CHADEMA YAKIRI KUFADHILIWA NJE YA NCHI...

Dk. Willibrod Slaa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimekiri kufadhiliwa kutoka nje ya nchi katika shughuli zake za kujijengea uwezo.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema hayo jana katika semina iliyoshirikisha baadhi ya viongozi wa chama hicho na wageni kutoka shirika la Chama cha Kikristo cha Ujerumani (CDU) la Konrad Adenauer Stiftung (KAS).
Kwa mujibu wa Dk Slaa, Chadema na KAS, wamekuwa na ushirikiano wa karibu kwa miaka sita sasa na ushirikiano huo umelenga zaidi kukuza demokrasia nchini.
Dk Slaa alidai kuwa Chadema ni chama chenye uwazi kwa kila mtu na katika uhusiano wao na KAS, hakiletewi fedha moja kwa moja kwa ajili ya operesheni au maandamano, ila kujijenga kiuwezo.
"Kwa sasa kumekuwa na propaganda zinazoenezwa kwamba Chadema wanapata mabilioni ya fedha kutoka kwa wafadhili, hii si kweli, ila wanatujengea uwezo na si kutufadhili kampeni.
"Napenda kusema propaganda za aina hii zimepitwa na wakati na wote watakaozifanya tutawafungulia kesi," alisema Dk Slaa.
"Wanaosema kwamba Chadema wanapokea mabilioni nao wanashirikiana na mashirika ya aina hiyo yenye mrengo mmoja na ni utamaduni duniani kote, vyama vyenye mrengo mmoja kushirikiana, hivyo hii dhana isipotoshwe," alidai.
Pamoja na kusema kuwa KAS haitoi fedha moja kwa moja kwa Chadema kwa ajili ya maandamano na kampeni, lakini Dk Slaa alidai kuwa shirika hilo huwasaidia wastani wa Sh milioni 60 kwa mwaka kwa ajili ya machapisho na kutoa elimu.
Pia alisema kipo chama cha Uholanzi ambacho hakukitaja jina, lakini akakiri kuwa huwafadhili Sh milioni 20 kulingana na idadi ya wabunge walio bungeni.
Pamoja na kusema kuwa ni kawaida kwa vyama vya mrengo mmoja kusaidiana duniani, Dk Slaa alisema chama hicho cha Uholanzi kinachowasaidia, pia hufadhili CCM fedha zaidi ya zinazopelekwa Chadema kutokana na chama hicho tawala kuwa na idadi kubwa ya wabunge.
Dk Slaa alidai kwamba kwa kuanzia wameamua kumshitaki Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.
Kwa mujibu wa madai ya Dk Slaa, tayari Chadema imefungua kesi namba 186 ya mwaka 2012, katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam dhidi Nape, ambaye anadaiwa alitamka Chadema kufadhiliwa kutoka nje.
Dk Slaa alidai kuwa kesi hiyo itakapokuwa ikiendelea, wataongeza watu wengine walioeneza kauli hiyo.
Akizungumzia semina ya kujenga uwezo iliyotolewa jana kwa makada wa Chadema, Dk Slaa alisema imelenga kuangalia wanavyoweza kuleta uchumi wa soko utakaoshirikisha watu walio katika ngazi za juu na chini.
Lengo la kushirikisha watu hao wa tabaka mbalimbali kwa mujibu wa Dk Slaa, ni ili raslimali za nchi zitumike kwa faida ya Watanzania wote ambapo pia mgeni kutoka KAS ambaye alipata kuwa Naibu Waziri wa Uchumi na Maendeleo wa Ujerumani, Klaus-Jurgen Hedrich atatoa mada.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema ili uchumi uwe endelevu, lazima wananchi wapewe haki na kuruhusu sekta binafsi kusimamia uchumi na si rahisi kusimamia uchumi kwa sera za kijamaa.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item