WAZIRI ATOA SIKU 30 JENGO LA GHOROFA 16 LIBOMOLEWE DAR...

KUSHOTO: Muonekano wa jengo hilo kutokea upande lilipoporomoka jengo lingine la ghorofa 16. KULIA: Jengo hilo kwa karibu.
Wakati Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, Profesa Anne Tibaijuka akitoa siku 30 ili kuvunja jengo la ghorofa 16 pembeni mwa lilipokuwa ghorofa lililoporomoka hivi karibuni na kuua watu 36 katikati ya Jiji la Dar es Salaam, Kamati ya Bunge inataka ubomoaji huo ufanyike ndani ya siku tano.

Mvutano huo uliibuka jana baada ya Waziri Tibaijuka na wajumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira inayoongozwa na James Lembeli, kutembelea eneo la maafa kwenye makutano ya mitaa ya Indira Gandhi na Morogoro. Waziri anayeshughulikia Mazingira, Dk Terezya Huvisa pia alikuwa miongoni mwao.
Wakati Tibaijuka akitoa siku 30 kwa mmiliki wa jengo hilo, M/S Ladha Construction Limited, wabunge walitaka libomolewe punde ili kuepusha kuporomoka na kusababisha maafa mengine kwa kuwa tayari linaonesha dalili za   hatari hiyo.
Akizungumza kwa hisia kali, Waziri Tibaijuka alisema: "Nimeagiza mmiliki wa ghorofa hizi 16 zinazoendelea kujengwa hapa abomoe jengo lake ndani ya siku 30 kwa sababu tumegundua limejengwa chini ya kiwango na limekiuka sheria ya mipango miji inayoruhusu ujenzi wa ghorofa saba hadi 10 tu kwa majengo ya katikati ya Jiji.
"Mmiliki wa jengo alifanya ujanja ujanja kujipatia vibali wakati ujenzi wake ukiwa ukingoni. Huu ni mchezo mchafu ninaotaka ukome kuanzia sasa, kwa kuwa unachezea maisha ya watu wanaokufa bila hatia, kutokana na kuangukiwa na majengo yanayoendelezwa bila kuzingatia sheria na viwango". 
Alilaumu wataalamu walioruhusu ujenzi huo na wa lililoporomoka, kwa kuwa wao ndio wanaotazamiwa kuhakikisha ujenzi wowote unaoendelea nchini ni wa viwango vinavyotakiwa.
"Na kwa sababu haya yametokea, nimejifunza jambo na sasa ninaamuru Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ihesabu majengo yote ya mjini yaliyo na ghorofa zaidi ya 10 ili yakaguliwe na kufanyiwa tathmini kama yanastahili kuendelea kuwepo au la. Yanayostahili kuwepo yatarasimishwa na wamiliki kupewa vibali lakini yenye kasoro yataondolewa mara moja.
"Endapo mmiliki huyu atashindwa kukamilisha ubomoaji wake ndani ya muda niliompa, atalazimika kulipa faini ya asilimia mbili ya gharama za uendelezaji haramu alioufanya kwa kila siku atakayoongeza katika ubomoaji huo. Kwa ndugu yetu huyu itakuwa ni gharama za ujenzi wa ghorofa sita alizozidisha," alisema.
Wakati akisema hayo, Lembeli alisema: "Siku 30 ni nyingi kwa jengo lenye hali mbaya kama hili la Ladha, hivyo, Serikali haina budi kumwamuru 'alishushe'ndani ya siku tano kuepusha kudondokea watu kama ilivyotokea kwa jengo lingine la mtu huyo.
"Kila mtu amejionea hali halisi kwamba limeanza kubomoka na msingi wake unatitia sasa kusubiri ubomoaji kwa siku hizo 30 ni kukaribisha hatari nyingine. Tunaomba hilo lizingatiwe na mhusika abomoe haraka kwa kuwa taarifa anayo na mamlaka husika zimeshapewa maelekezo, kuhakikisha analibomoa, hakuna linaloshindikana ikiamriwa hivyo."
Hata hivyo, Tibaijuka alijibu kuwa ubomoaji lazima uzingatie taratibu zote ikiwa ni pamoja na kuhakikisha unafanyika kwa hadhari kuzuia uporomokaji wa vifaa na jengo lenyewe, hivyo kipindi hicho kinajumuisha muda wa kutathmini namna ya kuendesha  ubomoaji usio na madhara kwa majengo mengine na watu.
Waziri alisema: "Ninasema hivyo huku nikitambua umuhimu wa kuondoa mara moja majengo yenye kuonesha ishara za kuleta hatari, lakini utaratibu lazima uzingatiwe pia ili kuepusha hatari isitokee kwa kufanya ubomoaji wa haraka haraka. Najua, huduma nyingi za jamii zimesimama katika eneo hili na tunataka ziendelee, ila hatufanyi hivyo bila kuzingatia madhara ya haraka zetu". 
Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemiah Mchechu alisema hawatakubali tena kumwachia mbia asimamie jengo kwa asilimia 100 kama sheria inavyotaka kwa kuwa wamebaini kuwapo hatari kubwa ya kuendelea kuwa na majengo yasiyo na viwango nchini.
"Tumekubaliana na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) tufanye ukaguzi katika majengo yote tuliyokuwa hatuyasimamii ili kujiridhisha juu ya ujenzi wake, kwa mfano jengo hili lililoanguka linaonesha wazi lilikuwa limejengwa chini ya kiwango na lilizidishwa sana mchanga na mbia alilisimamia mwenyewe".

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item