MWAKYEMBE AWATAJA WALIOPITISHA 'UNGA' UWANJA WA NDEGE DAR...
https://roztoday.blogspot.com/2013/08/mwakyembe-awataja-waliopitisha-uwanja.html
Dk Harrison Mwakyembe (kulia). |
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ametaja watu zaidi ya saba wanaodaiwa kula njama ya kupitisha dawa za kulevya kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam mwezi uliopita na kuagiza wafukuzwe kazi na kushitakiwa.
Watu hao waligundulika kupitia mfumo wa kamera za usalama (CCTV) katika uwanja huo wakiwamo maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa waliokuwa zamu kwa kuchelewa kufikisha mbwa kwa wakati mwafaka.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana, Dk Mwakyembe alisema Serikali imeliagiza Jeshi la Polisi kutumia mtandao wake wa kipolisi kumkamata Nassoro Said Mangunga aliyekwepa vyombo vya Dola Afrika Kusini na kutoweka.
Alisema Mangunga alitoweka na mabegi matatu ya dawa za kulevya na hivyo anatakiwa aunganishwe kwenye kesi inayokabili wasichana wawili Watanzania, Agnes Gerald 'Masogange' na Melisa Edward waliokamatwa wakiwa na mabegi sita ya dawa hizo.
Waziri alisema Serikali ina taarifa kuwa wasichana hao wamefikishwa mahakamani na hatma ya kesi yao wanaifuatilia kwa karibu.
Alisema wizara inaagiza mbeba mizigo, Zahoro Selemani afukuzwe kazi na mwajiri wake na asikanyage katika uwanja huo huku Polisi wakitakiwa kumkamata na kumwunganisha na wenzake kujibu mashitaka ya jinai chini ya sheria ya kuzuia dawa za kulevya sura ya 95 ya mwaka 1996.
Mwakyembe alisema kutokana na tukio hilo, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege inatakiwa kuwafukuza kazi mara moja wafanyakazi wake waliohusika na njama za kupitisha mabegi tisa yenye uzito wa kilo 180 kwenye uwanja huo Julai 5.
Alitaja wafanyakazi hao ambao ni maofisa usalama kuwa ni Yusuph Issa, Jackson Manyonyi, Juliana Thadei na Mohamed Kalungwana, ambao baada ya kufukuzwa kazi, wakamatwe na kuunganishwa kujibu mashitaka chini ya sheria ya kuzuia dawa za kulevya.
Pia aliitaka Polisi kumwondoa katika uwanja huo Koplo Ernest na kumchukulia hatua za kinidhamu kwa kushiriki katika njama hizo.
Waziri Mwakyembe aliitaka Idara ya Usalama wa Taifa kufanya uchunguzi wa kina kwa maofisa wake waliokuwa zamu kwa kuchelewa kufikisha mbwa wakati mwafaka hivyo kulisababishia Taifa fedheha kubwa.
Akizungumzia tukio zima lilivyoonekana katika kamera hizo, alisema siku hiyo saa 9.28 alfajiri zilimwonesha mbeba mizigo Selemani akizunguka zunguka eneo la kuingilia abiria kama mtu aliye na mihadi na mtu.
Pia zilimnasa mfanyakazi wa uwanjani hapo sehemu ya ukaguzi, Issa, akitoka na kuingia katika jengo la abiria na kuzungumza na simu, kitendo ambacho hakiruhusiwi kwa wafanyakazi wa eneo la ukaguzi wa abiria.
"Zilimwonesha Koplo Ernest akirandaranda eneo la uhakiki wa hati za kusafiria kama anayesubiri kitu, na ilipofika saa 10.15 alfajiri walionekana wasichana wawili na mvulana sehemu ya kuingilia abiria wakiwa na mabegi tisa yanayofanana," alisema Mwakyembe.
Wasichana hao walifuatana na Mangunga na Koplo Ernest akionekana akihangaika kusubiri abiria kuweka mizigo yao kwenye mashine ya ukaguzi kazi ambayo si yake.
"Aidha, mbeba mizigo Zahoro alionekana akisaidia vijana hao watatu kupeleka mizigo kwenye mashine ya ukaguzi na baadaye kuyafungasha kwa nailoni na kuyafikisha kaunta ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA)," alisema.
Dk Mwakyembe aliongeza kuwa baadaye Issa alimwondoa mfanyakazi mwenzake Manyonyi na kukalia kiti cha ukaguzi wa mizigo, dakika chache kabla ya vijana wenye mabegi tisa kuingia kwenye mashine, kinyume cha utaratibu kwani Issa hakujiandikisha kwenye kitabu cha wakaguzi.
Alisema ilipofika saa 10.16 alipitisha mizigo hiyo kwa dakika sita na kumwachia kiti Manyonyi na kuondoka akibadilishana maneno na Koplo Ernest na kumnong'oneza kitu Manyonyi na kuelekea ukumbi wa abiria wasafiri ndani ya nchi, mambo yote yalifanyika huku kiongozi wa sehemu ya ukaguzi, Thadei, akiwapo lakini hakushituka.
Baada ya kupitisha mizigo, walihamia kaunta ya SAA ambapo mabegi sita yalitakiwa kulipiwa malipo ya ziada kwa kila kilo iliyozidi (hulipiwa dola tano) na kutakiwa kulipa dola 600 lakini walitozwa dola 94 tu zilizothibitishwa katika stakabadhi, alisema Waziri.
"Katika tukio lisilo la kawaida, Mangunga ambaye hakuwa na tiketi ya kusafiria siku hiyo aliondoka kwenda Afrika Kusini na kulipa dola 60 kwa huduma hiyo, hivyo mhakiki wa nyaraka za safari nje ya ukumbi wa abiria siku hiyo, Kalungwana, hakupaswa kumruhusu aingie ndani bila tiketi," alisisitiza.
Alisema kwa kawaida mizigo hukaguliwa tena na mbwa, lakini siku hiyo walichelewa na kutumika baada ya mizigo kuingizwa kwenye masanduku ya chuma.
Mwakyembe alisema kwa abiria watatu kuwa na mabegi tisa tena yanayofanana si kitu cha kawaida kukwepa jicho la maofisa ushuru na forodha na vyombo vya usalama.