SPIKA MAKINDA AELEZA ALIVYONYANYASWA KIJINSIA...

Spika Anne Makinda.
Spika wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda amebainisha wazi kuwa amekuwa akifanyiwa ukatili kutokana na jinsi yake wakati akiwania nafasi mbalimbali za uongozi.
Makinda aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akifungua semina ya mabunge hayo, iliyoandaliwa na Chama cha Mabunge Duniani (IPU) kujadili ushiriki wa mabunge katika kupambana na tatizo hilo la ukatili katika nchi za ukanda huo wa Afrika.
Alisema tatizo la ukatili dhidi ya wanawake ni kubwa si tu Tanzania, bali duniani kote na takwimu za sasa zinaonesha kuwa kati ya wanawake wawili, mmoja lazima atakuwa ameathirika na ukatili huo ikiwa ni sawa na zaidi ya asilimia 60 ya wanawake waliofanyiwa ukatili duniani.
“Hili nawaambieni ni tatizo hasa kwetu sisi wanawake, mimi mwenyewe ni mmoja wa waathirika wa ukatili dhidi ya wanawake, na nilinyanyasika kweli hadi nilitamani kulia, ni moyo na ujasiri niliokuwa nao ndio uliniwezesha kuvuka manyanyaso yale,” alisema Makinda.
Alisema alianza kunyanyasika kutokana na jinsi yake wakati akiwania kwa mara ya kwanza nafasi ya ubunge kupitia Jimbo la Njombe Kusini ambapo bila kufafanua zaidi, alisema alinyanyasika sana alivyoingia kwenye kinyang’anyiro hicho kwa takribani miaka minne mfululizo.
“Unajua kipindi kile ndio kwanza uchaguzi wa vyama vingine ulianza kufanyika, hivyo kuingia kwangu kwenye kinyang’anyiro kile kutokana na jinsi yangu ya kuwa mwanamke tu nilinyanyasika hadi nilitamani kulia, ila sasa nawaambia haninyanyasi tena mtu,” alieleza Spika Makinda.
Hata hivyo, alisema bado manyanyaso na ukatili dhidi yake kutokana na jinsi yake yanaendelea hata alipopata nafasi ya Spika, ambapo amekuwa akiandamwa na maneno hasa kutoka vyombo vya habari.
Pamoja na kunyanyaswa kwake, mwanasiasa huyo mkongwe alisema pia kuna tatizo kubwa la ukeketaji, hivyo kushauri, katika mapambano dhidi ya utamaduni huo mbaya, wanaume washirikishwe kwani vijana wa kisasa wakiona uhalisia wa mwanamke aliyekeketwa  hawatoruhusu wenza wao kufanyiwa ukatili huo.
Alisisitiza kwamba kutokana na tatizo la ukatili dhidi ya wanawake katika nchi za Afrika Mashariki, Kusini na Kati, mabunge yana wajibu mkubwa wa kutoishia kutunga sheria na kusimamia Serikali pekee, bali kutafuta mfumo bora utakaowezesha kuhakikisha sheria wanazotunga zinatekelezwa ipasavyo.
“Na hapa ni pamoja na kuhakikisha sheria hizi zinazotungwa na lazima zilenge kuikomboa jamii na ndio sababu hasa ya semina hii ya leo,” alisema Spika huyo wa kwanza mwanamke Tanzania.
Alisema yapo mambo mengi yanayosababisha ukatili wa kijinsia hasa wanawake ikiwemo teknolojia duni na ukosefu wa elimu na hiyo ni kutokana na idadi kubwa ya wanawake ambayo ni sawa na asilimia 50, lakini maisha yao kuwa magumu na wale wakulima kutegemea zaidi jembe la mkono.
“Mimi nina uhakika kama mwanamke angewezeshwa na kutonyanyaswa nchi zilizoendelea nyingi hali yake kiuchumi ingeimarika kwa kuwa wanawake ni wengi na wanajituma zaidi,” alisema.
Hata hivyo, Makinda alizungumzia suala la Tanzania kuendekeza hulka ya maneno zaidi kuliko vitendo hali inayoirudisha nyuma kimaendeleo tofauti na nchi nyingine. “Hebu tuangalie Marekani, walikuwa na maneno mengi wakati wa uchaguzi, ulivyomalizika mnasikia kitu tena zaidi ya masuala ya maendeleo?” Alihoji.
Alisema nchini uchaguzi hata ukikamilika, bado maneno tena mengine yasiyo na maana na kuchekesha yanasikika na si vitendo jambo ambalo linaifanya nchi kuchekwa hadi na nchi za jirani akitolea mfano Kenya.
“Jamani hii hulka ya maneno kweli imezidi nchini, angalieni wenzetu wa Marekani uchaguzi umekwisha na maneno pia sasa wao ni vitendo kwa maendeleo ya nchi, lakini sisi oh my god! (Mungu wangu) miaka mitano mfululizo ni maneno, tukiendelea hivi tutazidi kuathirika kiuchumi,” alibainisha.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item