WANASIASA WAICHIMBIA KABURI SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA ZANZIBAR...

Balozi Seif Ali Iddi.
Makamu wa Pili wa  Rais, Balozi Seif Ali Iddi amehadharisha kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa inaweza kumeguka iwapo viongozi wataendelea kutumia vibaya majukwaa ya kisiasa kutoa kauli za chuki na matusi na kukashifu Serikali kwa maslahi binafsi.

Ingawa Balozi Iddi amesema uhusiano wa viongozi wakuu watatu wa nchi; Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad na yeye ni mzuri na wanafanya kazi vizuri katika Baraza la Mawaziri, aliishutumu CUF kutumia majukwaa ya kisiasa vibaya.
Amesema kasoro kubwa zinajitokeza katika majukwaa ya kisiasa ambako viongozi wamekuwa wakitoa kauli za chuki zenye kutia wasiwasi mkubwa wananchi na kuhoji uhusiano wa viongozi hao kiasi cha kutukanana hadharani.
Akifanya majumuisho jana na kujibu hoja za wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliochangia Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa mwaka ujao wa fedha, Balozi Idd aliilaumu hususan viongozi wa CUF. Maalim Seif ni Katibu Mkuu wa Chama hicho.
Alisema katika mikutano yao yote wanayofanya, wamekuwa wakitumia vibaya majukwaa kumtukana yeye binafsi na kumchonganisha na wananchi na Serikali iliyopo madarakani.
“Napenda kuwaambia wananchi uhusiano wa viongozi wakuu wa Serikali ni mzuri sana, lakini majukwaa ya kisiasa yanatumiwa vibaya kutukanana. Tukiendelea hivyo, hatufiki pahala na tutarudi tulikotoka,” alisema.
Kwa mujibu wa Makamu wa Rais, amekuwa akipewa majina mabaya na viongozi wa CUF katika mikutano ya kisiasa  ikiwemo 'laanatullahi' wakimaanisha kumlaani jambo ambalo alisema anajiuliza amewakosea nini.
Balozi Iddi aliwahadharisha  viongozi hao kwamba lengo la Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni kuleta mshikamano kwa Wazanzibari wote.
Alionya, kwamba watu wanaweza kurudi ambako hawakuwa wanazikana wala kushirikiana katika matukio kutokana na siasa za chuki na uhasama kutawala tangu ulipoingia mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992.
“Tuache kutukanana katika hadhara za majukwaa ya kisiasa. Hawa (CUF) sijui nimewakosea nini na kama majina yanachuna basi tayari ngozi yangu ingeathirika,” alisema.
Alikumbusha viongozi na wananchi kwamba kilichounganishwa ni Serikali yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa lakini vyama vya siasa na sera ni tofauti na hakuna sababu ya kulumbana katika hilo.
Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud, alisema Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) iko kwenye mchakato wa kuboresha Daftari la Wapiga Kura nchini kote.
Alitaka wanasiasa kujenga tabia ya kuwaamini watendaji wa taasisi hiyo na kuacha kuwahukumu kwa kuwashutumu, kitendo ambacho kinaweza kuzorotesha utendaji kazi zao.
“Tume hii imefanya kazi vizuri sana, tangu mchakato wa kura ya maoni mwaka 2010 pamoja na kusimamia Uchaguzi Mkuu ambao ulikwenda vizuri na vyama vyote kuridhika,” alisema Aboud.
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walipitisha makadirio ya mapato na matumizi ambayo yalichukua takribani saa tatu wakihoji vifungu vya matumizi.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar iliundwa mwaka 2011 baada ya wananchi kuiunga mkono kupitia kura ya maoni na kushinda kwa asilimia 64.
Muundo huo wa Serikali chini ya CCM na CUF, ulifikiwa kuondoa siasa za chuki na uhasama visiwani humo.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item