CHADEMA 'YATAWALA' MKUTANO WA CCM MOROGORO...
https://roztoday.blogspot.com/2013/04/chadema-mkutano-wa-ccm-morogoro.html
Viongozi wa CCM wakiwasili kwenye mkutano huo mkoani Morogoro jana. |
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, amewataka Watanzania kuachwa kudanganywa na wanasiasa makanjanja wa Chadema, kwa kuwa ni watu wasioitakia mema Tanzania.
Kinana alisema hayo jana wakati akiwahutubia wananchi wa Morogoro katika Uwanja wa Sabasaba, ambapo alisema makanjanja hao hawako tayari kuwahudumia wananchi, badala yake wako kwa maslahi yao na chama chao binafsi.
Aliitaka Chadema kuacha kiburi, matusi na hata udikteta kuhusu mchakato wa Katiba mpya, badala yake wakubali kuheshimu wenzao na kutambua kuwa Katiba ni ya Watanzania wote.
Katika mkutano huo, Kinana aliwashauri Watanzania kutokubali kurubuniwa na kujihadhari na kauli zenye kuchochea vurugu, kwani Chadema kinakowapeleka siko, badala yake wanataka kuteka nyara mchakato huo.
Alisema Chadema ni chama cha ajabu kwani Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alidiriki kusimama bungeni na kusema kuwa mchakato wa Katiba mpya haufai, kwamba muda uliotumika kuhoji watu haukutosha na hata katika uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza umekuwa ni wa hovyo.
Akikosoa kauli hiyo ya Mbowe, Kinana alimtaka akafanye utafiti kabla ya kuzungumza, kwa kuwa Tanzania ndio iliyohoji watu wengi katika mchakato wa Katiba kuliko Kenya na nchi nyingi duniani. Alisema tatizo la Mbowe ni kusoma alichoandikiwa.
Pia, alihoji wapi Mbowe anapata ujasiri wa kusema wajumbe wa Tume ya Kukusanya Maoni ya Katiba Mpya, hawana weledi. Akawataja Jaji Joseph Warioba na Dk Salim Ahmed Salim na kuhoji kama Mbowe anaweza kujilinganisha nao.
"Ndani ya hotuba yake Kiongozi wa Kambi ya Upinzai bungeni, alisema kuwa waliopewa dhamana ya kukusanya maoni ya Katiba mpya hawana ujuzi, suala hili si kweli, waliopewa dhamana hiyo ni watu makini, ambao wanaifanya kazi hiyo kwa uadilifu. Simzingizii hata akileta hotuba yake sasa hivi.
“Chadema lazima ikubali kuwa wameachiwa muda mrefu sana wa kujenga kiburi na kudekezwa… wakubali kuwa kuna watu zaidi yao na hata kabla yao pia kulikuwa na watu. Katiba ya Tanzania sio ya CCM, CUF, TLP, Chadema wala NCCR-Mageuzi, ni ya Watanzania wote,” alisema Kinana.
Alisema Chadema kimezoea kusikilizwa na matokeo yake wanataka kila hatua inayotekelezwa na Serikali, iwafurahishe wao.
“Wamewafanya watu wengine wajinga, kwamba hawana maana zaidi yao tu ambao lengo lao ni kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.
“Chama hicho hakina mkakati wala sera, ndio maana operesheni waliyoianza ya sangara, hadi leo haijulikani ilipofia…na sasa wamekuja na M4C ambayo nayo imebaki katika kofia,” alisema Kinana na kuongeza, Chadema haifai hata kidogo na Watanzania wakatae na wakisusa mchakato wa Katiba, wao waendelee.
Alisema licha ya Serikali ya CCM kufanya mambo mazuri na mengi kwa wananchi, lakini Chadema wamekuwa wakienda kinyume kwa kutokubaliana na hilo.
"Chadema ni watu hatari, ambao wanatakiwa kuangaliwa kwa kuwa wana malengo mabaya ya kuwapoteza Watanzania, msiwaamini ni walaghai na
madikteta wakubwa," alisema Kinana.
Kinana alisema Chadema wamekuwa wakitaka kuvuruga amani ya nchi ambapo hata mara nyingi wanapofanya maandamano, huambatana na vurugu ambazo wao ndiyo wahusika hasa.
Pamoja na kuichambua Chadema, Kinana aliamua kutoa ushauri kwa chama hicho wa kutafuta ufumbuzi wa matatizo yao, kuliko kutumia muda wao mwingi kunyoosha vidole kwa CCM katika kila jambo ambalo linakwenda kombo.
Wakati huo huo, CCM kimewataka baadhi ya viongozi wa chama hicho, kuacha tabia ya kutishia kujitoa ndani ya chama hicho, mara baada ya kukosa nafasi za uongozi katika chama hicho.
Akizungumza na wajumbe wa mashina na viongozi wa matawi ya kata jana, kabla ya mkutano wa kuhitimisha ziara yake mkoani Morogoro, Kinana alisema milango ipo wazi kwa wanachama wanaotishia kujitoa, kwani ni dhahiri wanautaka uongozi kwa maskahi yao binafsi.
“Mtu anakosa uongozi, anasema kama ni hivyo mimi nahama CCM naenda upinzani, ruksa nenda chama chochote kabla ya uchaguzi, kuliko kutaka yale ambayo wananchi hawayataki,” alisema Kinana.
Alisema viongozi wa aina hiyo wana uchu na madaraka na hawana nia njema na hivyo CCM haina budi kupitisha majina ya viongozi wanaotakiwa na wananchi.
“Naomba niseme kwamba hata wakati wa kupitisha majina ya wagombea, ni vyema kupitisha majina ya watu wanaohitajiwa na wananchi, kuliko kupitisha
majina tunayoyataka sisi,” aliongeza.
Kinana alisema baadhi ya migogoro ndani ya chama hicho inasababishwa na baadhi ya wanachama, ambao wana ubinafsi na uroho wa madaraka.
“Kuna baadhi ya wanachama wamekuwa wakisababisha migogoro ndani ya chama na yote hiyo ni ili kuandaa mazingira ya wao kutaka kuwa viongozi wakati wanaharibu.
“Kila mwanachama anatakiwa kutambua wajibu wake na kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa chama chetu,” alisema Kinana.