MWILI WA MEJA JENERALI MAKAME RASHID WAAGWA RASMI...
https://roztoday.blogspot.com/2013/04/mwili-wa-meja-jenerali-makame-rashid.html
Mamia ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wakiongozwa na Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi jana walijitokeza katika viwanja vya Karimjee kuuaga mwili wa Meja Jenerali mstaafu Makame Rashid, aliyefariki dunia wiki iliyopita katika hospitali ya Lugalo.
Akizungumza katika shughuli ya kuuaga mwili huo iliyoambatana na dua iliyoongozwa na Sheikh Mkuu wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, Rais Mwinyi alisema enzi za uhai wake, Makame alikuwa mtu aliyemheshimu kila mmoja bila kujali nyadhifa na heshima aliyonayo.
Alisema mbali na hilo, pia Makame aliheshimu misingi ya dini kwa kufanya ibada wakati wote, suala alilosema ni vyema likaigwa na kila mmoja kwa ajili ya kujiwekea amana yake mbele za Mungu siku yake itakapofika.
“Marehemu Makame atakumbukwa kwa mambo mengi sana aliyoyafanya akiwa kazini na hata nje yake, alipenda kumsikiliza kila mtu na kumsaidia pale ilipobidi hakika pengo lake litaendelea kutawala,” alisema Mwinyi.
Wengine waliomzungumzia Makame ni pamoja na aliyewahi kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Omari Mahita, Katibu mstaafu wa OAU, Dk Salim Ahmed Salim, na Profesa Philemon Sarungi aliyewahi kuwa Waziri wa Ulinzi.
Walimsifu kuwa ni mtu aliyekuwa na msimamo na mwenye kutambua wajibu wake wa kazi sehemu mbalimbali alizopitia.
Akitoa mawaidha katika dua hiyo, Sheikh Mkuu wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum aliwataka Watanzania kukumbuka kufanya ibada wakati huu wakiwa hai ili kuepuka adhabu za kaburi siku ya kiama.
Alisema sifa zote zilizotolewa kwa marehemu Makame ikiwemo ya ucha Mungu, ni ishara tosha kuwa kiongozi huyo alitimiza wajibu wake ipasavyo hapa duniani huku akisisitiza kuwa ni vyema kila muumini kujitathimini mwenyewe katika matendo yake.
Akisoma risala kwa niaba ya familia, mmoja wa wanafamilia hao Hamza Rashid, alisema Jenerali Makame alizaliwa Oktoba 23 Mwaka 1924 na kwamba kabla ya kifo chake amepitia nyadhifa mbalimbali za uongozi hapa nchini.
Alisema alijiunga na JKT mwaka 1963 na hatimaye kuwa Mkuu wa JKT wa tano tangu Januari 1989, hadi Oktoba 2001 alipostaafu akiwa amelitumikia Jeshi kwa miaka 37 na siku 22.
Alisema Makame aliyefariki dunia juzi saa 12:30 asubuhi, katika Hospitali ya TMJ Dar
es Salaam anatarajiwa kuzikwa leo katika kijiji cha Mnyawa, Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara huku akiacha mjane, watoto tisa na wajukuu wanane.