MKAGUZI MKUU HESABU ZA SERIKALI ATAKA HADHI SAWA NA BENKI KUU...

Ludovick Utouh.
Siku moja baada ya uongozi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutoa maoni ya Katiba mpya na kupendekeza mambo kadhaa yawemo, ikiwa ni pamoja na kumtaka Rais asifanye uteuzi wa moja kwa moja wa wajumbe wake, ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) nayo imetaka iwe taasisi huru.
Maoni hayo yalitolewa jana na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dar es Salaam.
Akiwasilisha maoni ya ofisi yake, alisema wanataka ofisi hiyo iwe kama ilivyo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) au Benki Kuu ya Tanzania ( BoT)  ili iwe na uhuru, hata wa kuajiri.
“Kuna wakati hata tukihitaji kuajiri mtu tunashindwa, kwani tunatakiwa kuanza kuandika barua serikalini, hivyo ni vema tukajitegemea kama ilivyo kwa taasisi nyingine,” alisisitiza.
Alibainisha kuwa si kwamba anataka ofisi hiyo iwe na nguvu kubwa  kiasi ambacho wakibaini suala ofisi hii ihusike kufungua mashitaka, bali watawasiliana na taasisi zenye jukumu la kushughulikia suala hilo.
Alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa kufanyia uchunguzi haraka taarifa za fedha zinazoonekana kuwa na utata.
Mbali ya Utouh, wengine waliotoa maoni yao jana ni mwanasiasa mkongwe nchini, Sir George Kahama ambaye hakuwa tayari kuzungumzia maoni yake na Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Didas Masaburi.
Juzi, uongozi wa NEC ukiwasilisha maoni yake kwa Tume, ulishauri Katiba imtake Rais asifanye uteuzi wa moja kwa moja wa viongozi wa Tume na badala yake kuwe na mchakato wa uteuzi wa wajumbe kuanzia kwa kamati ya wataalamu, jopo maalumu la Watanzania wanaokubalika katika jamii, wathibitishwe bungeni na ndipo Rais afanye uteuzi.
Aidha, baada ya uteuzi wajumbe waapishwe na Jaji Mkuu wa Tanzania, badala ya Rais kama ilivyo sasa. Walishauri pia kubadilishwe jina la Tume, kuwe na mahakama ya masuala ya uchaguzi, mbunge aruhusiwe kuhama chama na `kofia’ ya ubunge na pia kuwe na mgombea binafsi.
Mapendekezo hayo yaliwasilishwa mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva.
Alisema ni vema Katiba mpya ikaanzisha utaratibu wa uwazi zaidi wa uteuzi utakaojumuisha wadau wa uchaguzi kwa njia moja au nyingine, ikihusisha wataalamu wa masuala ya uchaguzi, sheria na jamii kisha mapendekezo yapelekwe bungeni kabla ya kuwasilishwa kwa Rais kwa uteuzi rasmi.
Kwamba, vyombo hivyo vitatu katika hatua tofauti vipendekeze majina ya wajumbe wa Tume na baadaye kuwasilishwa kwa Rais ili ateue mwenyekiti na makamu mwenyekiti miongoni mwao, itaondoa dhana ya wajumbe hao kuwa na utii kwa Rais.
Kuhusu kubadili jina, alisema Tume inapendekeza kuanzishwa kwa tume huru ya uchaguzi itakayojulikana kama Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ili kutoa sura kuwa uhuru wa Tume unaanzia kwenye jina.
Alisema Katiba ndiyo sheria mama, hivyo mambo yote ya msingi ya nchi huanzia kwenye Katiba, na hivyo kubadilishwa jina na kuweka neno ‘huru’ kunaweza kubadili fikra za wadau juu ya Tume ya Uchaguzi.
Aidha, NEC imependekeza kuwapo sheria itakayotoa mwanya kwa uamuzi wake kuhojiwa mahakamani, badala ya kusubiri wakati wa kuwasilisha kesi ya uchaguzi, hivyo kutaka Katiba mpya ipanue wigo wa demokrasia kwa kuanzisha mahakama ya mambo ya uchaguzi ili kuwezesha wadau au wananchi ambao hawakubaliani na uamuzi wa tume kupata nafasi ya kukata rufaa.
Jaji alisema licha ya Tume kupendekeza kuendelea na utaratibu wa uchaguzi mdogo, bado kuna umuhimu wa Katiba mpya kutoa utaratibu wa kudhibiti vyama vya siasa na wanasiasa kuhama na kufukuzana ndani ya vyama bila kuathiri nafasi ya uwakilishi ya kiongozi husika.
Kwamba, mbunge awe na haki ya kuhama chama na kiti chake cha  uwakilishi, huku ikishauri pia kuwe na mgombea binafsi katika uchaguzi.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item