WABUNGE WAANZA KUICHAMBUA SERIKALI DODOMA LEO...

Kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungao mjini Dodoma.
Leo Wabunge wanaanza kujadili kwa siku saba mfululizo bajeti ya Serikali ambayo ilisomwa  na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa wiki iliyopita.

Bajeti hiyo imeainisha maeneo ya  kufanyiwa kazi kwa lengo la kusukuma ajenda ya maendeleo huku miradi ya maendeleo katika Wizara kadhaa ikiwa imeongezewa fedha kama ilivyoombwa na wizara hizo. Baadhi ya Wizara ambazo zimepewa nyongeza ni pamoja na Maji, Kilimo na Uchukuzi.
Mjadala kuhusu bajeti ya serikali kwa wabunge utadumu kwa siku saba kabla ya kuhitimishwa Juni 25, huku ukitarajiwa kutawaliwa na majadiliano makali kutokana na hisia ambazo zimeanza kujitokeza siyo tu kwa wabunge, bali pia kwa watu wa kada tofauti.
Majadiliano makali yanategemewa kutokana na hisia ambazo tayari zimeshaanza kujitokeza hasa mtawanyiko wa kodi na tozo mbalimbali za ushuru zilizolenga kuongeza uwezo wa serikali wa kukamilisha mipango yake.
Aidha kitendo cha  serikali kutozingatia bajeti yake kwa mwaka huu wa fedha unaopita utafanya hoja za Wabunge kuwa na msimamo mkali zaidi hasa ikizingatiwa kwamba miaka iliyobaki ya kuonesha wamefanya kazi gani katika majimbo yao ni mdogo.
Taifa hili mwaka 2015 linaingia katika uchaguzi mkuu ambapo ni dhahiri kwamba wengi wa wanaotaka kurejea bungeni watahitaji kuonesha kwamba walishiriki kwa namna moja au nyingine katika maendeleo ya maeneo yao na taifa.
Tayari upande wa upinzani umeshaonesha kuwapo kwa upungufu katika bajeti hiyo ambayo wamesema haitoi nafasi mpya ya vyanzo vya mapato huku ongezeko lililokusudiwa katika mafuta likihofiwa kuwaumiza zaidi wananchi wa kipato cha wastani.
Mafuta ni sehemu ya eneo ambalo limekumbwa na ongezeko la kodi na ushuru katika baadhi ya bidhaa. Bidhaa nyingine ni soda, vinywaji vikali pamoja na leseni za magari.
Aidha kusudio la kuanzisha kodi na ushuru katika huduma mbalimbali zinazotolewa kupitia simu za mkononi, ikiwamo kodi ya zuio ya asilimia 10 ya kamisheni  ya uhamishaji wa fedha, pia wananchi wa kawaida wameanza kuliona kuwa tatizo kwao.
Katika hotuba yake Mgimwa alisema Serikali itaanza kutoza ushuru wa bidhaa wa asilimia 14.5 kwenye huduma zote za simu za mkononi badala ya muda wa maongezi tu  ambapo alisema katika ushuru huo, asilimia 2.5 zitatumika kugharimia elimu nchini.
Majadiliano yatakavyokuwa katika Bunge tayari yameshaanza kuoneshwa na mawazo ya watu wa kawaida, wataalamu na wanazuoni wengi kwa jinsi walivyohojiwa na waandishi wa habari tangu bajeti hiyo isomwe Alhamisi iliyopita. Hata hivyo, wengi wao wanaona mzigo wa kodi kwa watu wa kawaida.
Waziri Mgimwa alisema katika mwaka ujao wa fedha, Serikali itapandisha ushuru wa mafuta ya dizeli kutoka Sh 215 kwa lita hadi Sh  217 kwa lita, likiwa ni ongezeko la Sh 2.
“Tumeongeza Sh 2 tu kwa kuwa tunatambua tukiongeza ushuru mkubwa kwa magari makubwa ambayo yanatoa huduma kwa jamii, tutawaumiza wananchi,” alisema Dk Mgimwa.
Kadhalika, ushuru wa mafuta ya petroli umeongezwa kwa Sh 61, kutoka Sh 339 kwa lita hadi Sh 400. Hata hivyo, imeongeza kiwango cha ushuru wa mafuta kutoka Sh 200 kwa lita hadi Sh 263 kwa lita, sawa na ongezeko la Sh 63 kwa lita na wakati huo huo mafuta hayo yakiongezewa Sh 50 kwa kila lita, fedha zitakazotumika kuchangia mfuko wa kusambaza umeme vijijini.
Wakala wa Umeme Vijijini (REA) umeongezewa kiasi cha Sh bilioni 186.9 ambazo awali, hazikuwa zimetengwa baada ya Serikali kukubaliana na mapendekezo ya Bunge kupitia Kamati yake ya Bajeti, inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge.
Serikali pia imepandisha viwango vya ada ya mwaka ya leseni za magari. Magari yenye ujazo wa injini yenye ukubwa wa kati ya cc 501 na 1500 yatatozwa Sh 150,000 kutoka Sh 100,000 za sasa.
Bajeti ya serikali imelenga kuondoa vikwazo vya kukua kwa uchumi, kuwezesha maisha bora kwa wananchi na kuhakikisha inadhibiti mfumuko, kuweka mazingira bora ya uwekezaji na kuukuza uchumi kutoka asilimia 6.9 za ukuaji kwa mwaka hadi asilimia 7.
Kuangaliwa kwa misamaha kuliko elezwa na Waziri Mgimwa, ni maksi ambayo inaweza kufichwa na kutopatikana kwa vyanzo vipya vya kodi  ambavyo vingelisaidiana na vyanzo vya kawaida.
Taarifa ya mwisho ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)  katika misamaha zinaonesha kwamba serikali misamaha yake ilikuwa imefikia trilioni 1.8 hali inayoonesha matata katika ukusanyaji wa kodi.
Katika hotuba yake, Mgimwa alizungumzia kodi ya ongezeko la thamani ambapo huduma za utalii nazo zitatozwa kodi hiyo kwa asilimia 18.
Awali hawakuwa na kodi. Kodi hii ni wazi italipwa na watalii wenyewe kwa sababu wao ndio wanaopewa huduma katika mazingira ya kawaida.
 Mshauri wa masuala ya kodi, Innocent Makundi katika mazungumzo alisema kwamba kodi hiyo kwa huduma zinazotolewa katika sekta ya utalii ni dhahiri inavuta huku na kule kwa maana ya kwamba kila upande utanufaika kwa namna fulani.
 Aidha nafuu ya kodi ya ongezeko la thamani kwa viwanda vya nguo nchini  vitaleta nafuu kubwa katika uzalishaji ingawa suala la msingi linakuja utatambuaje kwamba mali ghafi hii ya nguo inakwenda moja kwa moja katika uzalishaji na hii haiendi.
Ni dhahiri mabadiliko haya yanayogusa uzalishaji hasa kwa wabunge ambao maeneo yao yanalima pamba yatawafanya wajadili hoja hii kwa makini zaidi huku serikali ikitakiwa kuangalia makusanyo yake kwa uhakika kutokana na uwezekano wa watu kutumia mwanya huo kuiibia serikali mapato yake.
Mabadiliko katika kodi ya mapato na kuondolewa kwa asilimia 1 kwa PAYE kunaweza kuzua gumzo kwa kuwa  kiasi hicho si kiwango ambacho kilikuwa kinatarajiwa  baada ya hotuba ya Rais Jakaya Kikwete Mei Mosi mwaka huu.
Pamoja na mtawanyiko wa utafutaji wa mapato na marekebisho yake yenye lengo la kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh milioni 510,017.50, bado wabunge watajadiliana kuhusiana na matumizi ya serikali yenye walakini.
Pamoja na makadirio katika upatikanaji wa fedha za maendeleo na matumizi,katika hali ya kawaida  wiki hii ya majadiliano itashuhudia wabunge wakichambua kwa makini bajeti hiyo na kuishauri serikali namna ya kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuelezea hofu zao.
Kwa ujumla, Sh 714 bilioni zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha 2013/2014. Haya ni matumizi ambayo yamekuwa yakiongezeka kila mwaka licha ya lengo la Serikali la kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima tangu mwaka 2010.
Ni dhahiri kwamba wabunge watachagiza kuongezwa fedha katika maeneo yanayonufaisha wananchi moja kwa moja kama vile afya, elimu, maji,  barabara, na kadhalika .
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesema bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2013/2014 bado ni tegemezi na imezidi kuwabebesha mzigo wafanyakazi.
Lipumba aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo alisisitiza kuwa bado bajeti hiyo inaonyesha kuwa matumizi ya Serikali ni makubwa.
“Kwa mtazamo wangu naona Serikali haijawa makini katika hili kwani  bajeti inaonesha dhahiri inategemea misaada na mikopo ya nje ya nchi,” alisema Lipumba.
Alisema bajeti hiyo imeshindwa kuainisha wazi fedha zilizokuwa zinaongezwa kwa kila wizara zinatolewa wapi huku akisisitiza kuwa nyongeza ya fedha hizo kwa kila wizara jumla yake ni Sh bilioni 500 sawa na asilimia 3.
“Swali ni kwamba fedha hizi zinatoka wapi  na isitoshe tatizo kubwa tulilonalo katika taifa ni hili la usimamizi mbovu wa miradi na kufanyiwa uchambuzi,” alisema.
Aidha alisema kitendo cha Bunge kuanza kujadili na kupitisha bajeti ya kila wizara hakikuwa kizuri kwa sababu haikubainishwa wazi kuwa fedha wanazozipitisha zinatoka wapi.
“Sasa tunashuhudia mapato ya ndani ni Sh trilioni 11.5 lakini matumizi ya kawaida ni  trilioni 12. 6 ambao ni makubwa kuliko matumizi ya ndani, hii inamaanisha bajeti ya maendeleo inategemea misaada,” alisema.
Alisema kwa upande wa bajeti ya maendeleo matumizi yake hayajapelekwa kwenye malengo yaliyokusudiwa, huku kukiwa na miradi iliyowasilishwa na kutajwa kwenye hotuba kila mwaka lakini haianzishwi wala kuendelezwa.
Kwa upande wa gesi, Profesa Lipumba, alisema bajeti hiyo haijaonyesha  uchambuzi yakinifu juu ya bomba la gesi la Mtwara kitendo ambacho kimefanya awasiliane na Benki ya Dunia kuhoji kama nao tayari wamepatiwa taarifa ya suala hilo ambao nao walidai kuwa hawana taarifa hiyo ingawa walishaomba.
Aidha mwenyekiti huyo, alisema kuwa bajeti hiyo haikuonesha utekelezaji wake wa ajira 70,000 zilizoainishwa katika bajeti ya 2012/13 na badala yake imetaja kwa mafungu bila ufafanuzi.
Kuhusu eneo la kodi kwa wafanyakazi, alisema asilimia moja iliyopunguzwa kwenye Kodi ya Lipa Kadri Unavyopata (PAYE) ni kiini macho kwani, bado kiasi kinachokatwa na Serikali ni kubwa kuliko kiwango anachopata mfanyakazi husika.
“Haiwezekani mtumishi anayelipwa mshahara wa Sh 500,000 atozwe kodi ya Sh 62,000, huu ni ukandamizaji mkubwa,” alisisitiza.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item