UHALIFU WAKITHIRI, WANANCHI 138 NA POLISI 6 WAUAWA...

Dk Emmanuel Nchimbi.
Vitendo vya uhalifu na hasa ujambazi wa kutumia silaha, vimeongezeka nchini na kusababisha wananchi kupoteza maisha na mali zao huku askari Polisi wakiuawa na majambazi.
Mbali na kukiri kuongezeka kwa uhalifu, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi ametoa onyo kwa Watanzania wanaomiliki silaha kiholela kuzisalimisha ndani ya siku 30 kuanzia jana.
Dk Nchimbi akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, alionya kuwa baada ya siku hizo 30, ambao watakuwa hawakutii amri, utafanyika msako mkali wa silaha hizo.
Alisema utafiti uliofanyika kuanzia Januari hadi Septemba mwaka huu, ulibaini kutokea kwa matukio 876 ya uhalifu ikiwemo unyang’anyi wa kutumia silaha na kusababisha vifo vya watu 138 na askari Polisi sita.
“Katika muda huo, silaha 62 ziliibiwa ama kunyang’anywa kutoka kwa wamiliki wake halali ambapo pia silaha 304 zilikamatwa katika matukio hayo mbalimbali ya uhalifu,” alisisitiza Dk Nchimbi.
Alisema katika matukio hayo mali zenye thamani ya Sh bilioni 4.5 ziliibwa kwa kutumia silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria zikiwemo zinazomilikiwa kisheria, lakini zinatumika isivyo halali.
“Takwimu zinaonesha kuwa miongoni mwa jamii kuna baadhi ya watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria na isivyo halali, ndio maana natoa mwito kwa mtu au kikundi chochote kinachomiliki silaha kinyume na sheria au isivyo halali, kusalimisha silaha hizo,” alionya.
Alitaja maeneo ambayo watu wanaweza kusamilisha silaha hizo kuwa ni vituo vya Polisi, kwa wenyeviti wa vitongoji/vijiji, watendaji wa kata, taasisi za kidini, wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa na kuahidi kuwa watakaorejesha silaha hizo ndani ya muda hawatochukuliwa hatua zozote za kisheria.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa ifikapo Januari 5, mwakani, kutafanyika operesheni kali nchi nzima ya kuwasaka wote wanaotumia au kumiliki silaha kinyume cha sheria na watakaobainika sheria itachukua mkondo wake.
Alivitaka vyombo vya habari kuisaidia Serikali katika mapambano dhidi ya watu hao wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kwa kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika kuwafichua.
“Katika vita hii, asilimia 90 nawaambia inahitaji sana nguvu ya vyombo vya habari kuliko dola,” alisema.
Kuhusu ushiriki wa baadhi ya askari katika matukio ya uhalifu, Dk Nchimbi alisema suala hilo analifahamu, lakini hawezi kulizungumzia zaidi na kutaka vyombo vya habari kufanya kazi yake ipasavyo.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item