PAPA FRANCIS KUENDESHA MISA JELA YA WATOTO...

Papa Francis (kulia) akizungumza na Benedict XVI walipokutana jana.

Papa Francis amekutana na mtangulizi wake kwa chakula cha mchana, ukiwa ni mkutano wa kwanza kufanyika kwa zaidi ya miaka 600 iliyopita.
Papa Francis aliruka kwa helikopta hadi Kasri ya Gandolfo kwa ajili ya chakula cha mchana cha faragha na Papa mstaafu Benedict jana.
Benedict ameishi katika kasri iliyoko pwani ya ziwa Kusini mwa Roma tangu mwezi jana, alipokuwa Papa wa kwanza katika karne sita zilizopita kujiuzulu, kwa sababu za kiafya.
Hakuna kumbukumbu yoyote ya wazi ya kuwapo kwa mkutano baina ya Papa na mtangulizi wake, kwa kuwa kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki amekuwa akichaguliwa baada ya kifo cha mtangulizi, BBC iliripoti jijini hapa.
Mwaka 1294, Papa Celestine V alijiuzulu baada ya miezi mitano ya upapa. Boniface VIII alichaguliwa siku chache baadaye na mtangulizi wake akawekwa kizuizini. Celestine alifariki dunia katika kipindi cha mwaka mmoja.
Kinyume chake, Papa Francis amekuwa akimzungumza vizuri mtangulizi wake. Moja ya majukumu ya awali aliyofanya akiwa Papa ni kumpigia simu Benedict katika kasri ya Gandolfo, ambako Papa huyo wa zamani alikuwa akifuatilia matangazo ya televisheni.
Papa huyo mstaafu anatarajiwa kuishi katika makazi hayo ya kipapa katika kipindi cha kiangazi hadi makazi mapya yanayoandaliwa kwa ajili yake yatakapokamilika ndani ya kuta za Jiji la Vatican mwishoni mwa Aprili.
Kwa upande wake, Papa Francis leo ataanza msimu muhimu wa liturujia kwa Kanisa kwa kuendesha Misa ya Jumapili ya Matawi katika uwanja wa Kanisa la Mtakatifu Petro.
Baada ya hapo ataongoza liturujia zingine sita wiki ijayo, zikifuatiwa na Misa ya Jumapili ya Pasaka.
Papa huyo mpya alichagua jina la Francis kwa heshima ya Mtakatifu Francis wa Assisi – Mtakatifu wa kitaliano wa karne ya 13 ambaye aliachana na maisha ya anasa ili asaidie masikini.
Papa Francis ameshalitaka Kanisa Katoliki kuwa karibu na watu wa kawaida, hususan masikini na wenye shida.
Papa Benedict hivi sasa ana makatibu wawili na wasaidizi wanne wa kike, huku akilindwa na maofisa wa Polisi wa Vatican.
Wakati huo huo, imeelezwa kuwa Papa Francis atafanya sherehe kubwa wiki ijayo katika Kanisa dogo la gereza la vijana badala ya Vatican au katika Kanisa Kuu la Roma ambako ilishawahi kufanyika, Vatican ilisema Alhamisi. 
Papa huyo ataendesha Misa ya Alhamisi Kuu mchana katika jela ya Casal del Marmo kwa ajili ya vijana katika moja ya viunga vya Roma.
Katika tukio hilo, Papa huosha na kubusu miguu ya watu 12 ili kukumbuka ishara ya huruma ya Yesu kwa wanafunzi wake usiku kabla ya kifo chake.
Mapapa waliotangulia wote kumbukumbu zinaonesha walikuwa wakiendesha sala hiyo ama katika Kanisa la Mtakatifu Petro au Mtakatifu Yohana katika Lateran, ambalo ni Kanisa la Papa katika dhamana yake ya uaskofu mkuu wa Roma.
Wasemaji wa Vatican walisema hawakumbuki tukio kama hilo kufanyika sehemu nyingine zaidi ya hizo mbili.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item