ALIYEMTEKA DK ULIMBOKA AMTAKA BALOZI WA KENYA KORTINI...

Dk Stephen Ulimboka.
Raia wa Kenya, Joshua Mulundi (21) anayekabiliwa na mashitaka ya kumteka na kutaka kumuua Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Stephen Ulimboka, ameiomba Mahakama kumleta Balozi wa nchi yake mahakamani.
Mulundi alitoa ombi hilo jana mbele ya Hakimu Agnes Mchome wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya upande wa mashitaka kudai kuwa upelelezi wa kesi yake bado haujakamilika.
Alihoji kwa nini upelelezi wa kesi hiyo unachelewa kukamilika na kwa nini upande wa mashitaka hawaleti mashahidi mahakamani ili kesi hiyo iishe?
Hakimu Mchome alisema jambo hilo liko nje ya  uwezo wa Mahakama hiyo kwa kuwa haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, isipokuwa Mahakama Kuu.
Mulundi aliiomba Mahakama kushinikiza Balozi wa Kenya aende mahakamani, huku akidai ameshaanza mgomo mahabusu na ataendelea nao. Hakimu Mchome alisema Mahakama hiyo haina uwezo wa kumshinikiza balozi wa nchi yake kufika mahakamani, lakini anaweza kufuata utaratibu kwa yeye kumuandikia Balozi  wake barua.
Hata hivyo Mulundi hakuridhika na majibu hayo na kuomba apelekwe kwa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ilvin Mugeta ili akawasilishe malalamiko.
Alitolewa katika chumba cha Hakimu Mchome na kupelekwa ofisini kwa Hakimu Mugeta ambako alidai upelelezi wa kesi yake unacheleweshwa.
Hata hivyo Hakimu Mugeta alisema Mahakama haina uwezo wa kuharakisha Polisi kukamilisha upelelezi kwa sababu kesi hiyo iko chini ya Polisi. 
Hakimu Mchome ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 23 mwaka huu itakapotajwa tena. Upande wa mashitaka uliwasilishwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka.
Alipotoka mahakamani, Mulundi alikuwa anachechemea hasa mguu wa kushoto kitu ambacho kilisababisha ashuke kwa taabu katika ngazi za Mahakama. Pia alionesha sura ya huzuni, lakini  Ofisa Magereza waliokuwa naye walishangaa na kudai alitoka mahabusu akitembea vizuri.
Inadaiwa kuwa, Juni 26 mwaka jana, katika eneo la Leaders Club, Mulundi alimteka Dk Ulimboka.
Katika shitaka la pili anadaiwa Juni 26 mwaka jana, akiwa katika eneo la Msitu wa Mabwepande Tegeta, Dar es Salaam,  kinyume cha sheria inadaiwa alijaribu kumsababishia kifo Dk Ulimboka. Kwa mara ya kwanza mshitakiwa huyo alipandishwa kizimbani mahakamani hapo Julai 13 mwaka jana.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item