WASIOAMINI MATOKEO KIDATO CHA NNE 'WAKATWA MAINI'...

Mkurugenzi Mkuu wa NECTA, Dk Joyce Ndalichako.
Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), limeeleza kuwa mara nyingi ukataji rufaa na usahihishaji upya wa mitihani hiyo, matokeo yamekuwa hayabadiliki kutokana na umakini wa usahihishaji.
Ofisa Habari wa Necta, John Nchimbi, alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na mwandishi, kuhusu matokeo ya wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka jana, waliokata rufaa kutaka mitihani yao isahihishwe upya.
Kwa mujibu wa Nchimbi, mpaka sasa wanafunzi 530 wamekata rufaa ya kutaka kusahihishiwa upya mitihani yao ya kidato cha nne, na matokeo ya wanafunzi saba tu, ndiyo yaliyobadilika.
Alisema katika wanafunzi hao saba ambao matokeo yao yamebadilika, mmoja matokeo yake amejikuta akipata alama F badala ya D aliyokuwa ameikatia rufaa kwenye somo la Kingereza.
Wanafunzi watano, wamejikuta wakipata alama D kutoka kwenye alama F ya awali, huku mmoja akipata alama C kutoka kwenye alama D ya awali.
Akizungumzia tathmini ya ukataji rufaa na usahihishaji upya wa mitihani hiyo, Nchimbi alisema: "Kwa sasa siwezi kukupa tathmini ya idadi ya walioomba kusahihishiwa upya kama imepanda au la.
"Lakini hata ukiangalia waliosahihishiwa kwa waliojitokeza katika awamu ya kwanza, watahiniwa saba ambao matokeo yao yamebadilika ni wengi, kwani miaka ya nyuma haifiki hata asilimia moja ya watu wanaoomba," alisema.
Hata hivyo, Nchimbi alisema bado Baraza hilo linatoa nafasi kwa wanafunzi wengine kuomba kusahihishiwa upya mitihani yao, na kuwa shughuli hiyo itafungwa rasimu Aprili 18 mwaka huu.
Akitangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika kati ya Oktoba 8 hadi 25 mwaka jana, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alisema ubora wa kufaulu umeporomoka.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, kati ya watahiniwa 456,137 waliofanya mtihani huo, watahiniwa 240,903 walipata daraja sifuri, sawa na asilimia 60 ya watahiniwa wote. Kati yao wanafunzi wa kike walikuwa ni 12,239 na wavulana 120, 664.
Watahiniwa 23,520 walipata kati ya daraja la kwanza hadi la tatu, ambapo 1,641 walipata daraja la kwanza, daraja la pili wanafunzi 6,453 na daraja la tatu watahiniwa 15,426. Wanafunzi 103,327 walipata daraja la nne.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item