HIKI NDICHO KIINI CHA ANGUKO LA ELIMU TANZANIA...
https://roztoday.blogspot.com/2013/04/hiki-ndicho-kiini-cha-anguko-la-elimu.html
Wanafunzi wakiwa darasani katika moja ya Shule za Msingi hapa nchini. |
Mdahalo wa Kitaifa wa Kushuka kwa Elimu nchini uliofanyika jana, umebainisha kiini cha kuporomoka kwa kiwango cha elimu na kuwabebesha lawama walimu, viongozi wa Serikali, wananchi na wazazi.
Akichokoza mada kwenye mdahalo huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Kitila Mkumbo, alisema upo utafiti unaonesha kuwa shule zinazofundishwa walimu wenye sifa, ndizo ambazo hazifanyi vizuri.
Kwa mujibu wa Dk Mkumbo, shule hizo zenye walimu wenye shahada, zilifanya vibaya kuliko zile zinazofundishwa na walimu wenye stashahada na wenye leseni za kufundisha.
Akifafanua matokeo ya utafiti huo, Dk Mkumbo alisema walimu hao wasomi wa shahada, walibainika ndio walimu wanaofanya kazi bila wito, wako tayari kuacha kazi hiyo wakati wowote, na walisomea ualimu ingawa sio fani wanayoipenda.
Katika utafiti huo, walimu hao waliuliza maswali mawili ya kwanini wamechangua kusomea fani ya uwalimu, na kama wanao mpango wa kukaa katika fani hiyo kwa muda gani.
Dk Mkumbo alisema walimu wale wenye elimu ya stashahada, walieleza kuwa na uhakika wa kuendelea kufundisha kuliko wale wenye shahada.
“Shule ya Mukoba (mwenyekiti wa CWT-Gratian, Shule ya Sekondari Benjamini Mkapa ya Dar es Salaam) ni miongoni mwa shule zenye walimu wengi wenye sifa, lakini ina wanafunzi wengi waliopata daraja 0, lakini shule kama Marian ina walimu wenye stashahada wanafanya vizuri.
“Ningekuwa ni Waziri wa Elimu, ningeajiri walimu wenye diploma (stashahada) na kuachana na wenye shahada maana hawa hawatulii na wengi wao walipohojiwa, walisema kama ukimaliza kutohoji ikatokea kazi ‘mbadala’ naondoka sasa hivyi,” alisema Dk Mkumbo.
Dk Mkumbo alisema pia udogo wa mishahara kwenye shule za umma, unachangia walimu wengi kutotulia shuleni kuliko wale wanaofundisha katika shule za watu binafsi na mashirika ya dini.
Hata hivyo alibainisha kwamba, Tanzania inalipa vizuri walimu sawa na wastani wa Dola za Marekani 6,000 kwa mwaka, kuliko nchi zingine Afrika ambazo wastani wa mshahara wa mwalimu kwa mwaka ni Dola 4,000.
“Katika wagonjwa wa elimu wa Afrika (katika mshahara), sisi tunakaribia kutoka wodini,” alisema Dk Mkumbo lakini akahadharisha kwamba, suala hilo haliondoi ukweli kuwa mishahara ya walimu, ikilinganishwa na kazi zingine ni midogo.
“Mtu mmmoja nilimuuliza kwa nini walimu wanalipwa mshahara kidogo, akasema eti wako wengi, sasa si muwapunguze!” Alihoji na kusababisha kicheko.
Akisisitiza katika mshahara, alitoa ulinganisho kwamba mwalimu mwenye shahada, akitoka chuoni hulipwa Sh 532,000 lakini anayesomea mifugo kuwa ofisa mifugo, hulipwa Sh 1,200,000.
Alisema pia mwalimu akimaliza mafunzo ya cheti, akienda kazini hulipwa Sh 277,000, wakati ofisa kilimo mwenye cheti huondoka mpaka na Sh 890,000.
Dk Mkumbo alisema kuna haja ya kuweka suala la elimu kuwa kipaumbele cha taifa na kuwekeza katika elimu, huku akinukuu viongozi mbalimbali akiwamo hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uongereza, Tony Blair.
Alisema Mwalimu Nyerere alitambua umuhimu wa elimu na aliwahi kuweka wazi kwamba kuna haja ya kuweka elimu kipaumbele, kwa kuwa miaka inayokuja, mataifa makubwa yatatumia elimu kukandamiza mataifa machanga.
Akilinganisha tofauti ya vipaumbele vya viongozi na kuporomoka kwa elimu, Dk Mkumbo alisema wakati Blair alipoulizwa kuhusu vipaumbele vyake, alisema kipaumbele cha kwanza ni elimu, kipaumbele cha pili ni elimu na kipaumbele cha tatu ni elimu, Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Benjamini Mkapa, alisema kipaumbele cha kwanza ni uchumi, cha pili ni uchumi na cha tatu ni uchumi.
Kuhusu kutokuwajibika kwa wananchi, Profesa Adolf Mkenda alisema viongozi wengi hawawajibi katika elimu kutokana na wananchi kutopiga kelele kuhusu elimu.
Alitoa mfano wa Blair alipoingia madarakani Uingereza, ambapo alisema wananchi walipiga kelele kuhusu shule ambazo watoto wake walikuwa wakisoma na kuhoji kama Watanzania wanazungumzia wanakosoma watoto wa viongozi.
“Wanaopigia kelele sera na kuzisimamia wakati watoto wao hawasomi kwenye shule hizo, wenzetu Uingereza Tony Blair walimuhoji ni kwanini watoto wake hawasomi shule za umma, je hapa tunahoji?
“Mtu anayesimamia kitu ambacho hakimuusu moja kwa moja je, anaweza kuwa na nafasi ya kukiboresha?” alihoji.
Kilio cha wazazi kutowajibika kwa watoto wao, kilitamkwa na wachangiaji wengi, huko mvutano kuhusu lugha ya Kiingereza au Kiswahili kutumika kufundishia ukiibuka.