TIKETI MPYA KWA NAULI MPYA, TIKETI ZA ZAMANI NAULI YA ZAMANI...
https://roztoday.blogspot.com/2013/04/tiketi-mpya-kwa-nauli-mpya-tiketi-za.html
Baadhi ya daladala zinazofanya safari zake katika jiji la Dar es Salaam. |
Abiria wa mabasi ya daladala jijini Dar es Salaam wameelekezwa kutokubali kulipa nauli mpya iwapo tiketi wanazopewa zitakuwa zimeandikwa nauli ya zamani.
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) imewataka abiria kutoa taarifa kwake juu ya magari yanayotoza nauli tofauti na iliyoandikwa kwenye tiketi ili wahusika wachukuliwe hatua.
Ofisa Mfawidhi wa Sumatra, Kanda ya Mashariki , Conrad Shio alisema mabadiliko ya nauli mpya yaliyoanza wiki iliyopita, yalitakiwa yaende pamoja na kubadili kiwango cha nauli kwenye tiketi na maandishi ya ubavuni mwa daladala.
Kwa mujibu wa ofisa huyo, tangu Jumamosi iliyopita hadi juzi, daladala 16 zimekamatwa kwa kutoza nauli iliyo tofauti na tiketi. Kabla ya kuanza kutumika kwa nauli mpya, Sumatra iliwataka wenye daladala kubadili tiketi ziendane na mabadiliko.
“Tumewasisitiza sana wenye daladala kuwa wahakikishe mabadiliko ya nauli yanakwenda pamoja na tiketi na kwamba wasioweza kufanya hivyo waendelee kutoza nauli za zamani na wananchi wasisite kutoa taarifa,” alisema Shio.
Wakati huo huo amezungumzia upungufu wa idadi ya daladala unaodaiwa kukabili maeneo mengi jijini, na kusema katika sheria ya Sumatra hakuna sehemu inayozuia wenye magari hayo kubadili njia kwa kuwa ni suala la kibiashara.
Alisema Sumatra haijafuta usajili kwa baadhi ya daladala na kwamba usajili unaendelea. Alifafanua kwamba wanaokimbia baadhi ya njia inatokana na msongamano uliochangiwa na matengenezo ya barabara.