VIPAUMBELE VYA KAMBI YA UPINZANI BAJETI IJAYO HIVI HAPA...

Kambi ya Upinzani imetoa mapendekeko ya vipaumbele vya Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2012/2013 inayotarajiwa kusomwa katika Bunge litakaloanza mwezi huu, huku ikitoa msisitizo zaidi kupunguza misamaha ya kodi kutoka asilimia tatu hadi kufikia moja.
Kwa mujibu wa taarifa ya mapendekezo hayo iliyotolewa jana na Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (pichani), mambo mengine yaliyopendekezwa na Kambi hiyo ni kupunguza kodi kwenye bidhaa za mafuta ili kupunguza mfumuko wa bei, kufuta mfumo wa posho za vikao na kupeleka sehemu ya tozo ya ujuzi kwenye Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (SDL).
Pia taarifa hiyo ilifafanua kuwa mapendekezo hayo, pamoja na mambo mengine yalikuwa sehemu ya Bajeti Kivuli iliyowasilishwa Bungeni na Kambi ya Upinzani ambapo Kodi za Mafuta ya Petroli na Dizeli na tozo ya SDL yalikubaliwa na kutekelezwa.
Ilielezwa kuwa pendekezo la misamaha ya kodi lilikubaliwa lakini Serikali imeshindwa kulitekeleza na pendekezo la kufutilia mbali posho za vikao halikukubaliwa.
Katika taarifa yake, Zitto alisema kuwa Kambi Rasmi ya Upinzani inataka maelezo ya kina ya kwa nini Serikali imeshindwa kutekeleza ahadi yake iliyoitoa bungeni kwamba misamaha ya kodi itapunguzwa mpaka kufikia asilimia moja ya Pato la Taifa. Hivi sasa misamaha ya kodi ni sawa na misaada yote kutoka nchi wahisani, yaani Shilingi 1.03 trillioni ambayo ni sawa na asilimia 3 ya Pato la Taifa, kwa mujibu wa taarifa hiyo.
Kwa upande wa mapato na matumizi katika mwaka wa fedha ujao, kambi hiyo imehoji kuhusu kiasi cha fedha kilichopendekezwa Shilingi 15 trillioni kutoka Shilingi 13 trillioni kuwa kitasaidiaje kukabiliana na changamoto zinazolikabili taifa kwa sasa iwapo kiasi kilichopitishwa na Bunge katika Bajeti inayoisha hakikufanikiwa kukabiliana na changamoto nyingi.
Aidha kambi hiyo pia imependekeza kuelekeza rasilimali fedha kwenye maendeleo vijijini hasa kujenga miundombinu kama barabara za vijijini na umeme vijijini; kuelekeza fedha za kutosha kukarabati Reli ya Kati na kufufua njia za Reli za Tanga, Moshi na Arusha na kushusha Kima cha Chini cha Kodi ya Mapato (PAYE) mpaka asilimia 9 ili kuwezesha wananchi wa hali ya chini kubaki na fedha za kutumia na kukuza uchumi.
Pia Kambi hiyo imependekeza kuongeza mapato ya ndani na kupunguza mikopo ya kibiashara kwa kuhakikisha mapato ya ndani yanafikia asilimia 2 ya Pato la Taifa, kuongeza nguvu za kisheria na udhibiti ili Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) ikusanye mapato zaidi kwenye kampuni za simu na kwenye shughuli za uchimbaji wa madini, mafuta na gesi.
Mapendekezo mengine ni pamoja na kupunguza na kufuta kodi kwenye bidhaa za vyakula kwa muda maalumu ili kushusha mfumuko wa bei; kuweka mfumo mpya wa elimu kwa kushirikisha sekta binafsi katika kutoa elimu kwa ubora zaidi, ikiwemo kuundwa kwa chombo cha udhibiti wa mapendekezo.
Hayo yamekuja wakati serikali tayari imeshatoa mwelekeo na vipaumbele vya bajeti ijayo mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo inatarajia kutumia kiasi cha Shilingi 15 trilioni.
Katika taarifa yake kwa Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk. William Mgimwa alieleza kuwa katika bajeti hiyo matumizi ya kawaida ya Serikali yanatarajiwa kuwa Shilingi 10 trilioni na fedha za maendeleo ni Shilingi 5 trilioni.
Kwa upande wa vipaumbele alisema kuwa kipaumbele cha kwanza katika Bajeti yake ya kwanza tangu kuteuliwa nafasi hiyo ni miundombinu ambayo imegawanywa katika makundi mbalimbali.
Dk. Mgimwa alisema kuwa miundombinu hiyo imegawanyika katika makundi manne ya reli, umeme, maji salama, usafirishaji na uchukuzi ambavyo vimetengewa jumla ya Shilingi 4.5 trilioni.
Vipaumbele vingine vya Serikali ni kilimo, viwanda, rasilimali watu, huduma za jamii, utalii, biashara ya ndani na nje na huduma za fedha.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item