Aamka asubuhi na kukuta miguu imekatika

Mmkazi wa Ludewa, Mkoani Njombe, Yohana Nkwera 
Mmkazi wa Ludewa, Mkoani Njombe, Yohana Nkwera (54) anadai kukatika miguu katika hali ya kushangaza.
Yohana anasema katika maisha yake amekuwa ni mwenye hofu kubwa baada ya kukumbwa na tukio hilo la aina yake la kukatika miguu akiwa usingizini. Anasema hadi sasa haelewi namna hasa tukio hilo lilivyomtokea, kwani hakuhisi maumivu yoyote .
Anasema tukio hilo la aina yake lilimtokea mwaka 1992, lakini halikuwahi kuandikwa wala kutangazwa, badala yake ni watu wachache waliokuwa wakilifahamu.
Anasema siku hiyo usiku alikwenda kulala kama ilivyo kawaida, alipoamka asubuhi alikuta miguu yake imekatika.
Kilichomshangaza zaidi ni kwamba hapakuwa na damu wala jeraha lilionekana. Palionekana pana kovu, kana kwamba alikatika mguu muda mrefu uliopita.
Anasema mara ya kwanza ulianza kupotea mguu wa kulia, hiyo ilikuwa ni mwezi Machi, 1992. Kutokana na tukio hilo, ndugu zangu walifanya jitihada mbalimbali ikiwemo kufanya maombi katika nyumba mbalimbali za ibada, huku wengine wakienda kwa kuwaona waganga wa jadi.
“Kama binadamu wa kawaida ilichukua muda sana kuamini kilichotokea ndani ya maisha yangu na mguu wangu,” anasema.
Mwezi mmoja baadaye yaani mwezi Aprili mguu wa kushoto nao ulikatika katika mazingira yaliyo sawa na yale ya awali.Inaweza kuwa vigumu kuamini lakini ulimwengu ndivyo ulivyo.
Anakumbuka mazingira ya kukatika kwake yanahusishwa na imani za kishirikina kwa sababu siku chache zilizopita kabla ya kukumbana na dhahama hiyo aliwahi kukorofisha na mtu katika vilabu vya pombe za kienyeji anayesadikiwa kufanya tendo hilo.
Baada ya miaka saba kupita Yohana alipelekwa Hospitali Teule ya Ikonda wilayani Makete kupata huduma za tatizo lake. Alifanikiwa kupata msaada wa baiskeli ya magurudumu, ambayo aliitumia kwa miaka mitano.
Kwa sasa baiskeli hiyo haifanyi kazi kutokana na watu wanaosadikiwa kuwa ni wezi kuiba matairi na vyombo muhimu vinavyoiwezesha baiskeli hiyo kufanya kazi.
Pamoja na kupewa baiskeli hiyo na wasamaria wema, Yohana anakiri pia kuchongewa viatu na hospitali hiyo ambavyo vinamuwezesha angalau kutembea umbali mfupi.
Kutokana na ulemavu huu wa kimiujiza, Yohana anakiri ndoto zake za maisha hazijatimia mpaka leo na inawezekana zikawa zimepotea kabisa.
Mipango yake
Alipinga mambo mengi yakiwemo kusoma na hata kufungua miradi ya maendeleo. Sasa ni kama anaona haiwezekani tena kwa sababu hana uwezo thabiti wa kufanya kazi; ukizingatia ni kijijini ambako kazi kubwa inayotegemewa kiuchumi ni kilimo cha jembe la mkono.
Ulemavu huo umesababisha ashindwe kuoa, kwani anasema katika ulimwengu wa sasa ni ngumu kuoana na mtu kama huna uwezo wa kumhudumia.
Anasema ilikuwa ni ngumu kwa ndugu kuamini kinachotokea lakini anawashukuru wasamaria wema walioendelea kumhudumia mpaka pale alipoikubali hali yake na kuanza kuishi katika huo mfumo mpya wa maisha.
Kwa sasa Yohana anaishi na dada yake mkubwa aitwaye Lucy Nkwera akimsaidia kwa mahitaji ya kila siku ikiwemo chakula na huduma za usafi na usalama kwa jumla.
Akisimulia kwa hisia, Yohana anakumbuka jinsi alivyokuwa katika hali ya uzima wa miguu na kujitegemea, kwamba anashangaa sana kuona leo amekuwa ni mtu wa kuomba msaada; kwa sasa msaada wake mkubwa ni dada yake huyo.
Lucy anasema, “Maisha ni magumu sana kwa kuwa anatakiwa kuwa karibu naye, kwani hakuna mwingine wa kumsaidia.”
Mbali na kupata huo ulemavu wa miguu, Yohana anaumwa ugonjwa wa kifafa, ambao nao aliupata baada ya kukatika miguu.
Ugonjwa huu unamfanya kupoteza fahamu mara kwa mara kitendo ambacho ni hatari kwa afya na maisha yake.
Anamshukuru Lucy kwa kuendelea kumhudumia kwa sababu kwa mazingira ya kawaida ni wachache wenye moyo wa huruma kiasi hicho, hasa kumhudumia mgonjwa ambaye hatarajii kupona leo hata kesho.
Anashukuru pia ndugu zake kutoka maeneo mengine akisema kuwa nao wamekuwa wakija kumtaka hali na kumletea vyakula.
Anaishukuru Serikali ya Kijiji cha Ludewa anachoishi, kwa kumkumbuka na kumhudumia kwa kadiri wanavyoweza.
Anasema kama Serikali na ndugu wasingekuwa wanamsaidia, huenda hali yake ingekuwa ngumu zaidi na ilivyo sasa kwani kwa jumla afya yake ni dhaifu.
Ushauri wake
Yohana anawaomba watu kuachana na tabia za kunyanyapaa walemavu.Anasema baada ya kuwa na ulemavu, kuna marafiki zake walimtenga.
“Inauma sana kuona kumbe wengine ni marafiki wa wakati wa raha...Ukiwa na matatizo wanakukimbia, hii tabia si nzuri, ni lazima tuwe na moyo wa kusaidiana wakati wote,” anasema Yohana.
Anaongeza kuwa hata yeye hakupenda kuwa katika hali ambayo anayo sasa. Ndiyo kusema kwamba yeyote anaweza kupatwa na lolote kabla ya hajafa, tusinyanyasane.

Na Ayubu Mapunda, Mwananchi
Source @Mwananchi

Related

Weird News 4684537220851093639

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item