SERIKALI YAUFYATA KWA WALIMU, YAREJEA MEZANI KWA MAZUNGUMZO...
https://roztoday.blogspot.com/2013/04/serikali-yaufyata-kwa-walimu-yarejea.html
Gratian Mukoba. |
Serikali imerejea katika meza ya mazungumzo na Chama cha Walimu Tanzania (CWT), pamoja na kutokuwepo kwa mazingira ya nia njema kutoka upande wa wawakilishi wa walimu katika mazungumzo hayo.
Taarifa ya Ikulu iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana, ilieleza kwamba Serikali imefikia hatua hiyo ili kuonesha utayari na nia njema katika mazungumzo hayo.
Mbali na utayari, pia Serikali imetangaza kwamba kutakuwepo na nyongeza nzuri kwenye mishahara, hasa ya watumishi wa ngazi za chini katika mwaka ujao wa fedha.
Kabla ya hatua hiyo, vyombo vya habari vilimkariri Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba akisema kwamba Serikali imekataa kukaa meza moja na CWT ili kuzungumzia nyongeza ya mishahara na posho za walimu, pamoja na kwamba chama hicho chenyewe kiko tayari kwa mazungumzo.
Mukoba pia alikaririwa akidai kwamba Serikali imepuuza amri ya Mahakama, inayotaka pande hizo mbili kukaa meza moja kujadili madai ya walimu.
Kutokana na madai hayo, Mukoba alilitaka Bunge na wazazi, kuingilia kati uamuzi wa Serikali kukataa kukaa meza moja na CWT.
“Serikali inapenda kuwafahamisha wananchi kuwa, madai haya yote hayana chembe ya ukweli na hayana nia njema, maana yanaweza kujenga chuki na mazingira ya kuzua mgogoro mwingine na Serikali usio na sababu, wala maslahi kwa walimu wenyewe na Taifa,” imeeleza taarifa hiyo ya Ikulu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Serikali imeeleza kuwa haijakataa majadiliano na CWT, na wala haijapuuza amri ya Mahakama, inayotaka pande zote mbili kurudi kwenye meza ya majadiliano.
Tofauti na madai ya Mukoba, taarifa ya Serikali ilieleza kuwa tangu amri ya Mahakama itolewe, tayari vimefanyika vikao vinne vya Baraza la Majadiliano ya Pamoja katika utumishi wa walimu.
“Vikao viwili vilifanyika mwaka jana Septemba 12 na Desemba 5. Vikao viwili tayari vimefanyika mwaka huu Januari 9-10 na Machi 22,” ilieleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilifafanua kwamba kilichochelewesha suala la mishahara na posho kujadiliwa katika vikao hivyo, si kwamba Serikali haikutaka mjadala huo.
“Sababu hasa ni kuwa CWT ilikata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu katika kesi Na. 96/2012, na Serikali iliwasihi viongozi wa CWT wafute rufaa hiyo, ili kuruhusu majadiliano ya mishahara na posho, lakini walikataa.
“Kitendo hicho hakioneshi nia njema upande wao. Nia njema ni sharti muhimu kwenye majadiliano haya. Kwa upande wake, ili kuonesha utayari na nia njema, Serikali sasa imekubali majadiliano hayo yaendelee, licha ya CWT kukataa kufuta rufaa yao,” ilieleza taarifa hiyo.
Serikali imeelezea sababu ya pili iliyochelewesha majadiliano ya maslahi ya walimu, kuwa ni madai ambayo awali viongozi wa CWT walikuja nayo, kuwa iteuliwe timu maalumu ya kuzungumzia maslahi, badala ya Baraza la Majadiliano ya Pamoja katika utumishi wa walimu, ambalo ndilo lipo kisheria kwa majadiliano hayo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, CWT ilichelewa kurejesha majadiliano kwenye Baraza hilo, mpaka wakati wa kikao cha Januari 9 hadi 10, mwaka huu.
Wakati Mukoba alikaririwa kwamba kikao kilichokataa kuzungumzia mishahara na posho za walimu ni kilichofanyika Aprili 2 mwaka huu, chini ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, Serikali imepinga madai hayo.
“Si kweli vilevile kuwa kikao kilichofanyika Ikulu, Aprili 2, mwaka huu chini ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Sefue, ndicho kilikataa majadiliano kuhusu maslahi ya walimu.
“Kauli hiyo ni upotoshaji wa makusudi usio na nia njema. Viongozi wa CWT wanajua vema kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, si sehemu ya mfumo wa majadiliano kuhusu maslahi ya walimu. Hivyo, kikao kinachoongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi, hakiwezi kuwa mahali pa majadiliano ya mishahara, posho na maslahi ya walimu,” ilieleza taarifa hiyo.
Ilifafanuliwa kwamba mkutano huo wa Aprili 2, uliitishwa na Katibu Mkuu Kiongozi kwa maombi rasmi ya uongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), ambao walitaka kujulishwa jinsi utaratibu wa majadiliano ya mishahara ya wafanyakazi wote utakavyokuwa, kutokana na kuanzishwa kwa mzunguko mpya wa Bajeti ya Serikali.
Serikali imeeleza kuwa kikao hicho kisingeweza kugeuka na kuwa kikao cha kujadili mishahara na posho za walimu, kama alivyokaririwa Mukoba akidai.
“Tunapenda wananchi na walimu wajue pia kuwa Gratian Mukoba, hakuwepo kwenye hicho kikao cha Aprili 2, 2013. Aidha, kikao hicho kilikuwa cha Tucta, hakikuwa cha CWT,” ilieleza taarifa hiyo.
Serikali imeelezea kupata tabu ya kuelewa nia na dhamira ya viongozi wa CWT, kwa kupotosha kwa makusudi wananchi na walimu kwa mambo yaliyo wazi.
“Serikali imeonesha nia na dhamira ya wazi ya kujadiliana na CWT, pamoja na vyama vyote vya wafanyakazi, kuhusu maslahi ya wafanyakazi. Vikao vingi vilivyofanyika na vinavyoendelea kufanyika kwenye mabaraza ya kisekta na Baraza Kuu, ni ishara ya wazi ya nia njema ya Serikali.
“Tunajiuliza, katika hali hiyo, juhudi hizi za viongozi wa CWT kuandaa mazingira ya mgogoro wa Serikali lengo lake ni nini hasa?” ilihoji taarifa hiyo.