CHEKA TARATIBU...
https://roztoday.blogspot.com/2012/03/cheka-taratibu_24.html
Vijana wawili wa Kisukuma, Masanja na Kashindye walipata zali la kwenye New York, Marekani kwa ziara ya matembezi. Walipofika Uwanja wa Ndege wa New York wakapokelewa vizuri na wenyeji wao ambao waliwapeleka moja kwa moja hotelini wapate kujipumzisha na uchovu wa safari. Walipofika hotelini wenyeji wakawaacha kwa makubaliano ya kuja kuwafuata kesho yake tayari kwa kuanza ziara. Wasukuma wale kama ilivyotarajiwa wakaanza kushangaa kila kitu, na kwa bahati mbaya ama nzuri walifikia chumba kilichopo kwenye ghorofa ya arobaini. Wakati wakipangua vitu vyao ndipo Kashindye akagundua kuwa wamesahau kubeba miswaki. Kama kawaida yake Masanja ndiye mjanja kidogo, hivyo wakakubaliana ndiye aende akatafute sehemu inayouza miswaki. Dakika kumi baada ya kuondoka, Kashindye akagundua kasahau pia kubeba kiwembe. Bila kupoteza muda akaelekea kibarazani na kuanza kupiga kelele, “Masanja na kiweeeeeembeee, Masanja na kiweeeeembee!” Kutokana na kelele zile wapangaji wa ghorofa ya chini yao wakatoka na kutazama kulikoni?” Mzungu mmoja kwa kutoelewa lugha akadhani shida ya Kashindye ni kutaka kuona chini, akampa darubini ili aache kupiga kelele. Kashindye kwa kutumia darubini akafanikiwa kumuona Masanja kwa karibu. Kitendo bila kuchelewa si akaanza kunong’ona, “Masanja, Masanja, Masanja na kiwembee!” Kwa mshangao Masanja aliendelea tu kuchanja mbuga ndipo Kashindye akarudia kelele kwa lafudhi ya Kisukuma, “We Masanja acha dharau, nimekwambia na kiweeembeee!” Duh, ushamba kweli mzigo!
