WALIOKUFA AJALI YA BOTI ZIWA TANGANYIKA WATAMBULIWA...


Imethibitika kuwa watu tisa wamekufa na wengine 12 hawajulikani waliko huku wengine 64 wakiokolewa baada ya boti ya abiria waliyokuwa wakisafiria katika Ziwa Tanganyika kuzama baada ya kukumbwa na dhoruba.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kigoma, Fraiser Kashai aliyekwenda eneo la tukio, alithibitisha jana mjini hapa, kwamba boti hiyo iitwayo Tunusuru Yarabi iliyokuwa ikitoka Kirando, Rukwa kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kupitia Rumonge, Burundi, ilikuwa na shehena ya dagaa, vyakula na bidhaa za viwandani.
Kamanda Kashai alisema hadi jana mchana miili ya watu wanane kati ya tisa iliyokuwa imeopolewa ilikuwa imetambuliwa na kati yao, saba ikiwa ya wanawake na miwili ya watoto wa kiume ambayo imehifadhiwa katika hospitali ya mkoa ya Maweni.
Aliwataja marehemu hao kuwa ni Shani Baba wa Kirand, Mzinga Kandoro, Mwalimu wa Shule ya Msingi Filbert Bayi ya Dar es Salaam, Wamjini kutoka Burundi na Sarah Joseph wa Karundu, Nkasi,  Rukwa.
Wengine ni Nuru Hassan wa Kirando, Rukwa; Sewa Seba wa Karungu, Rukwa; Shadrack Amnyasi wa Malindi, Rukwa, na mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja la Asha, mkazi wa  mjini hapa. Mwingine hakuwa ametambuliwa hadi jana.
Akizungumza mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kigoma chini ya Mwenyekiti wake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Issa  Machibya, nahodha wa boti hiyo  Akilimali Seif na baadhi ya abiria walionusurika ajalini, walisema boti hiyo ilizama baada ya kupigwa na wimbi kali ikapasuka na kuzama.
Nahodha huyo alisema boti yake haikuwa na hitilafu za kiufundi au mbovu, bali wimbi kubwa walilokumbana nalo ndilo lilisababisha kuzama na kusababisha vifo hivyo.
Alisema baada ya kupigwa na wimbi la kwanza, injini ilizima na wakati akifanya jitihada za kuwasha mashine nyingine alizidi kupigwa na dhoruba na ikapasuka vipande na kuzama.
Baadhi ya abiria walionusurika waliokuwa wakisafiri kwa boti hiyo, Mariam Saidi na Mohammed Shaaban walisema pamoja na dhoruba kusababisha ajali hiyo, shehena kubwa ya vitu mbalimbali vilivyokuwa vimebebwa katika boti hiyo vilichangia kuzama.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Herembe,  Jack  Mpapi alisema jitihada za wananchi wa kijiji hicho katika uokoaji hazikufanikiwa kutokana na hali mbaya ya hewa na mawimbi makubwa yaliyokuwa ziwani wakati huo.
Machibya na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na wilaya ambao walifika eneo la tukio walitoa pole kwa walionusurika katika ajali hiyo.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa alilaumu upakiaji wa mizigo kupita kiasi unaofanywa na boti hizo na inapotokea dhoruba inakuwa kazi kubwa kuokoka.
Sambamba na hilo, Mkuu wa Mkoa aliwataka wamiliki na waendeshaji wa vyombo vya majini kuzingatia hali ya hewa na dalili zake na kuchukua hadhari katika kuepuka majanga kama hayo.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item