MBUNGE JOHN MNYIKA ATIMULIWA BUNGENI...
https://roztoday.blogspot.com/2012/06/mbunge-john-mnyika-atimuliwa-bungeni.html
Mheshimiwa John Mnyika akiagana na baadhi ya wabunge wenzake nje ya viwanja vya Bunge mjini Dodoma, jana.
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) amefukuzwa bungeni na Naibu Spika Job Ndugai baada ya kutamka kuwa Rais Jakaya Kikwete ni dhaifu.
Licha ya maneno hayo, Mnyika pia amesema CCM ni wapuuzi na wabunge ni wazembe ndiyo maana Serikali imeandaa bajeti ambayo haitekelezi Ilani ya CCM na imeuweka kando Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.
Mnyika alikuwa akichangia hotuba ya Bajeti ya Serikali ambayo aliitumia kutetea bajeti kivuli ambayo ilipondwa na baadhi ya wabunge wa CCM, kuwa nayo haitekelezeki na wapinzani wanadanganya wananchi.
Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde ndiye aliyeongoza kebehi kwa wapinzani akatoa mifano namna bajeti yao isivyotekelezeka na jinsi viongozi wa chama hicho akiwamo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe wanavyohadaa wananchi.
Lusinde alizidi kukisakama chama hicho kuwa hakina ukamanda kwani pamoja na kuonesha kuwa wangetoa elimu bure kama walivyoahidi, kwenye bajeti yao hakuna kitu kama hicho.
“Makamanda gani hawa, hakuna cha ukamanda hapa suala si vua gamba vaa gwanda, hapa suala ni vua gwanda vaa uzalendo,” alisema Lusinde.
Katika kujibu hayo mapigo, Mnyika alisimama na kusema bajeti iliyowasilishwa bungeni na Serikali haitekelezi Ilani ya CCM na wala haiendani na Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano.
Hivyo mbunge huyo akatoa mfano kuwa wakati hotuba hiyo ina maneno mazuri; lakini kwenye uhalisia haiendani na mpango huo akatoa mfano kuwa barabara za kumaliza msongamano Dar es Salaam zimepangiwa Sh bilioni 10 tu.
Mbunge huyo aliongeza kuwa Upinzani umetoa mambo halisi na akatoa mfano kuwa waliahidi kulipa pensheni ya wazee, jambo ambalo Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alishawaahidi wakati akihutubia Morogoro kuwa wataanza kulipwa pensheni lakini kwenye bajeti ya Serikali hilo halimo.
Mnyika alisisitiza kuwa bajeti hiyo inashindwa kutekeleza sera ya CCM na Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano, “kutokana na udhaifu wa Rais Kikwete, uzembe wa wabunge na Bunge pamoja na upuuzi wa CCM.
“Haya mambo ndio yametufikisha hapa tulipo,” alisema Mnyika na kutoa mfano kuwa katika Bunge la Februari lilipokaa kama Kamati ya Mipango na kupitisha mpango ambao haujatekelezwa na bajeti hiyo, alishangaa iweje wabunge wa CCM wanaishabikia.
“Haya maneno makali mnayosema hapa nayatumia kwa kweli ngoja niyatumie kutokana na hali halisi ilivyo katika bajeti hii na maneno yanayotolewa na wabunge wa chama tawala,” alisema Mnyika.
Baada ya kutamka maneno hayo, alisimama Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, William Lukuvi na kuomba Mwongozo wa Spika akitumia kanuni za Bunge kifungu
kinachoeleza kulitaja jina la Rais kwa dhihaka bungeni.
“Kanuni inakataza kabisa hapa bungeni kuleta maneno tunayozungumza huko magengeni, maneno aliyotumia hapa ni dhihaka kwa Rais na pia ametumia lugha ya kuudhi.
“Maneno kwamba Rais Kikwete ni dhaifu na kwamba CCM ni wapuuzi ni maneno ya kuudhi…mimi namwomba Mnyika, ni Mbunge ninayemheshimu sana kwa hili kapotoka naomba afute maneno yake hayo, kwani ametumia vibaya jina la Rais kwa kumtaja kwa jina,” alisema Lukuvi.
Baada ya maombi hayo ya Mwongozo, Ndugai alisimama na kusema; “si tu kwamba amemsema Rais vibaya, lakini pia amelisema vibaya Bunge, hivyo nakuomba Mbunge uondoe neno hilo kuwa Rais Kikwete ni dhaifu…” alisema Ndugai.
Mnyika alisimama na kuomba asikilizwe kwanza, aeleze kwa nini alitumia neno hilo, hoja ambayo Ndugai aliikataa na kumtaka afute neno hilo kama anataka kuendelea kutoa mchango.
Lakini Mnyika alisimama na kusema: “Sitafuta neno hili la udhaifu wa Kikwete,” alisema Mnyika na kumlazimu Ndugai kutumia rungu lake la kanuni za Bunge linalomwelekeza kuwa mbunge akigoma kufuta kauli, Spika anaweza kumwamuru atoke nje ya ukumbi wa Bunge.
“Mimi ni Naibu Spika wa uhakika, kwa kuwa nimekutaka ufute kauli yako hujafanya hivyo, naamuru utolewe nje ya ukumbi wa Bunge na Polisi,” Ndugai alitoa kauli hiyo na hivyo kumfanya polisi wa Bunge kwenda alikokuwa amekaa Mbunge huyo ambaye hata hivyo, kabla Naibu Spika hajamaliza kutoa amri hiyo, alisimama na kuelekea lango kuu.
Baada ya agizo la Spika, askari wa Bunge walimwondoa Mnyika na kumsindikiza hadi nje, ambapo alizungumza na wanahabari na kufafanua, kuwa alisema hivyo kutokana na sababu alizokuwanazo, ila hakuzitaja.
“Rais Kikwete ndiye aliyesaini Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano kama Kiongozi Mkuu wa Nchi tena kwa wino mwekundu, mpango ambao sasa unapingana na Bajeti hii,” alisema Mnyika.
Hatua ya Ndugai kumtoa Mnyika nje ilizusha manung’uniko kutoka kwa wabunge wa Chadema na aliposimama Mbunge wa Viti Maalumu, Chiku Abwao (Chadema) alitoa mwito kwa kiti cha Spika kutoa usawa kwa wabunge wote kwa maelezo kuwa wakitoa lugha za kuudhi wabunge wa CCM hawachukuliwi hatua.
“Jana hapa sisi tuliitwa wapuuzi, lakini kiti hicho hakikuchukua hatua yoyote, haya mambo ya lugha ya kuudhi yanahusu wabunge wote na si wa upande wa mmoja,” alisema Abwao.
Baada ya wabunge wa Chadema kumlalamikia Ndugai kuwa anapendelea, Lukuvi alisimama na kutaka viongozi wa kambi mbili bungeni, Serikali na Upinzani, kumsaidia
Spika inapotokea mbunge amesimama na kutoa lugha ya kuudhi.
“Itashangaza kama sisi viongozi tutakuwa tunaongoza kutoa matusi, sisi tuliopewa dhamana hiyo tukisaidie kiti si kwamba Spika ataona na kusikia kila kinachosemwa,” alisema Ndugai.
Alitaka wabunge watofautishe hotuba wanazotoa majukwaani na bungeni. “Hapa bungeni tunabanwa na kanuni na lazima kila mbunge aziheshimu ili kuepuka matatizo yanayoweza kuwapata.
“Tukiruhusu haya mambo ya kusema watu bila hoja ya kuwajadili hairuhusiwi kikanuni, tukiruhusu hali hii tunaweza kupigana siku moja hapa,” alisema Ndugai.
Kabla ya hapo Ndugai pia alimpa onyo Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa aache tabia ya kupayuka ovyo bungeni kwani kufanya hivyo ni kuvuruga shughuli za Bunge.