MREMA ASEMA WANASIASA NDIO CHANZO CHA VURUGU...

https://roztoday.blogspot.com/2013/06/mrema-asema-wanasiasa-ndio-chanzo-cha.html
![]() |
Augustine Mrema. |
Wanasiasa wanaotafuta umaarufu kwa nguvu, wametajwa kuwa ndio chanzo cha vurugu mbalimbali nchini hivyo, wametakiwa kujifunza kutoka kwa wanasiasa wakongwe ambao licha ya kuwa na wafuasi wengi miaka ya nyuma, hawakuwahi kumwaga damu.
Aidha, wametakiwa kuacha kujinadi kwa kutumia makundi ya dini kwani ndiyo wachochezi wa kusababisha vurugu za kidini.
Hayo yamesemwa jana na mwanasiasa mkongwe aliyepata kushika nyadhifa kadhaa ikiwa pamoja na kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Naibu Waziri Mkuu, Augustine Lyatonga Mrema ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Jimbo la Vunjo na Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP).
Mrema aliyasema hayo alipokuwa akizindua chama cha ‘Undugu’ baina ya Wakristo na Waislamu cha Muslim and Christian Brotherhood Society (MCBS) ambacho alisema kimeanzishwa wakati mwafaka wakati Taifa linakabiliwa na matatizo mbalimbali ya vurugu za kidini na mengineyo.
Alisema kumekuwa na tabia ya wanasiasa kuilinganisha Tanzania na Libya au Misri vitu ambavyo ni tofauti, huku akitoa rai kuacha kuhusisha masuala yanayotokea nchini na ugaidi kwani kuna nchi za Magharibi zinasaka magaidi hivyo wasiingie nchini kuwasaka na kusababisha vita isiyo ya ulazima.
“Jambo la msingi ni wanasiasa wa sasa kujiangalia na kuacha kufanya siasa za chuki kwa kujifunza kwa wanasiasa wakongwe huku viongozi wa dini kutokukubali kutumika na wanasiasa. Hii itasaidia kuleta amani tuliyoizoea,” alisema Mrema.
Alisema kamwe Serikali isifumbie macho wanasiasa wachache wanaotaka kurubuni Watanzania kwa kuchukua hatua stahili kama iliyokuwa ikifanyika miaka ya nyuma kwa kutowaacha wanaotaka kuharibu amani ya nchi.
“Ni lazima kuwa na maamuzi hata kama jambo lenyewe ni zuri lakini watu wanatumia kuharibu amani kama ilivyofanya katika kuzuia mihadhara ambayo watu waliitumia kutukanana, lakini pia lazima wananchi kujenga tabia ya kuvumiliana katika changamoto mbalimbali,“ alisema.
Awali Mwenyekiti wa chama hicho kipya, Hamad Tao alisema nia ya chama hicho kilichoundwa na watu kutoka dini zote vyama vya siasa na wananchi wa kawaida ni kuzuia na kuepusha migogoro ya kidini na kuelimisha wananchi madhara yatokanayo na ugaidi.
Pia kuelimisha wananchi madhara yatokanayo na dawa za kulevya pamoja na umuhimu wa kuheshimu utawala wa sheria na madhara yatokanayo na imani za kishirikina.
“Lakini chama chetu bado kichanga hivyo tunahitaji msaada wa wanajamii wote wa kifedha na mawazo ili kuweza kufikia malengo na kuwaepuka maadui wanaotaka kuondoa amani yetu kwa kutumia masuala ya dini na mengineyo,” alisema.