HATIMAYE VITAMBULISHO VYA TAIFA VYAZINDULIWA RASMI...

Rais Jakaya Kikwete akizindua rasmi vitambulisho vya Taifa kwenye Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam, jana.

Vitambulisho vya Taifa ni moja ya vitu muhimu kwa Mtanzania na havipaswi kuchezewa ikiwa ni pamoja na ukiukaji wa masharti ya utoaji wao.
Kwa kutambua umuhimu huo, Rais Jakaya Kikwete, amesema hatakuwa na msamaha kwa watendaji wa Serikali watakaokiuka masharti na kuvitoa kwa watu wasiohusika.
Alitoa onyo hilo jana Dar es Salaam, wakati akizindua mfumo wa usajili na utambuzi wa watu na utoaji wa vitambulisho hivyo.
“Naomba asije mkimbizi au mgeni akapewa kitambulisho cha mkazi, namaanisha epukeni kumpa mtu kitambulisho asichostahili, eti tu kwa sababu ya ‘kitu kidogo’, kuweni macho katika hili,  kwani atakayebainika hatutakuwa na msalie Mtume naye,” alionya Kikwete.
Alisisitiza hatokubali utolewaji wa vitambulisho hivyo vya Taifa, ufanyike kiholela kwa kupewa wasiostahili, kama ilivyo sasa kwa utolewaji wa hati za kusafiria nchini.
“Matatizo tunayopata kwenye utoaji hati za kusafiria, yasiingie kwenye vitambulisho vya Taifa, kule kuna baadhi ya watumishi wasio waaminifu wanapokea fedha na kutoa hati za kusafiria kwa mtu ambaye si mkazi na hili linatuletea shida hadi nchi za nje, hati zetu zinakamatwa,” alisisitiza.
Huku akisisitiza kuwa kamwe hatokubali utolewaji wa vitambulisho hivyo vya Taifa, ufanyike kiholela kwa kupewa wasiostahili, kama ilivyo sasa kwa hati za kusafiria nchini.
Alitaka watumishi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), kuzingatia masharti ya utoaji vitambulisho hivyo na kuonya kuwa watakaokiuka masharti hayo, watachukuliwa hatua za kisheria.
Alisema jambo la msingi ni kwa Watanzania, wageni na wakimbizi wenye sifa kujaza taarifa zao kwa usahihi na watumishi wa Nida kuhakiki taarifa hizo kupitia vyombo husika.
Alitaka watumishi hao kuepuka makosa huku akiwasisitizia viongozi wa serikali za mitaa kuwa makini na wakazi wa maeneo yao. 
Alisema katika suala la utoaji vitambulisho hivyo, ikibainika mtu yeyote awe kiongozi au mwananchi amefanya udanganyifu, bila kujali nafasi yake achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.
Aliagiza  pia Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kuwa makini katika kutoa vyeti vya kuzaliwa. 
“Najua kwa kuwa sasa vitambulisho vimeanza kutolewa na wengi wasio na sifa ya ukazi sasa watakimbilia kwenu kutaka vyeti vya kuzaliwa kutafuta uhalali wao, kuweni makini na hawa wadanganyifu,” alisisitiza.
Pamoja na hayo, Rais Kikwete alipongeza hatua iliyofikiwa na Nida kutoa vitambulisho hivyo kwa mara ya kwanza, huku akiita kuwa ni ndoto ya muda mrefu ya Watanzania iliyotimia.
Alisema mradi wa vitambulisho vya Taifa ulianza 1961 nchi ilipopata uhuru, lakini ilikabiliwa na changamoto ukiwamo ukosefu wa fedha na baadhi ya viongozi wabinafsi, kuukwamisha kutokana na kutaka kujinufaisha wao na watoto wao.
“Leo kwa kujivunia vitambulisho vya kwanza vya Taifa vinatolewa kwa viongozi na yale maeneo yaliyoanza kusajili ambayo ni watumishi wa Serikali wa Dar es Salaam, Kilombero, wabunge na viongozi wakuu.
“Napenda kuwahimiza wananchi wajisajili ili kupata vitambulisho hivi kwani hakuna atakayeachwa awe kijijini au mjini,” alisema.
Alisema vitambulisho hivyo vina faida nyingi na si hiari katika nchi nyingi duniani. Alitaja faida yake kuwa mbali na kulinda mipaka ya nchi, pia vitarahisisha mambo mengi ikiwamo, upigaji kura za maoni ya Katiba.
Pia alisema vitasaidia katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 kwa kuwa vitatumika katika mashirika muhimu kama vile benki, kodi ya bima na hifadhi za jamii.
Alisema kwa sasa hatua inayofuata baada ya vitambulisho hivyo kugawiwa, ni kuendelea na usajili katika maeneo ambayo hayajasajiliwa, huku akitaka maofisa wa ubalozi kusubiri hadi pale watakapoandaliwa utaratibu wa kupata vitambulisho vyao.
Kuhusu changamoto ya ukosefu wa fedha, aliahidi kushughulikia suala hilo na kwamba tayari amezungumza na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa kuhakikisha mradi huo unatengewa fedha. 
“Jamani si mnajua maji ukishayavulia nguo sharti uyaoge, hivi vitambulisho ni muhimu sana vikamilike mapema,” alisisitiza.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi alisema mradi huo unaendelea vizuri, ingawa kutokana na kuhusishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), unatakiwa kukamilika haraka na hivyo changamoto kubwa kuwa upande wa fedha.
Alisema faida za kuchanganya mradi huo na NEC, ni kurahisisha na kupunguza gharama za kuandaa vitambulisho vingine vya kupigia kura za maoni na uchaguzi, lakini pia kumwepusha Mtanzania na usumbufu wa kurejea kutoa taarifa zilezile kwa mara nyingine.
“Kwa hili Mheshimiwa Rais naomba nikunong’oneze usisite kutumia nguvu zako zote ili tufanikishe mradi huu wa vitambulisho,” alisema Dk Nchimbi.
Kuhusu suala la utolewaji holela wa hati za kusafiria, Nchimbi alisema analifahamu na ameanza kulifanyia kazi na atawasilisha ripoti ya utekelezaji wake hivi karibuni kwa Rais Kikwete.
Mkurugenzi wa NIDA, Dickson Maimu, alisema tangu kuanzishwa kwa Mamlaka hiyo mwaka 2008, wamefanikiwa kusajili watumishi wa Serikali mkoani Dar es Salaam, Kilombero na Zanzibar, wabunge na viongozi wa juu na wastaafu.
Alisema baada ya jana kukabidhiwa takribani watu 47 vitambulisho hivyo, akiwemo Rais Kikwete na mkewe, Mama Salma, marais wastaafu Ally Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Amani Abeid Karume, leo Nida inatarajia kutoa vitambulisho hivyo kwa wabunge Dodoma.
Wengine baadhi waliopatiwa vitambulisho hivyo ni pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad, mwanasiasa mkongwe nchini Kingunge Ngombale-Mwiru, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Didas Masaburi na Mkuu wa Mkoa huo, Said Meck Sadiki.
Wengine ni Mkuu wa Jeshi la Polisi, Said Mwema, Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ),  Jenerali Davis Mwamunyange na aliyekuwa Waziri Mkuu, Dk Salim Ahmed Salim.
Wengine ni Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, Mwenyeviti CUF, Profesa Ibrahim Lipumba;  Mkurugenzi Mkuu wa PPF, William Erio, Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi na Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, ambaye hata hivyo hakuwapo.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item