JIBWA LACHACHAFYA MTAA NA KUJERUHI VIBAYA POLISI WATANO...
https://roztoday.blogspot.com/2012/03/jibwa-lachachafya-mtaa-na-kujeruhi.html
Picha mbalimbali zinazoonyesha patashika hilo kati ya jibwa na polisi ambao walilazimika kulitandika risasi nne ndipo amani ikarejea. PICHA MBILI KUSHOTO: Polisi wakishambuliwa na jibwa hilo. PICHA MBILI KULIA: Damu ya polisi waliojeruhiwa na ya jibwa baada ya kutandikwa risasi ikiwa imetapakaa katika barabara mtaani hapo.
Mwanamuziki akisakwa kwa tuhuma za utekaji, ameshitakiwa chini ya kifungu cha “Sheria ya Mbwa Hatari” juzi baada ya kumfungulia mbwa wake na kuwararua polisi watano waliokwenda kwake kumkamata.
Pierre Robinson mwenye miaka 25, alifikishwa mahakamani muda mfupi baadaye akituhumiwa kumwachia mbwa huyo kwa makusudi atoke nje ya nyumba mjini Albert Square, mashariki mwa London.
Pia anahusishwa na tuhuma kwa kumteka mtu mmoja, katika tukio la Machi 14, mwaka huu mjini Newham, polisi wamesema.
Polisi watano wamelazwa hospitali baada ya kujeruhiwa vibaya na mbwa huyo na inasemekana wakiuguza majeraha yao sehemu mbalimbali za mwili ambapo waligundulika mara baada ya mbwa huyo kupigwa risasi na kufa.
Ofisa mmoja wa polisi alivunjwa mkono na mbwa huyo, wakati wengine walitobolewa na kukwaruzwa na meno kiasi cha nyama kuning’inia kwenye miguu na mikononi. Baadhi watalazimika kufanyiwa upasuaji, na mwingine atalazimika kukatwa vidole kadhaa.
Polisi mmoja mwenye bunduki aina ya shortgun alifika eneo la tukio na kumaliza mapambano hayo pale alipomtandika risasi nne mbwa huyo baada ya polisis kadhaa kumzingira.
Robinson sasa anakabiliwa na mashitaka manne kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Thames, ikiwamo kumiliki mbwa mkubwa hatari, chini ya kifungu cha Sheria ya Mbwa Hatari.
Shitaka la pili limeelezwa kuwa ni kuachia mbwa kwa kukusudia na kujeruhi watu watano. Pia anakabiliwa na mashitaka ya utekaji nyara.
Majira ya asubuhi, polisi walikuwa wakifanya operesheni kali ya nyumba kwa nyumba kwa lengo la kusaka watuhumiwa wote wa makosa mbalimbali mjini humo.
Operesheni hiyo ya saa 48 ilishuhudia mamia ya askari wakisaka watu wanaotafutwa na polisi ama walioshindwa kufika mahakamani kujibu mashitaka yao.
Majirani wamesema, walisharipoti Halmashauri ya Mji huo mara kadhaa kuhusu mbwa huyo waliyempachika majina ya Nyati Kichaa na wengine wakimwita Sumu.
Wamesema mbwa amehusika kwenye mashambulio kadhaa ya kudhuru likiwamo lile la fundi mwashi mmoja aliyevutwa kutoka kwenye baiskeli yake na kuanza kuraruriwa vibaya mno kiasi cha ‘kuonekana kama analiwa akiwa hai’.
Shambulio hilo lilitokea kwenye mtaa wa makazi ya watu mjini Stratford, mashariki mwa London, ambapo mabaka ya damu iliyoganda yanaonekana kwenye barabara umbali wa futi 30.
Mashuhuda wamesema mbwa aliachiwa wakati askari wakimsaka mtu aliyevunja mlango kwenye nyumba moja mtaani hapo.
Wakazi wa Albert Square, Newham, wameeleza alimvamia kabla ya kuanza kumng’ata mwendesha baiskeli mwaka jana.
Mjamzito Rehema Nyange alisema wamewaita mara kadhaa wahusika wa Halmashauri ya Newham. Hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.
“Nimuonapo mbwa yule mtaani, huwa natimua mbio. Nilikuwa namwogopa sana. Unajua kuna watu wenye watoto hapa mtaani na kuna shule jirani na hapa. Ingekuwa rahisi mno kumdhuru yeyote,” alimalizia.
“Nafurahi hatimaye ameuawa.”
Akizungumzia shambulio aliloshuhudia Septemba mwaka jana, dada huyo mwenye miaka 30 anasema: “Alimshambulia kijana aliyekuwa akipita na baiskeli kuelekea kazini. Mbwa alikuwa akirandaranda mtaani. Kisha akamnyaka Yule kijana mguu. Alimtafuna vibaya sana.
“Iliwawia vigumu sana madaktari waliofika kumpa msaada, kwani walilazimika kuchana-chana suruali yake kwanza ndipo waweze kumtibu. Yalikuwa majeraha makubwam sana.
“Alikuwa akibebwa kama mtoto na mbwa huyo, kila mtu alikuwa akiogopa kwenda kumsaidia kwa kuhofia mbwa yule angemgeukia na kumshambulia.”
Msemaji wa Halmashauri ya Newham amesema: “Aprili 28 mwaka 2011, Halmashauri hiyo ilichunguza madai hayo kwamba mbwa kamng’ata mwendesha baiskeli mjini Albert Square.
“Mei 6, 2011, Maofisa wa Halmashauri wanaohusika na wanyama walifanya ziara eneo husika lakini hawakupatiwa ushirikiano wowote.
“Kesi hii ilijadiliwa na polisi pamoja na Halmashauri Juni, 2011.
“Kwa kuwa sasa unafanyika uchunguzi wa makosa ya jinai, haitakuwa wakati muafaka kutolea ufafanuzi wowote.”
Hatimaye mbwa huyo alizingirwa na askari kutoka vituo kadhaa vya polisi vilivyo jirani na hapo wakiwa wamebeba ngao za kudhibiti ghasia.
Ndipo askari mwenzao kutoka Kitengo Maalumu cha Polisi mwenye namba CO19 akawasili na kumtandika risasi nne mbwa huyo.
Dennis Clarke mwenye miaka 71 amebainisha kuwa aliwaita wahusika wa Halmashauri ya Newham miaka mitatu iliyopita kutaka kuelezea hofu yake lakini dhidi ya mbwa huyo lakini hakupata msaada wowote mpaka mbwa alipomng’ata mtu.
Akielezea tukio hilo la sasa anasema: “Nilichoweza kusikia kwanza ni kelele za mtu akiomba msaada. Nikatoka nje na kushuhudi polisi akiwa ameng’atwa mguuni na mbwa huyo hakumwachia. Alikuwa ameng’ang’aniwa.”
Mwanafunzi Gemma Smith mwenye miaka 27 aliongeza: “Niliamshwa na kelele na nikadhani kuna mtu amevamiwa.”
Anasema polisis waliwataka wakazi wote kuingia ndani wakati wakimdhibiti mbwa huyo.
“Nikasikia mlio wa risasi. Nilipotazama nje kupitia dirishani nikaona mbwa akigaagaa chini.”
Polisi wote watano inaelezwa kuwa hali zao zinaendelea vizuri kwenye Hospitali ya Royal London Hospital.
Halmashauri ya Newham imethibitisha ilichunguza madai ya mbwa huyo kumshambulia mwendesha baiskeli Aprili mwaka jana, na kusema kesi hiyo ilifikishwa na kuamuliwa na polisi mwezi Juni.
Utata ulioibuka ni kuwa kwanini polisi walishindwa kugundua mapema kwamba kuna mbwa hatari kwenye nyumba hiyo kabla hajasababisha madhara.
