MAWAZIRI SADC, MABALOZI WATEMBELEA ZIWA NYASA...
https://roztoday.blogspot.com/2013/08/mawaziri-sadc-mabalozi-watembelea-ziwa.html
Wananchi wakiendelea na shughuli za uvuvi katika Ziwa Nyasa upande wa Tanzania. |
Mawaziri zaidi ya 25 na mabalozi kutoka nchi 14 wanaohudhuria Mkutano wa 33 ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini wa Afrika (SADC) waliopo jijini hapa wametembelea Ziwa Nyasa upande wa Malawi.
Sambamba na hilo, Tanzania na Malawi zimeonywa ziache kuzungumzia mgogoro wa ziwa hilo na kuliacha suala hilo lishughulikiwe na jopo la marais wastaafu wa Afrika ambao ni Thabo Mbeki (Afrika Kusini); Joachim Chisano (Msumbiji) ambaye ni Mwenyekiti wa Jopo na Festus Mogae (Botswana) pamoja na wanasheria saba wa kimataifa.
Akizungumzia jana ziara hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema mawaziri hao walioneshwa ziwa hilo bila maelezo yoyote na wakapata chakula cha mchana na kuondoka.
"Ilikuwa raha na nafasi nzuri kwa sisi mawaziri wawili (yeye na Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Ephraim Chiume) kuzungumzia hali ya sasa ya mgogoro huu na namna ya kuandaa viongozi wetu (Jakaya Kikwete na Joyce Banda) ili wapate fursa ya kujadiliana juu ya mgogoro huu iwapo wataamua kulijadili," alisema.
Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Adadi Rajab ambaye yuko hapa kuhudhuria mkutano huo, alisema: "tulipelekwa Ziwa Nyasa lakini hatukuambiwa kitu chochote na tukala chakula cha mchana na kurudi, tulikaa pale kama saa moja na nusu; tulikwenda Salima upande wa Malawi".
Mgogoro huo uliibuka baada ya Serikali ya Malawi bila kushauriana na Tanzania kutoa leseni kwa kampuni mbili za kigeni kutafuta mafuta eneo la Ziwa upande wa Tanzania.
Chanzo cha mgogoro huo ni mikataba yenye utata iliyoachwa na wakoloni, ambapo kwa kulitambua hilo, marais waliotangulia hasa Bakili Muluzi na Bingu wa Mutharika wa Malawi na wenzao Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa waliendeleza mazungumzo.
Baada ya Rais Banda kuingia madarakani mgogoro huo uliongezeka, hasa baada ya kubainika kuwa katika ziwa hilo ambalo Malawi inaliita Ziwa Malawi kuna kiasi kikubwa cha mafuta.
Kuhusu mgogoro huo, Membe alisema kwa sasa Tanzania na Malawi zimekubaliana kutozungumzia mgogoro huo na kuachia jopo la marais kutafuta usuluhishi baada ya kuonywa na kushauriwa kufanya hivyo.
Hata hivyo, alisema iwapo jopo hilo litashindwa kutatua mgogoro huo au likashauri suala hilo lipelekwe Mahakama ya Kimataifa (ICJ), Tanzania itakuwa tayari kutekeleza hilo.
"Jopo la marais likishindwa au likatwambia tusonge mbele kwenye ICJ, Tanzania tutakuwa tayari lakini kisheria Malawi haiwezi kwenda ICJ peke yake, lazima Tanzania turidhie. Lakini tuna imani jopo la marais wa Afrika wanaoshughulikia mgogoro huu litaupatia ufumbuzi mgogoro huu," alisema Membe.
Hivi karibuni Malawi ilitishia kujitoa kwenye mazungumzo ya kutafuta suluhu ya mgogoro huo na kulipeleka suala hilo ICJ, lakini Tanzania ikasema kama Malawi itakiuka makubaliano ya suala hilo kutafutiwa ufumbuzi na jopo la marais, itaomba ushauri wa nini kifanyike kutoka kwa jopo hilo.
Tanzania iliionya nchi hiyo kutojaribu kugusa eneo hilo la mpaka na kueleza kuwa nchi nyingi zinaishangaa Malawi kwa uamuzi huo.
Makubaliano baina ya nchi hizo mbili yaliyofanyika Novemba 7 mwaka jana, Dar es Salaam, nchi hizi zilikubaliana jopo liwe sehemu ya mwisho ya makubaliano.
Tayari Malawi imelalamika Uingereza, Marekani, Umoja wa Afrika (AU) na SADC.