UTAFITI WAONESHA WATANZANIA HAWANA IMANI NA POLISI, WANASIASA...

Askari wa Jeshi la Polisi wakiwa kazini.
Watanzania wamepoteza imani na wanasiasa, polisi na wafanyabiashara, huku wakiwakubali zaidi, viongozi wa dini, walimu, madaktari na wauguzi.


Ripoti ya Maoni ya Watu kwa mwaka 2012 iliyoandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Kuondoa Umasikini (Repoa) na kutangazwa hivi karibuni, imebainisha hayo huku ikiwahusisha wanasiasa hao na ununuzi wa kura wakati wa uchaguzi.
Mbali na wanasiasa, Watanzania pia wameelezea kuamini kuwa watendaji wa Serikali, ndio wanufaika wakubwa wa misaada inayotolewa kwa Tanzania, kuliko wananchi wa kawaida.
Katika ripoti hiyo, Watanzania walipotakiwa kutaja sekta inayoongoza kwa rushwa, walitaja ni askari wa usalama barabarani (trafiki) wakifuatiwa na wenzao, polisi wa kawaida.
Eneo la tatu kwa kuwa na wala rushwa kwa mujibu wa maoni ya Watanzania, ni katika mfumo wa sheria, na hapo Mahakama ikihusishwa na kufuatiwa na huduma za afya zinazotolewa na Serikali.
Mamlaka za kodi, zimetajwa pia kwa kuhusika na rushwa ambapo watendaji wake wameshika nafasi ya tano na kufuatiwa na mamlaka za leseni na vibali.
Nafasi ya saba kwa kula rushwa, kwa mujibu wa maoni hayo, imechukuliwa na watendaji wa Shirika la Umeme (Tanesco) na kufuatiwa na watendaji katika sekta ya elimu na mamlaka za maji.
Kuhusu mahitaji muhimu ya maisha ya mwanadamu, hasa chakula, Watanzania wengi wanaoishi vijijini, ambao kwa mujibu wa ripoti hiyo si asilimia 80 tena, bali asilimia 64, wameelezea mara kwa mara kuishi bila kupata milo mitatu.
Aidha, walipoulizwa kama Serikali inajitahidi katika kukabiliana na rushwa, asilimia 31 ya Watanzania walisema hakuna kitu kinachofanyika huku asilimia 26 wakisema imefanya kitu kidogo na asilimia 20 wakisema inajitahidi kwa kiwango cha juu.
Walipoulizwa tatizo kubwa linalowakabili, Watanzania wengi, zaidi ya nusu ya wahojiwa, walisema ni matatizo ya kifamilia kama ugonjwa, kufiwa na ajali na robo yao ndio walisema gharama za maisha, ajira na kipato.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item