WALIOMWIBIA SHARO MILIONEA AJALINI WAREJESHA VITU KINYEMELA...

Huku msako wa watu waliomvua nguo msanii wa filamu na muziki, marehemu Hussein Ramadhan Mkieti maarufu Sharo Milionea, ukiendelea, vitu kadhaa vya marehemu vimerejeshwa polisi kinyemela na watu waliodai kuwa wameviokota.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Costantine Massawe alisema jana kuwa mali hizo za Sharo Milionea zilisalimishwa kwa nyakati tofauti na watu hao waliosisitiza kwamba wameviokota.
Hata hivyo kwa mujibu wa Kamanda Masawe, kupatikana kwa mali hizo hakutasitisha msako wa watuhumiwa waliomvua nguo na kumpora mali Sharo Milionea bali kumetoa taarifa zilizowasaidia polisi kubaini watuhumiwa wanne.
Kamanda Masawe alisema kwa sasa polisi inawasaka watuhumiwa hao wanne (majina yao yamehifadhiwa) ambao ni wakazi wa Kijiji cha Songa wilayani Muheza kwa  kuhusika na wizi wa mali za marehemu Sharo Milionea.
Alisema watuhumiwa hao ambao ni wanaume wamebainika baada ya msako huo uliofanywa kijijini hapo.
Alisema Polisi kwa kushirikiana na uongozi wa Kijiji cha Songa iliamua kufanya msako wa nguvu kwa lengo la kupata mali za marehemu.
“Usiku ule wa saa 2.30 siku ya Jumatatu marehemu Hussein Ramadhan alipopinduka kwa gari watu wasiojulikana walifika eneo la tukio na kuiba vitu mbalimbali kama betri, redio na tairi la akiba kutoka kwenye gari.
“Lakini hawakuishia hapo kwa sababu walithubutu kumvua marehemu suruali, saa ya mkononi, mkanda wa suruali, viatu na fulana aliyokuwa amevaa na kumwacha akiwa nusu utupu,” alisema RPC.
Akitaja mali hizo Kamanda Masawe alisema; “Lilipatikana begi moja lenye nguo za marehemu ambalo wakati msako unaendelea
lilisalimishwa na mtu mmoja ambaye tumebaini ana uhusiano ya karibu  na mtuhumiwa.”
Alitaja vitu vingine kwamba ni suruali, fulana, mkanda wa suruali, saa ya mkononi aina ya Black Berry, redio, betri na tairi ya akiba.
Kamanda Masawe alisema watuhumiwa hao wanne wanajulikana ingawa hawajakamatwa kwa kuwa walitoroka kijijini hapo baada ya msako kuanza lakini askari wanaendelea na jitihada za kuwakamata ili wafikishwe mahakamani.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item