MWIGULU NCHEMA ASEMA CCM HAIEPUKI LAWAMA MLIPUKO WA BOMU ARUSHA...

https://roztoday.blogspot.com/2013/06/mwigulu-nchema-asema-ccm-haiepuki.html
![]() |
Mwigulu Nchemba. |
Chama Cha Mapinduzi (CCM), hakina namna ya kujivua lawama katika tukio la bomu la kurushwa kwa mkono, kutupwa katikati ya wafuasi wa Chadema, Arusha na kusababisha mauaji.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Mwigulu Nchemba, alisema hayo juzi jioni na kuongeza kuwa, Chadema imekuwa ikitumia mwanya huo kuhujumu chama hicho tawala.
“Jambo likitokea kama hili, CCM hata isiposhiriki, haina kinga,” alisema Mwigulu ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi wakati akichangia Bajeti ya Serikali na kuhadharisha kwamba Chadema inatumia mwanya huo kuhujumu.
Alinukuu ripoti ya Jukwaa la Wahariri, kuhusu utekaji wa Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Absalom Kibanda, ikieleza kwamba baadhi ya makada wa Chadema, walipata mafunzo nje ya nchi ya utesaji kwa lengo la kuikosanisha Serikali na CCM kwa wananchi.
“Kama waliweza kumvisha raia sare za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), watashindwaje kumvisha mtuhumiwa wa bomu la Arusha sare za Polisi?” Alihoji Mwigulu.
Alihoji pia picha iliyo katika mtandao ikimwonesha anayedaiwa kuwa mtuhumiwa wa mauaji hayo ya Arusha na kutaka kujua aliyepiga alikuwa na ujasiri gani wakati bomu limetupwa?
“Hata yule aliyechukua mkanda hakushitushwa na lile bomu, aliendelea kuchukua ile picha kama vile yuko katika sherehe ya Send Off (kuaga mwali),” alisema Mwigulu.
Kwa mujibu wa Mwigulu, hata picha ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), akiwa na fuko la fedha wakati watu wanakufa na wamemwaga damu, linaonesha kuwa limepangwa.
Alikuwa anazungumzia tukio la mwishoni mwa wiki Arusha ambako bomu lililolipuliwa katika mkutano wa kufunga kampeni za udiwani wa kata nne za Arusha ulivuruga mkutano huo na kusababisha vifo na majeruhi kadhaa.
Aidha, kutokana na mlipuko huo, uchaguzi wa kata za Kimandolu, Elerai, Kaloleni na Themi katika Jiji la Arusha uliahirishwa hadi mwishoni mwa wiki ijayo, ambapo kama inavyotarajiwa, mchuano mkali unatarajiwa kuwapo baina ya CCM na Chadema.
Mlipuko katika mkutano huo wa Chadema ambao viongozi wake wameelekeza lawama kwa Polisi, umekuja mwezi mmoja baada ya kutokea mlipuko katika Kanisa Katoliki la Joseph Mfanyakazi la Olasiti nje kidogo ya Mji wa Arusha, ambako takribani watu watatu walikufa na wengine kadhaa kujeruhiwa huku Balozi wa Vatican nchini na watawa waliokuwa katika shughuli maalumu ya kuzindua Parokia mpya ya Mtakatifu Yosefu wakinusurika.
Katika taarifa yake juzi kwa vyombo vya habari, Chama cha Democratic (DP) kilitilia shaka madai kuwa bomu lililolipuliwa Arusha lilimlenga Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Alisema ingekuwa lengo ni kummaliza Mwenyekiti huyo, lingeelekezwa jukwaani na tena isingesubiriwa amalize kuhutubia na kuondoka hata hatua moja.
Taarifa hiyo iliyosainiwa na Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila, ilisema “bomu hilo lilielekezwa kwa walalahoi walioteketezwa kwa ajili ya kufanikisha malengo ya kisiasa.”
Alielekeza lawama kwa Chadema wenyewe akisema ndio wahusika wa shambulio hilo, baada ya kubaini kuwa uchaguzi ambao ungefanyika Jumapili usingekuwa na matokeo mazuri kwao.
“Hauwezi kukwepeka ukweli unaoonwa na wananchi wengi, kwamba uchaguzi uliokuwa ufanyike Jumapili tarehe 6 Juni, ulikuwa mgumu sana kwa Chadema na viongozi wake waliihofia sana hali hii,” ilisema taarifa.
Ilibaini kwamba wale madiwani waliofukuzwa na kusababisha uchaguzi mdogo walikuwa na ushawishi katika kata hizo, kwa vile wapiga kura ndio waliowapa nafasi hizo na kuhujumiwa baadaye.
“Homa ya Chadema ya uchaguzi Arusha ilipanda zaidi kutokana na udhaifu wa viongozi wake wa kupenda sana mapambo ya sifa, tena wasizokuwa nazo katika kujipa mvuto bandia kwa wananchi, hata kwa kuteka sera na itikadi na kaulimbiu za DP na wengine … Mbowe aliweka wazi kwamba ni lazima washinde kwa gharama yoyote,” ilisema taarifa.
Ilisema kilichofanyika Soweto ni mbinu chafu ya kisiasa ya kujipatia ushindi kwa kura za huruma kwa gharama za uhai wa wanaouawa na kujeruhiwa na kupata ulemavu. Hata hivyo uchaguzi huo uliahirishwa hadi Juni 30.