RADI YAUA MWANAFUNZI WA SEKONDARI TARIME...
https://roztoday.blogspot.com/2013/01/radi-yaua-mwanafunzi-wa-sekondari-tarime.html
Kamanda Justus Kamugisha. |
Watu wawili wamekufa katika matukio mawili tofauti wilayani Tarime, mkoani Mara, akiwemo mwanafunzi wa Sekondari aliyekufa baada ya kupigwa na radi.
Vifo vya watu hao vimethibitishwa na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Kipolisi ya Tarime na Rorya, Justus Kamugisha.
Alisema katika tukio la kwanza lilitokea juzi majira ya saa 10 jioni katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Rebu iliyoko katika katika kata ya Turwa, tarafa ya Inchage, wilayani hapa, mwanafunzi wa kidato cha pili, Marwa Chacha Homaye alipigwa radi na kupoteza maisha wakati akitibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime.
Alisema kuwa katika tukio hilo mtu mwingine, James Homaye (46), alijeruhiwa vibaya na radi hiyo na amelazwa katika hospitali hiyo ya wilaya.
Katika tukio la pili, mwanaume mmoja, Masele Magumba (44), mkazi wa wilayani Bariadi mkoani Simiyu, alikutwa akiwa amekufa karibu na nyumba yake, baada ya kukatwa panga mwili mzima.
Alisema kuwa mwanaume huyo inadaiwa aliuawa na mtu aliyetajwa kwa jina moja la Nindwa anayesadikiwa alikuwa rafiki wa karibu wa marehemu.
“Mtuhumiwa huyo alikuwa rafiki wa karibu wa marehemu na walikuwa wakilala nyumba moja, sasa chanzo cha tukio hilo ni pale mtuhumiwa alipomdai marehemu shilingi 60,000 ambazo zilikuwa ni ujira wao baada ya kupalilia shamba la miti,” alisema Kamanda Kamugisha na kutaja shamba hilo la miti kuwa ni mali ya Masero Ryoba, mkazi wa kijiji cha Mgena wilayani hapa.