana na uongozi wa juu wa Dayosisi kwa ufafanuzi.
Askofu Lekashu alipoambiwa kuwa tuhuma hizo si za uongozi wa juu ni zake binafsi kama Askofu, alipinga kutoa ufafanuzi na kusema: “Wasiliana na uongozi wa Dayosisi.
“Nimekuambia acha kunisumbuasumbua na leo iwe mwisho kunipigia simu juu ya mambo ya Kanisa… wenye kuweza kueleza mambo ya Kanisa ni viongozi wa juu wa Dayosisi,’’ alisema Askofu Lekashu na kukata simu. 
Wakati hayo yakiibuka ndani ya usharika huo, Usharika wa Ngateu Jumapili iliyopita ulitoa tamko la kumkataa Askofu Lekashu kuendesha ibada katika usharika huo na jimbo kwa jumla, kwa madai kuwa ndiye chanzo cha Mchungaji Mollel kufukuzwa, kwani amekuwa akitoa taarifa zisizo sahihi kwa uongozi wa juu wa Dayosisi.
Wazee hao wa Baraza walisema uamuzi huo umetolewa baada ya kufanya uchunguzi wa kina na kugundua kuwa Askofu Lekashu ni tatizo ndani ya kanisa hilo, hivyo hawamhitaji kuendesha ibada kanisani na hata katika misiba ya waumini wa jimbo hilo.
Mbali ya hilo, usharika huo uliazimia tangu Jumapili kutopeleka asilimia 40 ya sadaka kama mchango wa maendeleo ya Dayosisi hadi Mchungaji Mollel atakaporejeshwa kazini na kuendelea na shughuli za kichungaji.
Wazee hao pia waliutaka uongozi wa Dayosisi, kumrudisha Mchungaji huyo bila masharti, kwani kwa kumrudisha kwa masharti ikiwa ni pamoja na kumtaka aombe radhi ni kupoteza muda, kwani halitafanyika kabisa.
Mchungaji Mollel alisimamishwa na kufukuzwa, akidaiwa kukiuka kanuni za KKKT. Lakini, ilielezwa chanzo ni msimamo wake wa kupinga ubadhirifu ndani ya kanisa hilo, hasa katika miradi, ikiwamo ya hoteli ya kitalii ya Arusha Corridor Springs iliyosababisha deni la Sh bilioni 11 na hivyo kuweka mali za kanisa katika hatari za kufilisiwa na benki moja nchini.
Wakati huo huo, kikao baina ya uongozi wa juu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati na Baraza la Wazee wa Usharika wa Ngateu, kilichokuwa kifanyike jana chini ya Msaidizi wa Askofu, Solomoni Massangwa, kimeahirishwa kwa kinachodaiwa kuwa ni Askofu kuwa na udhuru, ambao hata hivyo haukuelezwa ni wa aina gani.
‘’Tumepewa taarifa kuwa kikao kimeahirishwa leo (jana) na hakuna taarifa nyingine iliyosema kitafanyika lini na sisi tunaendelea na mikakati mingine,‘’ alisema mtoa habari wetu.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item