WALIOMSHITAKI GODBLESS LEMA WADAIWA KUTOKUWA NA HAKI...

Godbless Lema.
Mawakili wa aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) waliokata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha uliomuondoa madarakani, wamedai kuwa wanachama wa CCM waliofungua kesi hiyo hawakuwa na haki kisheria ya kufanya hivyo.
Wakili wa Lema, Method Kimomogoro akisaidiana na Tundu Lissu, walidai hayo jana katika Mahakama ya Rufaa, Dar es Salaam wakati wakiwasilisha hoja 18 za kupinga hukumu hiyo iliyomng’oa madarakani Lema.
Wakiwasilisha hoja hizo mbele ya Jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Natalia Kimaro, Bernard Luanda na Salum Massati, mawakili hao walidai kuwa hukumu iliyotolewa haikukidhi vigezo.
Walidai kuwa ushahidi uliotolewa haukuthibitisha mashitaka bila kuacha shaka na Jaji aliegemea ushahidi ambao haukidhi viwango.
Kwa mujibu wa madai hayo, Jaji Gabriel Rwakibarila alitoa hukumu kwa kuegemea ushahidi wa mashahidi 14 ambao haukukidhi viwango, lakini aliendelea kutumia ushahidi wa shahidi wa 11 na 14, wakati awali alidai ushahidi wao haukukidhi viwango.
Wakili Kimomogoro alidai kuwa Jaji alivutiwa na ushahidi wa mashahidi hao kwa sababu ya njia walizotumia kuutoa na siyo kwa sababu ya uzito wa ushahidi.
"Jaji alivutiwa na shahidi wa 11, Amina Ally kwa sababu yeye ni muuza mitumba, kwa hiyo ndiyo ilimvutia mpaka kuona ushahidi wake umejitosheleza," alidai Kimomogoro.
Alidai waliofungua kesi hawana haki kisheria kwa kuwa aliyetukanwa katika kampeni za uchaguzi ni aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk Batilda Burian, na ndiye aliyetakiwa kufungua kesi na siyo kufunguliwa na wanaCCM hao watatu ambao hawakueleza ni jinsi gani ubaguzi na maneno hayo uliathiri haki yao ya kupiga kura.
"Na katika ushahidi wao walidai kuwa, walimshawishi Dk Burian kufungua kesi, lakini yeye alikataa, sasa kwa nini wao walikuja kufungua kesi wakati hakuna haki yao ya kupiga kura ilivunjwa?" Alihoji Wakili Kimomogoro.
Wakili Lissu alidai kuwa hakuna sheria ya uchaguzi inayoeleza matusi na maneno ya udhalilishaji yanaweza kuwa sababu ya kutengua matokeo ya uchaguzi.
Alifafanua kuwa katika Maadili ya Uchaguzi ndiko wanakataza maneno ya ubaguzi, udhalilishaji, maneno ya kashfa na adhabu yake ni faini ya kuanzia Sh 50,000 hadi 150,000.
Aliongeza kuwa Sheria ya Uchaguzi haielezi kama maneno ya ubaguzi ni kosa la jinai, lakini wameeleza kuwa mtu atakayevunja maadili, ataadhibiwa kulingana na adhabu iliyotolewa kulingana na kanuni za maadili.
Lissu alidai kuwa Jaji hakupima ushahidi wa upande wa mashitaka kama waliyathibitisha bila kuacha shaka na pia hawakupeleka vielelezo muhimu ikiwemo CD zilizoonesha Lema akitukana pamoja na Batilda kutotoa ushahidi mahakamani hapo.
Aliongeza kuwa hapakuwa na uthibitisho kama watu walifungua mashitaka ni wapiga kura halali wa Jimbo la Arusha Mjini kwa kuwa hawakuwasilisha vitambulisho vya kupigia kura na Jaji hakupata nakala ya vitambulisho vyao iliyothibitishwa.
Kwa pamoja, mawakili hao waliiomba Mahakama kutengua uamuzi uliomtoa Lema madarakani na upande wa waliowashitaki walipe gharama za uendeshaji wa kesi pamoja na gharama ya mawakili wawili.
Naye Wakili wa Mashitaka ambao ndio wajibu rufani, Alute Mughwai aliiiomba Mahakama kutupilia mbali rufani hiyo kwa kuwa hoja zilizotolewa na upande wa Lema hazitoshelezi kutengua uamuzi wa Mahakama Kuu.
Pia Mughwai ambaye ni ndugu na Lissu, aliiomba Mahakama iwaamuru upande wa kina Lema walipe gharama za kesi pamoja na mawakili.
Alidai kuwa hapakuwa na ushahidi wa mazingira kwa kuwa mashahidi walidai walimuona na kumsikia Lema akitoa maneno ya ubaguzi na ushahidi wa shahidi mmoja uliungwa mkono na mashahidi wengine.
Baada ya kusikiliza hoja hizo, majaji hao watatu wameeleza kuwa watatoa notisi ya tarehe ya hukumu; huku Lema akiwaomba wafuasi wake kuwa watulivu na kusubiri siku hiyo muhimu kwao.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item