Posho za Bunge la Katiba kufuru

SIKU chache tu baada ya Rais Jakaya Kikwete kutangaza majina ya wajumbe walioteuliwa kuingia kwenye Bunge Maalumu la Katiba, posho za wabunge hao kwa siku ni kufuru.
Habari ambazo gazeti hili imezipata, zinasema kuwa posho ya mjumbe mmoja kwa siku ni sh 700,000 hivyo kwa siku 70 kila mjumbe atalipwa sh milioni 49.
Endapo Bunge hilo linalotarajiwa kuanza Februari 18 litalazimika kuongeza siku 20, na hivyo kuwa na siku 90 bungeni, kila mjumbe ataibuka na kitita cha sh milioni 63.
Malipo ya wabunge hao kwa siku ni tofauti na wenzao wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ambao kwa kikao wanalipwa sh 200,000 na fedha za kujikimu zisizopungua sh 150,000 kwa siku hivyo kuwafanya kupata sh 350,000.
Inaelezwa kuwa kiasi hicho cha posho kimependekezwa kwa wabunge hao kwa vile hawana mishahara, wala magari na nyumba kama ilivyokuwa kwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyoongozwa na Jaji mstaafu, Joseph Warioba au kwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ambao wana mishahara, posho, mafuta ya magari na mikopo.
Vyanzo vya habari vinasema kulikuwa na mvutano mkubwa serikalini kuhusu posho hiyo kwani kulikuwa na pendekezo la sh 500,000 na sh 700,000 kwa siku.
Akizungumzia posho za wabunge hao, Katibu wa Bunge, Thomas Kashililah, alisema kuwa bajeti ya Bunge la Katiba imo ndani ya bajeti ya serikali katika mfuko mkuu wa Hazina uliopitishwa katika Bunge la Bajeti Juni 2013.
Alisema kuwa bajeti ya Bunge hilo ni sh bilioni 28 zilizotengwa, lakini hadi sasa hajui kila mjumbe atapata kiasi gani kama posho kwa siku.
“Mamlaka ya kuamua yapo kwa rais kwa mujibu wa sheria namba 83 ya mwaka 2011, ambayo imempa mamlaka hayo kupanga masharti ya wajumbe wa Bunge hilo.
“Kuhusu kulipwa laki saba kwa siku hatujasikia tetesi hizo hadi sasa, lakini bajeti hiyo ya bilioni 28/- imezingatia viwango vilivyopo sasa,” alisema.
Wakati wa mchakato wa katiba, serikali ilitenga sh bilioni 40 kwa ajili ya mishahara na posho za wajumbe 34 wa Tume ya Kuratibu Maoni ya Katiba, iliyoongozwa na Jaji Warioba.
Kwa mujibu wa kasma ya tume hiyo iliyoko kwenye bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2012/2013, serikali imetenga sh bilioni 40 ambapo sh bilioni 10 kwa ajili ya posho ya mwaka mmoja tu.
Katika kasma hiyo, wajumbe hao 34 walilipwa posho ya sh 450,000 kwa siku, sawa sh milioni 13.5 kwa mwezi na kwa mwaka kila mjumbe alipata sh milioni 300.
Malipo hayo yalianza kutolewa Julai mosi mwaka jana hadi pale tume ilipomaliza muda wake hivi karibuni.
Katika kasma hiyo, madereva, na watumishi wengine wa tume walitengewa sh bilioni 4.8 na kila mfanyakazi alilipwa posho ya sh 50,000 kwa siku.
Posho ya mwenyekiti na makamu wake, iliongezewa fedha za viburudisho, hivyo fungu lao lilikuwa kubwa zaidi.
Gharama nyingine za bajeti hiyo ni pamoja na sh milioni 250 zilizotumika kwa ajili ya ulinzi na usalama wa ofisi za tume na sh milioni 10 zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za mazishi endapo mmoja kati ya wajumbe hao angepoteza maisha. Mjumbe mmoja, Dk. Sengondo Mvungi, alifariki dunia.
Mbali ya posho hiyo, kila mjumbe alipewa ‘shangingi’ pamoja na nyumba ya kuishi wakati uhai wa tume hiyo ilikuwa miezi 18 tu.
Wajumbe wa tume hiyo kutoka Tanzania Bara ni Profesa Mwesiga Baregu, Riziki Shahari Mngwali, Dk. Mvungi ambaye alifariki dunia mwishoni mwa mwaka jana, Richard Shadrack Lyimo, John Nkolo, Alhaji Hamad Saidi El Maamry na Jesca Sydney Mkuchu.
Wajumbe wengine wa tume hiyo kutoka bara ni Profesa Palamagamba Kabudi, Humphrey Polepole, Yahya Msulwa, Esther Mkwizu, Maria Malingumu Kashonda, Mheshimiwa Al-Shaymaa Kwegyir, Mwantumu Jasmine Malale na Joseph Butiku.
Wajumbe wa tume hiyo kutoka Tanzania Visiwani ni Dk. Salim Ahmed Salim, Fatma Saidi Ali, Omar Sheha Mussa, Raya Suleiman Hamad, Awadh Ali Saidi, Ussi Khamis Haji na Salma Maulidi. Wengine kutoka Visiwani ni Nassor Khamis Mohammed, Simai Mohammed Saidi, Muhammed Yussuf Mshamba, Kibibi Mwinyi Hassan, Suleiman Omar Ali, Salama Kombo Ahmed, Abubakar Mohammed Ali na Ally Abdullah Ally Saleh.
Shughuli Bunge Maalumu la Katiba zitaratibiwa na sekretarieti ambayo katibu wake atakuwa Assaa Ahmad Rashid na Naibu Katibu atakuwa Casmir Sumba Kyuki.
Tanzania Daima, imedokezwa kuwa baadhi ya makamishna wa Bunge, walikwenda mkoani Dodoma kukamilisha taratibu mbalimbali ili wajumbe wafanye vikao katika mazingira mazuri.
Chanzo kimoja kimeongeza kuwa masuala yanayohusu Bunge hilo yanashughulikiwa kwa ushirikiano kati ya Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi.
Kiliongeza kuwa Sekteratieti ya Bunge hilo inatarajia kuanza kazi wakati wowote kuanziasa sasa ikiwashirikisha watumishi wa umma kutoka maeneo tofauti kulingana na sifa walizonazo na mahitaji.
 
Source @Tanzania Daima

Related

WorldNews 1091388931905762229

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item