MABASI YAGONGANA BUNDA NA KUUA WATU SABA...

Kamanda Absalom Mwakyoma.
Watu saba wamekufa na wengine 47 kujeruhiwa baada ya mabasi mawili waliyokuwa wakisafiria kugongana eneo la Nyatwali wilayani hapa kwenye barabara kuu ya Musoma - Mwanza.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Absalom Mwakyoma aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa ajali hiyo ilitokea juzi saa 11 jioni ikihusisha mabasi ya Mwanza Coach namba T 736AWJ lililokuwa likitoka Musoma kwenda Mwanza na basi la Best Line namba T535 AJR likitoka Mwanza kwenda Tarime.
Kamanda Mwakyoma alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa mabasi hayo huku akiapa kuwachukulia hatua madereva ambao hata hivyo walitoroka baada ya tukio hilo.
Alisema watu sita walipoteza maisha papo hapo huku mwingine akifia Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda (BDDH).
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk Rainer Kapinga alitaja waliokufa na kutambuliwa na ndugu zao kuwa ni Robert Manyiri (64) wa Butiama; Grace Mlemwa (50) wa Musoma; Magori Ibrahim na Amina Juma na kwamba maiti wengine watatu hawajatambuliwa na miili yao imehifadhiwa hospitalini hapo.
Aidha, Dk Kapinga alisema majeruhi wanane kati ya 47 waliopokewa BDDH wamehamishiwa katika hospitali ya rufaa ya Bugando, Mwanza kwa matibabu zaidi.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Joshua Mirumbe aliyefika eneo la tukio mapema, jana aliwaasa watumiaji wa barabara hiyo inayotengenezwa kuwa makini wanapoendesha magari yao kwa kuwa imejaa vumbi inayosabababisha madereva kutoona vizuri.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item