SERIKALI YACHARUKIA WASIOTII SHERIA BILA SHURUTI...

Mizengo Pinda.
Serikali imechoka na vurugu ambapo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ametangaza rasmi kwamba inafahamu zinasababishwa na wanasiasa na wafuasi wao na kuonya kwamba wakikaidi amri ya kuacha fujo nguvu za ziada zitaendelea kutumika.
Pinda pia hakusita kukumbusha Watanzania, kwamba Chadema iliposhindwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, ilitangazia umma kwamba; “nchi haitatawalika” na kufafanua, kwamba huenda vurugu zilizopo, ni mwendelezo wa ahadi hiyo ya Chadema kwa Watanzania.
Pinda alitoa kauli hiyo ya Serikali jana, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM), katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu.
“Ona sasa Mangungu anasema vyombo vya Dola vinapiga watu, hawa wanafanya fujo, wanaambiwa acha, wanakaidi, utapigwa tu…watakupiga tu na mimi nasema muwapige tu maana tumechoka,” alisema Pinda.
Katika swali lake, Mangungu alisema Afrika nzima, nyimbo za Taifa, zinasema hekima, umoja na amani ni ngao yetu na kumtaka Pinda atoe kauli ya Serikali kuhusu hali ya vurugu inayotokea nchini, hasa  Arusha.
Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji (CUF), alihoji kwa nini Pinda aruhusu raia wapigwe wanapokaidi amri halali, wakati Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inakataza Serikali kumpiga raia na kumdhalilisha.
Akijibu hoja hizo, Pinda alifafanua, kwamba kuna tofauti ya mtuhumiwa aliyefikishwa katika vyombo vya sheria, ambaye Katiba inakataza kufanywa chochote, lakini anayekaidi amri halali lazima ashurutishwe kuitii.
“Lazima uweke tofauti ya aliyekamatwa na aliyefikishwa katika vyombo vya sheria, ambaye Katiba inasema asifanywe chochote, lakini ukiambiwa usiandamane, ukaamua kuandamana na sisi tutakwenda hivyo hivyo mpaka tujifunze kutii sheria bila shuruti,” alionya.
Pinda alitaka Watanzania wasijitokeze kutetea wahalifu hao wakiwamo wanasiasa, badala yake waiache Serikali ifanye kazi yake.
Alisema nchi ikiingia katika vurugu, hakuna mshindi kwa kuwa kila mtu ataathirika hasa wanawake, watoto na wenye ulemavu.
Akizungumzia suluhisho la vurugu hizo, Pinda alisema viongozi wa kisiasa wanawajibika kuweka kando itikadi zao za kisiasa na kukubaliana kuwa na lugha moja.
Alisisitiza, kuwa kama viongozi hao hawatakubaliana, Serikali haina namna isipokuwa kupambana na wahalifu na kuahidi kuwa mapambano hayo yatafanyika kwa nguvu.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema Serikali imeshapata orodha ya viongozi wanaochochea vurugu Mtwara na imeahidi kumkamata mmoja baada ya mwingine na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
Pinda alisema kazi iliyobaki ni kuwakamata watuhumiwa wote na aliwaonya wasilete jeuri wakati wa kukamatwa.
Kabla ya Mangungu, Mbunge wa Viti Maalumu, Clara Diana Mwatuka (CUF), juzi alipopewa nafasi ya kuchangia Hotuba ya Bajeti ya Serikali, alisema anashindwa kuchangia vizuri kwa kuwa ana uchungu watu wa Mtwara wanapigwa.
Mwatuka alisema sasa hivi Mtwara kumejaa magari ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kiasi cha kutishiwa katika uchaguzi mdogo wa madiwani uliofanyika Jumapili.
Pinda alisema alimsikia Mwatuka akilalamika juzi na kuongeza, kuwa alitarajia kujitokeza watu watakaosema vyombo vya Dola vinawaonea.
Kabla ya kauli hiyo ya Pinda, Serikali baada ya vurugu hizo, ililaani na kuapa kusaka waasisi wa vurugu hizo ndani na nje ya Mtwara.
Akitoa kauli ya Serikali bungeni kulaani vurugu hizo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi aliliambia Bunge kuwa waliohusika kupanga, kushawishi, kuandaa na kutekeleza vurugu hizo hawatakwepa mkono wa sheria.
Katika kauli hiyo ya Serikali, Waziri Nchimbi alisisitiza kuwa Watanzania wana Taifa moja ambalo maliasili zake ni za wote na kuonya kuwa tabia iliyoanza kujengeka ya kila eneo kutaka inufaike peke yake na mali za eneo husika, italigawa Taifa vipande.
Alihadharisha kuwa baadhi ya taasisi za kiraia na vyama vya siasa kwa maslahi binafsi yasiyo na upeo mpana, vinaweza kudhani kuwa kuunga mkono madai ya namna hiyo ni kujiimarisha na kukubalika kwao kwa jamii, lakini badala yake wataipasua nchi na kusababisha vifo vya maelfu ya watu na kulijaza Taifa vilema na majeruhi.
"Wasaliti wa Taifa hili wanafahamu maendeleo makubwa yatakayopatikana Mtwara na nchi nzima kutokana na rasilimali gesi, hivyo wanatumia vibaya ufahamu wetu mdogo kuhusu gesi na kuchochea upinzani dhidi ya mradi huu unaotarajiwa kukomboa Watanzania," alisema Waziri.
Alisema vita inayofahamika kama vita kuu ya Afrika katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo iliyopiganwa kati ya 1998-2003, msingi wake ulikuwa ni rasilimali. Vita hiyo ilisababisha vifo vya watu milioni 5.4, magonjwa na njaa na kuhoji kama huko ndiko Tanzania inapelekwa.
Alisisitiza Watanzania wanatakiwa kujua kuwa wana dhamana ya kuendeleza umoja, amani na kuchangia maendeleo ya nchi na tofauti zinazojitokeza lazima ziendelee kuzungumzwa kwa uwazi, kuheshimiana na kuzingatia sheria na utaratibu wa nchi.
Mbunge wa Mtwara Mjini, Hasnein Murji (CCM) anakabiliwa na kesi ya uchochezi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini humo.
Inadaiwa kuwa Januari 19 Murji akiwa maeneo ya Ligula mkoani Mtwara, alichochea watu kutenda  kosa la kufanya vurugu kupinga ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam. 
Katika hatua nyingine mkulima mkazi wa Kijiji cha Lumbila, Kata ya Ruanda, Mbozi mkoani Mbeya, Rajabu Mwashitete (25) ameuawa na polisi kwa kupigwa risasi.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 7 mchana katika kijiji hicho, baada ya polisi waliokuwa wakiendesha msako dhidi ya wahalifu ambao ni waporaji katika Mlima Senjele kuzingirwa na watu zaidi ya 150 wakiwa na silaha za jadi na kutaka kuwashambulia na hivyo kuzua vurugu.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani, watu hao walikuwa na mapanga, marungu, mashoka na mawe na walikuwa wakizuia polisi kukamata wahalifu licha ya kuwa walishakamata mali inayodhaniwa kuwa ya wizi ambayo ni madumu zaidi ya 100 ya dizeli.
“Katika vurugu hizo walichukua madumu matatu yenye ujazo wa lita 60 kila moja, mawili yenye ujazo wa lita 20 na manane ya lita 30, hivyo kufanya askari washindwe kuchukua vielelezo vyote,” alisema Kamanda. Aliongeza kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi.
Katika tukio hilo, mkulima mwingine wa Lumbila, Charles Mwawalo (27) alijeruhiwa kwa kupata michubuko tumboni na uchunguzi unafanywa kubaini ni kitu gani kilichomjeruhi.
Kwa mujibu wa Kamanda, wananchi walifunga barabara kuu ya Mbeya-Tunduma kwa mawe na magogo na kusababisha msongamano wa magari barabarani.
Hali ilirejea kuwa tulivu baada ya Kamanda Athumani kufika eneo la tukio na kuzungumza na wananchi na viongozi wa eneo hilo, kisha kufungua barabara.
Askari wanne walijeruhiwa katika tukio hilo, kati yao watatu walitibiwa na kuruhusiwa na askari mmoja  kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kwa matibabu zaidi.
Kamanda Athumani alitoa mwito kwa jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi, kwani ni kinyume cha sheria badala yake wawe na utamaduni wa kutatua kero na malalamiko yao kwa njia ya mazungumzo kwa kuyawasilisha katika mamlaka husika.
Aidha, aliwaambia waliowahi kuibiwa au kuporwa mali yakiwamo mafuta, wajitokeze Polisi kwa ajili ya hatua zinazostahili.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item